loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanaonyonyesha, wajawazito, barakoa na janga la corona

GAUDENCIA (31) na Modesta (27) ni wanawake wanaonyonyesha. Mtoto wa Gaude ana umri wa miezi 11 sasa, huku yule wa Mode akiwa na umri wa miezi 10.

Gaude anaishi Sirari, Tarime mkoani Mara. Mode, anaishi nyumbani kwao maeneo ya Njiapanda ya Kitunda, Buza wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam.

Kwa nyakati tofauti wanasema, mwaka jana ulipoibuka ugonjwa virusi vya corona (Uviko -19), walikuwa na ujauzito.

“Nilipata wakati mgumu sana kuvaa barakoa maana hata katika hali ya kawaida ninapolala, huwa sijifuniki usoni kwa hiyo, barakoa ilikuwa kimbembe kwa sababu nikivaa, kupumua inakuwa ‘issue’ (tatizo)…,” anasema Gaude.

Anaendelea: “Ingawa nilikuwa najisikia vibaya kuzivaa, nilikuwa ninalazimisha tu, maana hapa ni mpakani (Kenya na Tanzania), na mimi nina watoto wengine, hivyo inabidi kujihami hivyo hivyo kuwalinda watoto wangu maana hata walipokuwa wanatangaza mara kwa mara idadi inavyoongezeka ya watu wanaokufa, walikuwa wananiua zaidi.

Gaude anasema: “Namshukuru Mungu nimejifungua salama na mpaka sasa tuko salama…”

Mode yeye anasema: “Kweli wakati wa corona barakoa zilikuwa mtihani mkubwa, maana kujilinda ninataka, lakini nikivaa najisikia kufakufa hivi; ninakosa hewa na kuanza kupumulia juu juu. Kwa kweli ilibidi nimwachie Mungu na kumtegemea yeye tu…”

Kwa nyakati na mazingira tofauti wanasema, uhakika wa kama watoto wao watakuwa salama ikitokea wao wakapata maambukizi, ulikuwa mtihani mzito uliowasababishia msongo wa mawazo.

“Kilichokuwa kinanipa hofu zaidi ni kuwa, nikipata corona, si nitamwambukiza mwanangu hata hajazaliwa?” anasema Gaude.

Anaongeza: “Na je, kama nimejifungua salama, nitafanyaje ili nisimwambukize mtoto wakati ananyonya maziwa yangu?”

Gaude na Mode, wanawakilisha wanawake wengi wakiwamo wajawazito na wanaonyonyesha ambao hawakufikiwa na elimu sahihi ya kutosha ulipoibuka ugonjwa huu nchini hivyo, kuonesha haja ya makundi hayo kupewa elimu sahihi, ya kutosha na endelevu ili corona inapoibuka, wawe na taarifa sahihi za kutosha.

Haya yanabainika baada ya Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kupitia ufadhili wa shirika la kimataifa la UN-Women (Tanzania) kwa wandishi wa habari wa mikoa mbalimbali kuwajengea uwezo zaidi wa kubaini na kuibua changamoto, fursa, na mbinu walizotumia wanawake wakiwamo wenye ulemavu na wajawazito, kukabili athari za ugonjwa huo ulipoibuka nchini na nini kifanyike ukiibuka tena.

Mwenyekiti wa Tamwa, Joyce Shebe anasema, serikali na wadau wengine zikiwamo taasisi za dini na mashirika binafsi, washirikiane kuweka mipango ya kimkakati kuwalinda wanawake wakiwamo watoto wa kike, wenye ulemavu, wajawazito na wanaonyonyesha ili janga kama hili linapotokea, wasaidiwe kupata huduma muhimu.

Hudumu hizo anazitaja kuwa ni pamoja na elimu sahihi na ya kutosha mintarafu kujikinga na namna sahihi ya kuishi kabla, wakati na baada ya janga.

Anasema katika kipindi cha corona, moja ya changamoto walizopata wajawazito wengi ni ugumu wa kutafuta na kupata huduma za kliniki na wataalamu wa afya.

Shebe anasema: “Katika kipindi hicho, iliwagharimu wajawazito hasa namna ya kwenda kliniki au hospitali na kumpata daktari kwa wakati na kwa wengine, ilionekana kama vile hospitali si sehemu salama ingawa kwa Tanzania hali ilikuwa nzuri tu; huwezi kulinganisha na mataifa mengine.”

Mtandao  wa Jinsia Tanzania (TGNP) ni miongoni mwa taasisi wadau katika mradi huo wa elimu kwa waandishi wa habari mintarafu madhara, fursa na changamoto za corona kwa wanawake.

Katika tamko lake la Aprili 3, 2020, kuhusu ‘Virusi vya Corona na Athari zake kwa Wanawake na Watoto wa Kike,’ mtandao wa TGNP unasema, katika kipindi cha majanga kama corona, ni muhimu kuwapo mikakati madhubuti ya kuwalinda wanawake wakiwamo wajawazito na wanaonyonyesha kwa kuwafikia na kuwapelekea huduma na elimu huko waliko ili wawe na taarifa sahihi, waondoe hofu, wajikinge na kuwakinga wengine wakiwamo watoto wao.

Wadau wengine katika mradi huo kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben, ni Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) na African Women Leaders Network (AWLN).

Taarifa hiyo inasema: “… Ukweli wa kitabibu kuhusu mwanamke mwenye ujauzito na aliyetoka kujifungua ni kuwa, wengine kinga zao si imara sana hususan kwa kipindi anaponyonyesha.”

“Hospitali zilizo na wauguzi wanawake wazazi wa chini ya mwaka mmoja, tunashauri wasipangiwe majukumu ya kuhudumia wagonjwa wa corona. Hii si tu kwa wanawake wajawazito walio kwenye sekta ya afya, bali hata walio katika jamii zetu. Ni vyema wao wenyewe kujilinda na pia, jamii, waajiri na serikali tuwalinde kwa kuwaepusha na misongamano.”

TGNP unasema, katika huduma za kliniki kwa wajawazito na watoto, ambapo mara nyingi huwa na msongamao wa watu, ni vyema kusisitiza taratibu za kujikinga ikiwemo kupata huduma wachache wachache kwa kukaa mbali kwa mita moja toka mtu na mtu.

Kwa mujibu wa chapisho la mtandaoni la Elimu ya Afya kwa Umma Kuhusu Kujikinga na Ugonjwa wa Covid- 19 lililotolewa na Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Juni 2020, corona haiambukizi mtoto aliyeko tumboni na maziwa ya mama hayana virusi vya corona.

Chapisho lingine mtandaoni linasema: “Tafiti na shahidi za kisayansi zilizopo mpaka sasa hazijaonesha uwezekano wa mtoto aliye tumboni kuambukizwa virusi vya corona na mama yake wakati wa ujauzito au kujifungua....”

Kuhusu kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 kutoka kwa mama anayenyonyesha kwenda kwa mtoto, wizara inasema: “Nawa mikono kwa maji tiririka na sabuni kabla ya kumgusa mtoto wako. Vaa barakoa wakati wa kunyonyesha na muda wote anapokuwa karibu na mtoto.”

“Nawa mikono yako kabla ya kugusa chupa ya kuhifadhia maziwa na iwapo utatumia pampu ya kukamulia maziwa, hakikisha unazingatia kanuni na taratibu za usafi.”

Wataalamu mbalimbali wa afya wanasema ili kujikinga dhidi ya maambukizi, wajawazito watumie njia zote zilizoanishwa katika makundi mengine ikiwa ni pamoja na kupunguza safari zisizo za lazima, kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji tiririka, pamoja na kula mlo kamili (lishe bora).

Kwa mujibu wa uchunguzi, katika kipindi cha corona mwaka jana, kipato kwa watu wengi kilishuka kutokana na kusitishwa kwa shughuli nyingine na wengine kufanyia kazi nyumbani, hali iliyoathiri lishe katika familia kadhaa.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Ngorongoro, Benezeth Bwikizo, anasema:“Kwa kuwa wanawake wengi wako katika ujasiriamali mdogo ukiwamo wa kuuza vitu kama matunda ofisini na barabarani, hali ya lishe kwa wengine wakiwamo wajawazito iliyumba.”

Akiwa katika kituo kimoja cha televisheni nchini wiki iliyopita, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Dk Godfrey Chuwa, anasema lishe bora huongeza kinga ya mwili kwa wagonjwa, wazee na watu wengine wakiwamo wajawazito na watoto.

Vyanzo vinasisitiza kuwa, mlo kamili hujenga mwili na kuimarisha mfumo wa kinga kwa kupunguza uwezekano wa kupata maambukizi ya magonjwa.

“Unatakiwa kula chakula bora kutoka shambani hasa vyakula visivyo vya viwandani. Unatakiwa kila siku upate vitamini, madini lishe, nyuzi lishe, protini na virutubisho vinavyosaidia mwili kuondoa sumu mwilini,” kimeandika chanzo kimoja mtandaoni.

Alipoulizwa maoni yake kuhusu baadhi ya wajawazito kupata shida kupumua wanapotumia barakoa, Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (Prolife) Tanzania, Emil Hagamu anasema: “… Unajua hata kama mtu si mjamzito, barakoa ikibana sana, inamfanya mtu anapopumua na kutoa kabondaiksaidi (hewa chafu), badala ya kuitoa nje, analazimika kuivuta kuirudisha ndani; sasa hatuwezi kujua kama zilikuwa zinabana sana, au la.”

Hagamu anasema: “Kitendo cha kurudisha hewa chafu mwilini, kinadhoofisha mwili. Sasa kama mtu katika hali ya kawaida barakoa ikibana sana inakuwa shida, kwa mjamzito itakuwaje… Barakoa zitumike kwa umakini kama inavyoshauriwa na watalaamu. Hii nayo ni elimu wanayopaswa kuipata sawasawa wajawazito”

Mtaalamu wa saikolojia-tiba jijini Dar es Salaam, Dk Saldin Kimangele akihimiza barakoa sahihi na matumizi sahihi ya barakoa.

“Wakati mwingine hata barabarani unashangaa kuona mtu ana barakoa, lakini ameining’iniza kwenye kidevu; si sahihi...”

Uchunguzi umebaini baadhi ya watu huvaa barakoa zinazopwaya na kushuka kidevuni hali inayowalazimisha kuzipandisha mara kwa mara, huku wakiwapo wengine wanaovaa zinazobana kupita kiasi hata kuwapa ugumu wa kupumua.

Hagamu anasema: “Nadhani si sahihi kuvaa barakoa inayobana sana na pia, si sahihi kuivaa muda wooote hata pasipo na msongamano wa watu wala tishio…”

Mwongozo wa Kinga na Kuzuia Maambukizi katika Jamii Dhidi ya Ugonjwa wa Corona (Covid-19) uliotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Aprili, 2020, unasema ili barakoa ziwe nyenzo muhimu kukinga na kupunguza uwezekano wa maambukizi, zitumike kwa kuzingatia kanuni maalumu kabla ya kuvaa, wakati wa kuvaa na kuvua na kuziteketeza kwa moto zilizotumika.

“ WAPO wanaume wanaoona aibu kwamba nikienda na mke wangu ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi