loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ubunifu huu utaendeleza bunifu huu utaendeleza uhifadhi Ngorongoro

“ KWA kuwa sheria hairuhusu kulima ndani ya hifadhi, serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilitafuta eneo hili nje ya hifadhi ili wananchi waweze kukodi na kulima mazao mbalimbali yatakayowawezesha kupata chakula na kuepuka kutegemea mifugo pekee.”

Anasema Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) anayesimamia Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii, Dk Christopher Timbuka hivi karibuni alipozuru Mradi wa Shamba la Mang’ola Juu wilayani Karatu katika Mkoa wa Arusha lililoanzishwa ili kuwasaidia wananchi wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kulima mazao mbalimbali ya chakula.

NCAA ndiyo iliyosaidia upatikanaji wa shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 53 ili kuwasaidia wananchi wa vijiji vilivyoko ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kukodi na kulima mazao mbalimbali yakiwemo mahindi na maharage kwa ajili ya chakula.

Kwa nyakati tofauti, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Benezeth Bwikizo, anashauri jamii katika wilaya hiyo hususan wanawake, kutotegemea shughuli za utalii pekee kama njia ya kupata kipato ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza hasa sekta hiyo inapokumbwa na changamoto kama kupungua kwa watalii kutokana na sababu mbalimbali.

Bwikizo anasema hatua hii itawasaidia pia hata wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuwa sheria za uhifadhi haziruhusu kufanya shughuli za kiuchumi kama kilimo hifadhini.

Anasema: “Hivyo, ni vizuri wanajamii hasa wanawake ambao huwa ni waathirika wakubwa hasa yanapotokea majanga, kutobweteka kwa njia moja pekee ya kipato, bali kuwa na uzalishaji wa namna mbalimbali, hasa wa kupitia kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara.”

Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Dk Freddy Manongi anasema, upo uhusiano mkubwa baina ya hifadhi hiyo na wenyeji wanaoishi ndani ya hifadhi. Manongi anasema: “Popote duniani, ni vigumu kukuta watu wanaishi katika hifadhi na wanaendesha mila zao kama kawaida huku kukiwa na wanyamapori, lakini katika Hifadhi ya Ngorongoro, watu wanaishi na mifugo yao… Hiki ni kivutio kikubwa cha wageni nchini na tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kukiendeleza.”

Mara kadhaa Dk Manongi amenukuliwa akisema: “Unajua, majukumu makubwa ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, hasa ni kuendeleza uhifadhi na kuhifadhi, kuendeleza utalii; na kuendeleza wenyeji katika shughuli zao yaani, maendeleo ya jamii ya watu wanaoishi ndani ya hifadhi ambao kwa kiasi kikubwa sana, ni wa Kabila la Wamasai.”

Hivi karibuni, HabariLEO likiwa Ngorongoro, lilishuhudia wenyeji wakiishi ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wakiendesha ufugaji wa ng’ombe, mbuzi, kondoo na punda huku wanawake wengi wakiwa katika maboma mbalimbali yenye vivutio kadhaa vya utalii kama ngoma za asili ya Kimasaai, mavazi, na mapambo mnbalimbali yanayotengenezwa kwa shanga.

Hata hivyo, katika mazungumzo, Dk Manongi anafafanua akisema: “Lakini, kwa kuwa katika hifadhi shughuli za kibinadamu kama kilimo, biashara na hata ujenzi wa nyumba bora haziruhusiwi, hifadhi inawaendeleza watu kwa namna mbalimbali maana uchumi wa watu hao unategemea mifugo pekee.” Mintarafu Mradi wa Shamba katika Kijiji cha Mang’ola Juu wilayani Karatu, Naibu Kamishina Timbuka anasema: “Mradi umeanza msimu huu na kadri unavyoendelea, tunaamini wananchi wengi watahamasika kulima kwa kuwa eneo lipo la kutosha.”

Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayesimamia Idara ya Maendeleo ya Jamii wa NCAA, Mdala Fedes, anafafanua kuwa, mradi huo ulianza kwa kutoa elimu na hamasa kwa wananchi wa vijiji 25 katika kata 11 zilizopo ndani ya hifadhi kuhusu uwepo wa fursa hiyo.

Anasema wananchi 246 kutoka vijiji mbalimbali vikiwemo vya Sendui, Bulati, Misigyo na Olpiro walikubali kuanza kulima na tayari kati ya ekari 53 zilizolimwa msimu huu, ekari 47 zimeshaoteshwa mazao mbalimbali.

Kwa mujibu wa Mdala, lengo la NCAA ni kuwahamasisha zaidi wananchi ili waendeshe kilimo cha kitaalamu na hivyo, kupata tija zaidi. Anasema: “Tumewaunganisha na wataalamu wa kilimo ili waelimishwe kulima kitaalamu na kupata mazao ya kutosha kuliko kutegemea serikali moja kwa moja… Tunalenga mwakani hali ya hewa ikiruhusu, wananchi walime ekari 500 kwa kuwa eneo lipo la kutosha.”

Ndiyo maana kutokana na hali na lengo hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Sendui katika Kata ya Alaelelai wilayani Ngorongoro, Meeli Saruni, anaishukuru serikali kupitia NCAA kwa kuwasaidia kupata eneo hilo na kuahidi kuhamasisha wananchi wa vijiji vingine kujitokeza kwa wingi hasa katika msimu wa kilimo utakaofuata.

Katika semina ya hivi karibuni kwa wahariri na wandishi wa habari iliyofanyika katika ofisi za NCAA, zilizopo katika Kreta ya Ngorongoro, Ofisa Uhifadhi Mwandamizi wa NCAA, Elibariki Bajuta, anasema hifadhi inazo shughuli mseto yaani, utalii, uhifadhi na shughuli za binadamu katika eneo moja.

“Hata hivyo, changamoto kubwa ipo katika uhifadhi na shughuli za binadamu (wakazi),” anasema. Kwa nyakati tofauti, Bajuta na Dk Manongi wanasema, uhusiano huo baina ya hifadhi na wananchi walio ndani yake, unakumbana na changamoto kubwa ya asili ambayo sasa ni mtihani unaohitaji majawabu makini na moyo wa kizalendo.

“Kadiri unavyowekeza zaidi katika uhifadhi, ndivyo unavyoathiri maendeleo ya jamii na unavyowekeza zaidi katika maendeleo ya jamii, ndivyo unavyoathiri uhifadhi. Kwa hiyo utaona shughuli za upande mmoja zinaathiri upande mwingine. Huu ni mtihani na changamoto kubwa,” anasema Bajuta.

Dk Manongi anasema: “Tunajitahidi sana kutafuta njia za kupunguza athari ili kutoathiri upande wowote maana tunapenda maendeleo ya jamii, na tunapenda hifadhi na bado tafakuri zaidi za wadau zinahitajika...” Kutokana na hali hiyo, anasema kumekuwa na changamoto kadhaa zikiwamo za magonjwa kutoka kwa wanyamapori kwenda kwa watu na mifugo, pamoja na magonjwa kutoka kwa watu au mifugo kwenda kwa wanyamapori huku kukiwa na changamoto kubwa zaidi ya wenyeji kuwa wategemezi wa NCAA huku wakiongezeka na mifugo pia ikiongezeka.

“Hali hii pia imesababisha kuharibika kwa mazingira; vyanzo vingi vya maji vimepungua na kiwango cha maji kimepungua na kuwapo migogoro baina ya watu na wanyamapori maana makazi yameongezeka kwa kuwa watu nao wanaongezeka na kuwa tishio kwa uhifadhi,” anasema.

Kuhusu suala hili, Bajuta anaongeza: “Kimsingi huu ni mtihani mkubwa katika ‘kubalance’ uhifadhi endelevu na maendeleo ya wakazi maana ongezeko la watu na makazi, linatishia uhifadhi endelevu na uhifadhi endelevu na uboreshaji wa miundombinu yake, unatishia ustawi wa wenyeji walioko ndani ya eneo.”

Wadau wanasema mradi huo wa shamba ni hatua nzuri kuelekea kuwawezesha wananchi wa vijiji hivyo ndani ya hifadhi kuondokana na utegemezi wa serikali kwa mahitaji yao hususan chakula uliopo sasa na kwamba, kwa kulifanikisha hilo, NCAA imeona mbali maana itasaidia kuendeleza uhifadhi Ngorongoro.

Mmoja wa wanahabari wa jijijini Arusha aliyeshiriki semina hiyo anasema ni vyema hatua hiyo iende sambamba na kuwaelimisha na kuwahamasisha wenyeji kuona umuhimu na faida kubwa ya vizazi vyao kuendesha maisha nje ya hifadhi ili kuufanya uhifadhi kuwa endelevu zaidi.

Anasema: “Hii ni kwa kuwa ni rahisi wenyeji kupisha hifadhi kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori, kuliko wanyama kupisha wenyeji na kuanza maisha sehemu nyingine na jambo hili linahitaji utashi na uzalendo…”

Hivi karibuni gazeti hili lilimnukuu mmoja wa maofisa wa serikali katika Wilaya ya Ngorongoro akisema: “Kama inavyofanyika kwa maeneo hatarishi na yenye miradi ya kimkakati, serikali ijenge msingi wa kusaidia vizazi vingine vya jamii hizo, kuishi nje ya eneo hilo kuepusha ongezeko la kaya na maendeleo ya watu katika hifadhi yanayoathiri uhifadhi...”

Wadau mbalimbali wanapongeza kuanzishwa kwa mradi huo wa shamba wakisema uendelezwe zaidi kwa kuwa utaondoa utegemezi unaotokana na ugawaji wa chakula kwa wenyeji unaofanywa na NCAA wa gunia takriban 10 za mahindi kwa mwaka kila kaya, hali inayowachochea kuendelea kurudi hifadhini hata wanaohitimu elimu vyuoni, jambo ambalo ni tishio kwa uhifadhi endelevu.

“ WAPO wanaume wanaoona aibu kwamba nikienda na mke wangu ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi