loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dk Mwinyi aanza kupokea kero kielektroniki

WADAU wa maendeleo wakiwemo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesema

uamuzi wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kuzindua mtandao wa mawasiliano ya kielektroniki kupokea kero za wananchi, utaongeza uwajibikaji wa viongozi.

 

Mwakilishi wa Bumbwini, Mtumwa Peya alisema jana kuwa mfumo ni mzuri kwa sababu utawawezesha wananchi kuwasilisha kero na maoni kwa Rais hivyo kuinua mwamko kwa wizara na taasisi kuwajibika ipasavyo.

 

“Unajua Rais hawezi kuonana na wananchi wote kila mmoja, kwa hiyo huu mfumo utamuwezesha kupata maoni mengi kwa wakati mmoja. Taasisi na wizara sasa zitaacha kuzembea na kuwajibika kwa kuogopa kutajwa kila mara,”alisema Peya.

 

Pia alisema kazi ya wawakilishi itakuwa rahisi, kwa kuwa kupitia mfumo huo watajua kero na malalamiko ya wananchi ikiwemo pia kuwasilisha kero na malalamiko hayo kupitia mfumo huo.

 

Mwakilishi wa Jimbo la Shaurimoyo, Hamza Hassan Juma alisema alichofanya Dk Mwinyi ni sehemu ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuzipatia ufumbuzi kero zinazowakabili wananchi.

 

Mwakilishi wa Kuteuliwa, Juma Ali Khatib alisema, alisema alichokifanya Dk Mwinyi ni sahihi 

 

Mchambuzi wa Siasa,  David Kafulila alisema jana kuwa uwajibikaji wa viongozi utaongezeka kwa sababu watendaji wazembe na wasio waaminifu, watahofu kuwa udhaifu wao utafahamika kirahisi kwa sababu ya matumizi makubwa ya simu na intaneti.

 

“Utaratibu huo ukisimamiwa kikamilifu na wananchi wakapewa taarifa za kero walizowasilisha itaongeza zaidi imani ya umma kwa serikali yao kuwamtu yeyote bila kujali nafasi yake na bila urasimu anayo nafasi ya kutoa kero au maoni yake kumfikia Rais pasipo urasimu”alisema Kafulila.

 

Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) Zanzibar, Mzuri Issa alisema mfumo huo wa ukusanyaji maoni kwa njia ya kieletroniki ni muhimu kwa kuwa unakuwa kiungo cha mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wananchi na kiongozi wao.

 

Alisema awali wananchi walikuwa wakisikia kila kitu kutoka kwa viongozi kupitia hotuba na matukio na kwamba hawakuwa na njia ya moja kwa moja ya kuwasiliana na viongozi wao.

“Hii ni tija muhimu kwa wananchi, sasa wanapata fursa ya kuhoji na kutoa maoni yao. Mfumo huu utachochea maendeleo, utendaji na uwajibikaji lakini pia utaondoa ukandamizi kwa wananchi,” alisema Issa.

Wakati akizindua mfumo huo, Dk Mwinyi alisema amedhamiria kuwatumikia wananchi na yupo tayari kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili ili kuleta mabadiliko makubwa serikalini.

Mtandao huo wa mawasiliano unaojulikana kwa jina la “Sema na Rais Mwinyi SNRMWINYI” umeanzishwa kwa lengo la kuwawezesha wananchi kutoa taarifa kwa Dk Mwinyi, yakiwemo malalamiko dhidi ya watumishi wa serikali.

Dk Mwinyi alisema mfumo huo utaonesha mtumishi gani kutoka taasisi ipi asiyewajibika kikamilifu katika kutoa huduma kwa wananchi.

Alisema katika kipindi kifupi tangu kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, katika sehemu anazopita wananchi wamekuwa na hamu na shauku ya kutaka kuwasilisha malalamiko zikiwemo taarifa kuhusu watendaji wa serikali na taasisi zake kwa ujumla.

“Nilipokuwa nikiomba kura katika kipindi cha kampeni niliyafikia makundi mengi na kutoa ahadi zangu kwao...yapo malalamiko kwa taasisi zetu ambazo hazifanyi kazi kwa wananchi sasa mfumo huu utatuonesha nani asiyewajika na katika maeneo gani”alisema Dk Mwinyi.

Mapema Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Zena Ahmed Said aliwataka watumishi wa umma, wawajibike kwa mujibu wa sheria ili kukidhi matarajio ya serikali ya Dk Mwinyi.

Alisema mfumo huo wa kielektroniki, kwa kiasi kikubwa utawalenga watumishi wa umma ambao wamekabidhiwa majukumu na serikali ya kuwatumikia wananchi.

Zena alisema anatarajia kuwa mfumo huo, utaongeza ari kwa watumishi wa umma kufanya kazi na kuwajibika ili kufikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Nane.

“Uzinduzi wa mfumo huu kwa kiasi kikubwa utatusaidia sisi viongozi kujua kwa upande wa watumishi wa umma nani asiyewajibika na kuweza kuchukuwa hatua za kisheria”alisema.

Zena alisema, katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane, suala la uwajibikaji kwa watumishi wa umma, mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu wa uchumi ni miongoni mwa mambo yaliyopewa kipaumbele cha kwanza.

Alisema katika siku 100 za kwanza tangu Dk Mwinyi aingie madarakani yamepatikana mafanikio mengi.

“Katika kipindi cha siku mia moja za Rais Dk Mwinyi kuwepo madarakani mafanikio mengi yamepatikana ikiwemo kurudisha nidhamu kwa watumishi wa umma na kujenga uaminifu katika sekta ya fedha”alisema.

Mapema Mkurugenzi wa kampuni ya RAHISI, Abdurahman Hassan alisema huo ni mfumo unaotumika katika bara la Afrika kuwawezesha viongozi wakuu kukusanya taarifa za malalamiko yanayotolewa na wananchi na kuyafanyia kazi.

Kwa mfano alisema wasimamizi wakuu wa mfumo huo ni makatibu wakuu na mawaziri hivyo watapokea malalamiko ya wananchi na kumfukishia Rais na yeye atajua namna ya kuyashughulikia.

“Katika mfumo huu wananchi wataweza kutumia simu za kisasa na zile za kawaida za tochi kwa kutumia nambari ya 07772-444449 kupitia tovuti ya www.snrmwinyi.co.tz'alisema.”alisema Hassan.

 

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Zanzibar

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi