loader
Dstv Habarileo  Mobile
Benki ya Afrika yasifu uthubutu wa JPM kupaisha uchumi

Benki ya Afrika yasifu uthubutu wa JPM kupaisha uchumi

BENKI ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imepongeza uthubutu wa Rais John Magufuli, ulioiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi yenye uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika, licha ya janga la kusambaa kwa virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Aidha, alimsifu Rais Magufuli kwa kuwa kiongozi anayetenda zaidi, hasa linapokuwa suala linalohusu utekelezaji miradi.

Rais wa AfDB, Dk Akinwumi Adesina, alitoa pongezi hizo katika salamu fupi kuhusu uimara wa uchumi wa Tanzania na pongezi kwa Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka jana.

“Kwanza napenda kumpongeza Rais John Magufuli kwa kuchaguliwa tena. Kuchaguliwa huko kuwa Rais tena wa Tanzania ni fursa nzuri ya kuendelea kujenga Tanzania yenye mafanikio makubwa,” alisema Dk Adesina.

Aliwataka viongozi wengine barani Afrika, watambue kuwa Rais Magufuli ni mtu wa kuchukua hatua, hasa linapokuja suala la utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa wananchi.

“Labda niwatahadharishe jambo, Rais Magufuli ni mtendaji. Sasa hivi ukizungumzia suala la miradi haipunguki kwake, ni mtu mwenye kasi, humaliza miradi hii na kuanza mingine,” alisema Dk Adesina.

Hivi karibuni akizungumzia mkutano wa wadau wa maendeleo na wawekezaji uliofanyika jijini Dar es Salaam, alisema Rais Magufuli na Ofisi yake ya Uwekezaji chini ya Waziri wa Nchi, Profesa Kitila Mkumbo inafanya mambo makubwa na kuwahusisha wadau wa maendeleo.

 

“Pili nawapongeza waandaji wa mkutano huu kwa kuandaa jukwaa kwa wadau wa maendeleo na wawekezaji kupata fursa nyingi za uwekezaji zilizopo Tanzania hivyo wadau hao walikuja wakati muafaka na sehemu sahihi ambayo ni Tanzania” alisema.

Kuhusu ukuaji wa uchumi wa Tanzania, Dk Adesina alisema Tanzania ilifanikiwa katika ukuaji wa Pato la Taifa (DGP) la asilimia 6.9 mwaka 2019.

"Wakati ukuaji wa uchumi uliposhuka barani Afrika hadi asilimia -2.1 mwaka 2020 kutokana na janga la Covid-19 ambalo sote tunapambana nalo, Tanzania bado imeweza kurekodi ukuaji wa asilimia 2.1, hilo ni jambo kubwa sana. Sasa kuna mwanga unaangaza mwisho mwa handaki. Benki ya Maendeleo ya Afrika ilitabiri kuimarika kwa uchumi wa Tanzania mwaka 2021,” alisema.

Ukuaji halisi wa Pato la Taifa, unatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 4.1 mwaka 2021 na utaongezeka mpaka asilimia 5.8 mwaka 2022. Alisema Tanzania ni nchi inayostahimili na yenye misingi madhubuti ya uchumi.

“Ebu fikiria kuhusu hili, mwaka jana Tanzania imekuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati, miaka mitano kabla ya malengo ya kufika huko. Huu ndio uongozi,” alisema Dk Adesina.

Alisema uchumi wa Tanzania ni kielelezo dhahiri wa maelezo ya nini maana ya uchumi unaostawi na wenye nguvu.

“Pamoja na ukuaji wa asilimia 17.4 katika sekta ya ujenzi; asilimia 8.8 katika sekta ya uchukuzi; na asilimia 6.7 katika sekta ya kilimo, Tanzania imekuwa ikifanya maboresho ya kibiashara na kanuni na sheria zake na kuleta matunda thabiti katika miaka kadhaa iliyopita hatua inayostahili pongezi,” alisema Dk Adesina.

Alisema wawekezaji wanahitaji uhakika wa ulinzi wa biashara zao, uwezeshwaji na mazingira mazuri ya sheria za biashara yanayolindwa na uthabiti na utulivu wa Serikali, utekelezaji wa sheria na dhamira ya Serikali, uwazi na uwajibikaji,” alisema Rais huyo wa AfDB.  

Dk Adesina alisema Tanzania imejipambanua katika dhamira ya dhati kwa uwazi, uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa. “Hapa ndipo mahali sahihi pa kuwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na aliyewahi kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe na Mbunge wa zamani, David Kafulila, alisema pongezi hizo za AfDB ni matokoe ya uongozi thabiti wa Rais Magufuli.

“Hii ni kuidhinishwa kwa Rais Magufuli kuwa mtu wa namna gani na ni sifa kwa taifa letu kutoka kwa taasisi yenye sifa nzuri na inayoaminika duniani,” alisema Kafulila.

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi