loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Urasimishaji wa bandari bubu   unaboresha mapato, usalama

URASIMISHAJI wa vyombo vya majini na bandari ambazo haziniwa rasmi katika Ziwa Victoria unatajwa kuwa njia bora ya kukuza mapato ya Serikali kwa kuweka mazingira salama kwa wananchi wanaosafiri na wanaotumia vyombo hivyo kwa ajili ya shughuli za kibiashara ikiwemo usafirishaji mizigo.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imepewa majukumu makubwa yanatokana na sheria ya Bunge iliyoanzisha TPA. Sheria namba 17 ya mwaka 2004 inasema kwamba kazi za TPA ni kuhakikisha inajenga, kuendeleza na kusimamia bandari zote nchini.

Kwenye moja ya mahojiano aliyowahi kufanyaMkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko, alisema kuwa eneo lolote lile ambalo chombo cha majini kinakwenda kwa lengo la kufanya biashara, kubeba abiria au kwa sababu ya kujihifadhi dhidi ya upepo mkali, basi eneo hilo huitwa bandari.

Alisema, “Hivyo, TPA inaangalia mahali kokote ambako vyombo vya majini vinakwenda na kusimama kwa ajili ya biashara au shughuli nyingine.”

Katika kuhakikisha kuwa Serikali inapata pato halali, TPA imekuwa ikishirikiana na wadau wengine likiwemo Shirika la Uwakala wa Meli nchini (TASAC) katika usimamizi wa vyombo vinavyofanya shughuli zinazokuza uchumi.

Katika eneo la Ziwa Victoria, TPA na TASAC wameshirikiana kwenye mambo kadhaa na miongoni mwa hayo ni uimarishaji miundombinu na utoaji elimu kwa wote wanaonufaika na usafiri wa majini na kuhakikisha bandari ‘bubu’ zinakuwa rasmi.

URASIMISHAJI BANDARI

Kakoko alisema katika mahojiano na gazeti hili kwamba moja ya jukumu la TPA ni kujenga na kuendeleza bandari kwenye eneo la bahari nchini kuanzia eneo la kaskazini ambako Tanzania inapakana na Kenya hadi kusini inakopakana na Msumbuji. Pia kwenye maziwa yote hasa yale ya Ziwa Victoria, Tanganyika, Nyasa na kwenye mito.

Mkurugenzi huyo Mkuu alisema kazi nyingine ya TPA ni kushirikiana na taasisi zingine za umma au sekta binafsi kuendeleza bandari nchini na hivyo hata bandari ndogo ndogo ambazo zilikuwa siyo rasmi, TPA ilikuwa inajipanga kuzirasimisha.

Alisema kwamba wakati mwingine wanaoanzisha bandari hizi zisizo rasmi ni taasisi za umma lakini nao unakuta hawana uelewa kuhusu sheria inasema nini kuhusu bandari.

“Pamoja na kujenga na kufanya matengenezo au kushirikiana na wawekezaji wengine, TPA tuna kazi pia ya kuendesha shughuli za kibandari. Yaani, bila kupitia kwa mtu mwingine, tunapokea meli, tunazileta bandarini, tunazifunga, tunaanza kupakia mizigo au kupakua pamoja na kutunza shehena tukisaidiana na wadau wengine,” alisema.

BANDARI BUBU ZIWA VICTORIA

Meneja wa zamani wa Bandari za Ziwa Victoria, Morris Mchindiuza, aliwahi kuliambia gazeti hili kwamba moja ya changamoto wanazokutana nazo ni ziwa hilo kuwa utitiri wa bandari binafsi au bandari ‘bubu’.

“Licha ya sheria kueleza waziwazi kwamba TPA ndio pekee yenye mamlaka ya kusimamia bandari, lakini kumekuwa na changamoto kidogo kwa baadhi ya halmashauri kuelewa na kusaidia TPA katika kutekeleza sheria hii ya Bunge (17/2004),” alisema.

Alisema katika kupambana na tatizo hilo wamekuwa wakitoa elimu kwani baadhi ya watu hawana kabisa uelewa huo.

“Tulianza kufanya mikutano na wakuu wote wa mikoa mitano inayozunguka Ziwa Victoria (Mara, Mwanza, Kagera, Simiyu na Geita), kwa kuwaeleza  juu ya hii sheria na pia tumekutana na wakuu wa wilaya zote ambazo ziko pembezani mwa Ziwa pamoja na wakurugenzi wa halamshauri zote,” alisema.

Alisema athari za bandari hizo binafsi ni pamoja na kuikosesha serikali mapato na kupitisha vitu hatarishi kwa usalama wa taifa.

“Tunajua sote kwamba serikali inapata mapato kwa ajili ya kuhudumia wananchi kutoka vyanzo mbalimbali. Hiki ni chanzo pia cha mapato ya serikali kuu. Sasa utakuta kwa kuwa wao wanaendesha bandari hizi katika utaratibu ambao si wa kisheria, kunakuwa hakuna vyombo sahihi vya serikali kwa ajili ya kukusanya mapato,” anasema.

 USAJILI WA VYOMBO, KUONGEZA USALAMA WA MIZIGO

Ofisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli nchini (TASAC) mkoani Geita Rashid Katonga anaeleza kuwa wamiliki wa boti wanapaswa kusajili boti zao ili ziweze kupa kibali cha kuendesha shughuli za kiuchumi kwenye mazingira salama.

Kwa mujibu wa Afisa huyo anasema kuwa mkoa wa Geita wenyewe unakadiriwa kuwa na zaidi ya boti 1000 zinazotoa huduma ya usafirishaji wa watu na mizigo katika Ziwa Victoria.

Anasema boti 750 zikiwemo za uvuvi pamoja na zinazosafirisha abiria na mizigo ndizo zimesajiliwa na hivyo kufanya kazi zake kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria na mapato na tozo mbalimbali za Serikali zinapatikana.

MIUNDOMBINU RAFIKI BANDARI NDOGO 

Katika Mialo ya Nkome, Mchangani na Makatani wilayani Geita ambapo shughuli mbalimbali za kibashara zinafanyika na huduma kutolewa, kumeonekana kuwa uboreshaji wa miundombinu ya bandari ndogo au urasimishaji wa bandari ‘bubu’ utasaidia kukuza pato la taifa.

Katonga anasema kuwa kama kwao kama TASAC wanahakikisha urasimishaji wa vyombo vya majini vinafanyika ili kuipa nafasi TPA kuandaa miundombinu rafiki vya vyombo kufanya shughuli za usafirishaji ulio halali.

“Kumekuwepo bandari bubu nyingi, kwa kutambua hilo tunaboresha usalama kwa kusajili boti na vyombo vingine kwa kuangalia iwapo vimekidhi vigezo vya usalama vya kuwa majini yaani kubeba abiria au mizigo.

“Kisha tutairahisishia TPA kwenye kutoza pale wanapoenda kwenye bandari zilizo rasmi ambapo upakiaji na ushushaji wa mizigo utafanyika,” anasema   

BILIONI 4.2 ZATENGWA USALAMA MAJINI

Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Emmanuel Ndomba anasema, “Si Serikali wala mwananchi anaweza kunufuaka na biashara zinazosafirisha kwenye maji yawe ya ziwa au bahari bila ya kuzingatia usalama wa chombo na usalama wa wale wanaosafiri.”

Mkurugenzi huyo anabainisha kuwa Serikali kwa kuona umuhimu wa usalama majini na kwa kutambua uchumi utokanao na Ziwa Victoria, imewekeza Sh bilioni 4.2 kwaajili ya kujengwa vituo sita kati ya kumi vitakakuwa vikitumika katika shughuli za ufuatiliaji na uokoaji katika Ziwa Victoria.

Anasema ujenzi wa vituo hivyo utaanza katika mwaka huu wa fedha katika maeneo ya Mwibara, Kakukuru, Nansio, Mwigobero, Ilemela (Makao Makuu) na Magarini.

Anasema kuwa lengo lake ni kuona kuwa wanaotumia vyombo hivyo kibiashara wanakuwa salama lakini pia kutoa nafasi kwa TPA kukusanya vyema mapato kupitia bandari ramsi zinazokuwa kwenye mwambao wa ziwa hilo.

SERIKALI YATOA NENO

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, aluiwahi kukiri uwepo wa bandari binafsi nyingi Mwanza, lakini akasema mchakato wa kuona bandari hizo zinasimamiwa kisheria chini ya TPA umeshaanza.

“Kwa vile mchakato umeshaanza, matumaini yangu ni kwamba muda si mrefu tutafanikisha hili,” anasema.

 

 

 

 

 

Swali: Nia ya kufunga ...

foto
Mwandishi: Alfred Lasteck

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi