loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Yanga yageukia ukarabati jengo

KLABU ya soka ya Yanga imetangaza kuanza rasmi ukarabati wa jengo lake lililopo mtaa wa Mafia na Jangwani, Dar es Salaam ambalo ndio makao yake makuu.

Akizungumza na vyombo vya habari jana Makao Makuu ya klabu hiyo, Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla alisema ukarabati huo utafanywa na wanayanga wenyewe kupitia michango yao kwenye vikundi na matawi mbalimbali ya klabu hiyo.

''Yanga tuna timu nne, gharama za kuweka timu kambini kwa maana ya kulipia hoteli ni kubwa sana, tukishakarabati jengo letu timu zetu za U-17, U-20 na Yanga Princess zitakuwa zinakaa kwenye jengo letu zinapokuwa na mashindano,'' alisema Msolla.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa tawi la klabu hiyo la Lite, Eliti Ebete ambaye tawi lake ndio limefanya ukarabati wa kupaka rangi jengo hilo alisema baada ya kumaliza kupaka rangi kinachofuata hivi sasa ni kukarabati vyumba ndani na kuviweka katika mazingira bora yatakayompa mchezaji ari ya kuipambania timu yao.

Aliyataka matawi mengine ya Yanga kujitolea kuipendezesha klabu yao ikiwamo kukarabati vyumba pamoja na kununua samani za ndani ambazo ni  rafiki kwa wachezaji.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu wa Yanga,  Injinia Bahati Museba alisema gharama ya kukarabati kila chumba kimoja kwenye jengo hilo ni Sh milioni 6, ambacho ndani yake kitakuwa na vitanda viwili seti ya runinga, jokofu na choo cha ndani.

Alisema baada ya tathmini yao wao kama kamati walijitolea kutengeneza chumba kimoja cha mfano ambacho kimegharimu kiasi hicho cha fedha na kwamba mbali ya vyumba, pia watafanya ukarabati wa vitu vingine ikiwamo bwawa la kuogelea.

Akizungumza kuhusu mashabiki na wanachama, Dk Msolla alisema hiyo ni fursa pekee kwa makundi mbalimbali ya klabu hiyo kujitolea kukarabati vyumba hivyo ili kuisaidia klabu kupunguza baadhi ya gharama.

Alisema mpaka sasa baadhi ya watu wamejitokeza na kutoa kiasi hicho cha fedha ili kukarabati vyumba hivyo na katika kutambua mchango wa kila atayesaidia ukarabati wa chuma kimoja chumba hicho kitaandikwa jina lake mlangoni.

Aidha, Dk Msolla alisema hivi karibuni ujenzi wa uwanja wao wa Kaunda unatarajiwa kuanza rasmi lengo ni timu zao za vijana pamoja na ya wanawake kufanyia mazoezi hapo, huku wakisubiri kukamilika uwanja wao wa kisasa Kigamboni.

Hii si mara ya kwanza kwa Yanga kufanya ukarabati wa jengo hilo na kuweka vitanda vyumbani, ilishawahi kufanyika hivyo enzi za Mwenyekiti Yusuph Manji, lakini pamoja na kukarabatiwa na kuwekewa samani, timu haikuwa ikikaa hapo na badala yake ilitafutiwa hoteli za kifahari. 

KLABU ya soka ya Simba imeingia mkataba ...

foto
Mwandishi: Mohamed Akida

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi