loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Unataka ufadhili wa masomo? Hii inakufaa

SAMBAMBA na kutekeleza ilani ya CCM na maono ya Rais John Magufuili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimeungana na vyuo vingine vikubwa duniani kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kwa kuzingatia viwango vya juu vya ufaulu wao.

Ufadhili huu si mkopo kama unaotolewa na Bodi ya Mikopo Tanzania, bali mnufaika hatolazimika kurudisha gharama yoyote baada ya kuhitimu masomo yake.

 

Kwa hatua hiyo, UDSM ni chuo cha kwanza nchini kuja na mpango huo kati ya vyuo vyote vilivyopo, japo ufadhili kama huo umekuwa ukitolewa na vyuo mbalimbali ughaibuni.

 

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye, anasema ufadhili kwa wanafunzi wenye ufaulu wa juu katika masomo ni utaratibu wa vyuo vikuu vingi maarufu duniani.

 

Anasema kuna wanazuoni wengi nchini walionufaika wa utaratibu kama huo, hasa waliosoma katika nchi za Marekani, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani na nyinginezo na hivyo UDSM imepania pia kuwanufaisha Watanzania kupitia utaratibu kama huo.

 

“Kwanza, kwa umri wetu kama taasisi ya elimu ya juu tunaanza huu utaratibu tukiwa tumechelewa sana. Hata hivyo, Waswahili wana msemo maarufu wa ‘kawia ufike’. Hatimaye katika hili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimefika,” anasema.

 

Profesa Anangisye anasema wazo hilo lilizaa andiko ambalo lilipitishwa na kuidhinishwa na vikao rasmi vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuanza kutumika rasmi kuanzia mwaka wa masomo wa 2019/2020 kwa ushirikiano wa menejimenti na watendaji wake katika vyuo vishiriki, ndaki, shule kuu na idara.

 

Anasema wanufaika wa ufadhili huo unaotolewa na UDSM uko katika makundi mawili ambayo ni ‘UDSM Merit Scholarships’ na ‘International Kiswahili Scholarships’.

 

Anasema UDSM Merit Scholarships ni ufadhili unaoligusa kundi la vijana wa Kitanzania wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi ya kidato cha sita na watakaohusika ni wale wanaojiunga na shahada za awali.

Anasema vijana wa kitanzania wenye ufaulu wa juu katika shahada za awali na watakaochaguliwa kujiunga na shahada za uzamili, hasa za umahiri watapata pia ufadhili huo.

 

 

Kuhusu ufadhili wa kundi la International Kiswahili Scholarships, Makamu Mkuu wa Chuo anasema unalenga kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza Kiswahili Kimataifa na kwamba International Kiswahili Scholarships inatolewa kwa wanafunzi kutoka nchi za Kiafrika.

 

“Ufadhili huu ni kwa wanafunzi wanaotaka kusoma masomo ya umahiri katika Kiswahili. Katika mwaka huu wa masomo chuo kimetoa ufadhili kwa wanafunzi watatu ambao ni Julius Matovu kutoka Uganda, Daniel Kotey kutoka Ghana na Vedaste Habumurey kutoka Rwanda,” anasema.

Anaongeza kuwa chuo hicho pia kimetoa fursa ya ufadhili kwa wanafunzi kutoka Sudani Kusini wanapotaka kusoma Shahada ya Awali ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

 

“Utekekelezaji unasubiri kukamilika kwa makubaliano kati ya Serikali za Tanzania na Sudan Kusini kuhusu utekelezaji wa makubaliano ya awali kuhusu ufundishaji wa Lugha ya Kiswahili nchini Sudani Kusini.

 

“Rais John Magufuli amesema katika hotuba zake, tena sio mara moja, kwamba tutakuwa a donor country, (nchi mfadhili). Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeanza kuyaishi maono hayo,” anasema.

 

Kwa mujibu wa Profesa Anangisye, msukumo wa kuanzisha mpango huo ulichochewa na kiu ya menejimenti ya chuo hicho katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwekeza kwenye elimu ya watoto wa Kitanzania katika ngazi zote za elimu ikiwemo elimu ya juu katika nchi ya Tanzania.

 

Anasema hatua hiyo pia inalenga kuboresha  maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa watoto na vijana wa Kitanzania kwani wanufaika wa ufadhili huo wakihitimu watakuwa na mchango muhimu katika maendeleo ya nchi katika sekta zote ikiwemo sekta ya viwanda.

 

Hatua hiyo anasema inalenga pia katika kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike katika masomo ya sayansi na teknolojia katika elimu ya juu.

 

“Katika hili tunaunga mkono jitihada za Rais Magufuli. Kwa meneno yake Rais, alisema mwaka jana, 2020: ‘Tutahimiza ufundishaji wa masomo ya sayansi na hisabati, hususan kwa wanafunzi wa kike…’.”

 

Anasema: “Ikumbukwe kuwa tangu kuanzishwa kwake, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeendelea kuwahudumia Watanzania wote bila kujali maeneo wanayotoka, vipato vyao, wala vigezo vingine vya ubaguzi. Ufadhili huu unakisogeza Chuo hiki karibu zaidi na wananchi.”

 

Kwa mujibu wa Profesa Anangisye, ufadhili wa wanafunzi kutoka nje ya nchi ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (Toleo la Mwaka 2020). Sura ya Tatu: Huduma za Jamii hususan kwenye eneo la Elimu ya Juu, kipengele (f) (uk. 130) inayozungumzia; “Kuongeza udahili katika elimu ya juu kwa makundi yote yakiwemo wanafunzi kutoka nje ya nchi”.

 

Anataja idadi ya wanafunzi wanaofaidika na ufadhili huo kwa mwaka kuwa ni takribani 62 (+3). Mgawanyo ambao unazingatia vigezo vya usawa wa jinsia lakini kwa kusisitiza masomo ya Sayansi na Teknolojia, na utaifa kwa ufadhili kwa wanafunzi wanaotoka nje ya Tanzania.

 

“Wakati tunaanza tuliweka lengo la kutenga zaidi ya Sh milioni 237 kwa mwaka kwa ajili ya ufadhili huo. Wanafunzi waliolengwa wamepatikana na wanaendelea kunufaika na ufadhili huu.

 

“Ili mwanafunzi aliyepata ufadhili aendelee kunufaika ni lazima aendelee kufanya vizuri katika masomo yake. Wale ambao watashindwa kupata viwango vya juu vya ufaulu katika masomo yao kila mwaka ufadhili utasitishwa. Naomba nitumie nafasi hii kuwaasa wanafunzi walionufaika na fursa hii kuongeza juhudi katika masomo yao,” anasema.

 

Anawaasa wanufaika watarajiwa yaani wanafunzi walioko sekondari sasaa kuongeza juhudi katika masomo kwani chuo hicho kinawasubiri wale wenye ufaulu mzuri ili wapate ufadhili utakaowawezesha kusoma kozi yoyote ya Sayansi na Teknolojia.

 

“Kwa wale ambao tumewapa ufadhili huu, tunawaasa waendelee kusoma kwa bidii ili wasije kupoteza nafasi hii adhimu. Hakuna ‘kula bata’ Chuo Kikuu Chuo cha Dar es Salaam. Ni kusoma kwa juhudi na maarifa,” anasema.

 

Anasema pamoja na kutambua jitihada kubwa ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali katika kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Chuo kinatambua mchango wa taasisi za Serikali, sekta binafsi, na watu binafsi katika kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

 

Hivyo chuo anasema hicho kinatoa wito kwa mashirika, taasisi za umma, sekta binafsi na watu binafsi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwekeza katika elimu ya vijana.

 

“Wito wetu unatokana na ukweli kuwa kuna familia ambazo hazina uwezo wa kumudu kikamilifu gharama za elimu ya Chuo Kikuu. Hivyo tunaamini mpango huu utaungwa mkono na wabia wetu kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wananufaika na ufadhili huu,” anasema.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako anasema katika kuhakikisha Watanzania wanaendelea kupata taaluma bora ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa nchi kwa ufanisi na ubunifu wa hali ya juu, wizara ya elimu itaendelea kushirikiana na Menejimenti ya Chuo ili kufikia azma hiyo.

 

Profesa Ndalichako anasema, UDSM kinatambulika kuwa ni taasisi kinara wa taaluma nchini Tanzania, na moja ya vyuo vikuu mashuhuri miongoni mwa vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za Elimu ya Juu Barani Afrika.

 

“Nimearifiwa kuwa mpango huu wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wenye ufaulu wa juu uliasisiwa katika mwaka wa masomo 2019/2020 na hivyo tayari wanafunzi wameanza kunufaika na mpango huu. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimekuwa mfano mzuri kwa kuanzisha mpango huu wa ufadhili,” anasema.

 

Profesa Ndalichako anasema ufadhili huo ni mzuri kwani unamwezesha mnufaika kugharimiwa masomo yake na hatakiwi kurejesha fedha zilizotumika kumsomesha.

 

“Cha kuzingatia tu ni kwamba, mnufaika atatakiwa kuendelea kufanya kazi kwa bidiii na kufuatilia masomo kwa umakini kwani Chuo kinaweza kumuondolea ufadhili iwapo ataonekana kutokuwa na maendeleo ya kuridhisha kitaaluma,” anasema.

 

“Hivyo, ninapenda kutumia nafasi hii kutoa wito kwa taasisi za elimu ya juu, kuiga mfano huu. Aidha, natoa wito kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kuhakikisha kuwa wanasoma kwa juhudi na maarifa ili wafaulu vizuri na hatimaye wapate nafasi hii adhimu,” anasema Profesa Ndalichako.

 

Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu Huria nchini (OUT), Faustin Silvester anasema huo ni utaratibu mzuri kwa sababu kuna watoto wengi wa maskini wana akili za kutosha lakini wanashindwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu kwa kukosa ufadhili.

 

 

“ WAPO wanaume wanaoona aibu kwamba nikienda na mke wangu ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi