loader
Dstv Habarileo  Mobile
Tanzania na utajiri wa wanawake wenye uwezo katika uongozi

Tanzania na utajiri wa wanawake wenye uwezo katika uongozi

JUZI wanawake nchini waliungana na wenzao duniani kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani iliyokuwa na kaulimbiu isemayo: “Wanawake Katika Uongozi: Chachu Kufikia Dunia Yenye Usawa.” Siku hii huadhimishwa kila ifikapo Machi, 8.

Kupitia makala mbalimbali kabla ya siku hii, nilisoma moja iliyoandikwa na Vick Kimaro katika HabariLEO iliyokuwa inasema, Tanganyika ilipopata uhuru ikiongozwa na Mwalimu Julius K. Nyerere mwaka 1961, Baba wa taifa aliunda baraza la mawaziri ambalo halikuwa na mwanamke ambaye ni ‘waziri kamili.’

Miongoni mwa wanaharakati mashuhuri waliokuwa mstari wa mbele kupigania uhuru wakati huo, Bibi Titi Mohammed, alimwendea Mwalimu na kumuuliza kulikoni hakuna mwanamke ambaye ni waziri.

Taarifa za kihistoria zinasema, Nyerere alimjibu kuwa, amejitahidi lakini imekuwa vigumu kumpata mwanamke mwenye sifa stahiki kuwa waziri kamili, bali naibu waziri. Ndipo Bibi Titi akamuuliza: “Hao wanaume wenye sifa leo walikuwa wapi wakati tunapigania uhuru?”

Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Joseph Khenani anasema: "Kama vile ambavyo kuna wanaume ambao hawawezi, wapo na wanawake baadhi ambao hawawezi; lakini kama vile ambavyo kuna wanaume wanaoweza na wanawake tunaweza vile vile" katika siasa na uongozi.

Mongella; Getrude Mongella ni sehemu ya utajiri iliobarikiwa kuwa nao Tanzania wa kuwa na wanawake wenye vipaji na uwezo wa kuongoza na kuwakilisha jamii katika nyanja, sekta na ngazi mbalimbali za kijamii wakishika hata nafasi za kisiasa ambazo awali, zilidhaniwa kuwa ni za wanaume pekee.

“Kama unataka kuwa kiongozi, lazima kwanza uwe na picha kamili ya unachokitaka, lazima usimamie kanuni na maadili. Kanuni na maadili haziwezi kukuangusha kamwe,” anasema Getrude Mongella katika mkutano wa African Women’s Forum nchini Ghana Januari 1997.

Huyu ni mwanamke wa Kitanzania aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Bunge la Umoja wa Afrika. Kati ya mwaka 1993 hadi 1995, alikuwa Katibu Mkuu wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Wanawake na kuhudhuria Mkutano wa Nne uliofanyika Beijing nchini China mwaka 1995.

Kazi kubwa ya kututuka na uwezo wa uongozi aliouonesha huko, imemfanya ajulikane miongoni mwa Watanzania kama ‘Mama Beijing.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, Boutros Boutros Ghali, ndiye aliyemkabidhi Mongella dhamana hiyo.

Januari 2007, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (wakati huo), Ban Ki-Moon, akauona uwezo wa mwanamke mwingine wa Kitanzania; akamteua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Dk Asha-Rose Migiro, kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Dk Migiro aliutumikia wadhifa huo sawia akiyatetea mataifa yanayoendelea na kuonesha umahiri mkubwa katika uongozi wa kitaifa na kimataifa akiwa mfano bora wa wanawake wa Kitanzania wenye uwezo mkubwa katika uongozi na siasa. Kwa sasa Migiro ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.

Mwanamke mwingine ni Anna Mghwira. Katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, alikuwa mwanamke pekee aliyeingia katika kinyang’anyiro akiwa mgombea Urais kupitia chama cha ACT-Wazalendo.

Licha ya kuwa mwenyekiti wa chama hicho cha upinzani (wakati huo), uwezo wake katika siasa safi na uongozi bora, ulimfanya Rais John Magufuli kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, wadhifa anaoutumikia hadi sasa.

Wakati Anna Mghwira anaingia katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015, chama hicho kilisema ana sifa zote za kuwa kiongozi bora wa kitaifa.

Mwaka jana ulipoibuka ugonjwa wa Covid-19  nchini katika kuthibitisha ujasiri, uwezo na upendo wa wanawake kwa taifa, huku akiwa mkuu wa mkoa, Mghwira alisaidia mapambano kwa kujitangaza kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo (corona) na kujitenga kadiri ya maelekezo ya wataalamu. Ujasiri wake ulishangaza wengi.

Hazina nyingine ya wanawake Watanzania wanaoonesha uwezo wa wanawake katika ushiriki wa siasa na uongozi, ni Watanzania kama Samia Suluhu Hassan na Anne Makinda.

Makinda ni Spika wa Kwanza Mwanamke katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tangu mwaka 2006 hadi 2010, alikuwa Naibu Spika chini ya Spika Samuel Sitta. 

Uwezo wake katika uongozi akiwa naibu spika, ulilifanya Bunge kumchagua kuwa Spika mwaka 2010 akiweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza Tanzania kushika wadhifa huo na kuonesha uwezo wa wanawake katika siasa na uongozi.

Alistaafu mwaka 2015 na nafasi yake kushikwa na Job Ndugai anayeitumikia hadi sasa. Kazi aliifanya na Anne Makinda akadhihirisha ukweli kuwa, ‘Wanawake Wanaweza.’

Kwa upande wake Samia Suluhu, kwanza alionesha umahiri mkubwa katika uongozi alipochaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba Mwaka 2014. 

Uwezo huo ukakishawishi Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia mgombea urais wake katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, Dk John Magufuli, kumteua kuwa mgombea mwenza.

Samia Suluhu ameweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Tanzania katika wadhifa wa Makamu wa Rais. Uwezo na utumishi wake makini katika siasa na uongozi hadi sasa, ni ushahidi tosha kuwa wanawake wanaweza; tena kwa ufanisi. Marekani unaweza kusema nao wametuiga na sasa wana makamu rais mwanamke!

Mgombea Urais wa ADC katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Queen Sendiga ambaye ni mwanamke mwenzake, anakiri uwezo wa Samia katika siasa na uongozi wa taifa.

Hata hivyo, licha ya Tanzania kuwa na utajiri mkubwa namna hiyo wa kuwa na wanawake wengi wenye uwezo mkubwa katika siasa na uongozi katika nyanja, sekta na ngazi mbalimbali, bado jamii haijatambua umuhimu wa kuwashirikisha kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi na hata kuwapa fursa za kushiriki siasa na uongozi ipasavyo.

Kimsingi, wapo wanawake wengi wasioonekana wala kujulikana katika siasa na uongozi kwa kuwa hawajapewa fursa za kutumika kama viongozi bora nchini, lakini kinachofurahisha, wachache waliopata fursa hiyo, wameonesha uwezo mkubwa.

Ndiyo maana shirika la kimataifa la UN–Women (Tanzania), liliamua kukifadhili Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) na wadau wengine, kuendesha mradi wa ‘Wanawake Wanaweza’ na kutoa mafunzo kwa wanahabari kuhusu namna ya kuwaibua wanawake.

Lingine ilikuwa kuibua changamoto zinazowakumba wanawake katika harakati za kushiriki siasa na uongozi ili wengine wawe kioo kwa wenzao na hasa, kuhamasisha jamii kubadili mtazamo kuhusu uwezo na ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi kwa kuwa, wanawake wanaweza.

Kimsingi, Wanawake Wanaweza ni mradi unaolenga kuwawezesha wanahabari kuhamashisha na kuwaelimisha wanawake ili wajitokeze kuwania nafasi za uongozi ama wa kuchaguliwa, au kuteuliwa katika kada mbalimbali kadiri ya sifa na uwezo.

Watetezi wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia wanasema kukiwa na ongezeko la viongozi wanawake katika jamii na katika sekta na ngazi mbalimbali, itakuwa rahisi kukabili changamoto mbalimbali zinazoisumbua jamii (serikali) kwa kuwa hata katika sekta isiyo rasmi kiuchumi, wanawake ndio wengi.

Ndiyo maana Februari 2018, akiwa spika, Makinda alinukuliwa akiwaomba wabunge wa viti maalum, waanzee kujiamini na kwenda kugombea majimboni watakapo maliza vipindi viwili bungeni.

Kimsingi, ili kuibua wanawake viongozi wengi zaidi katika jamii, jitihada zinapaswa kuanza katika ngazi za familia kwa kuwaamini, kuwatia moyo na kuwaonesha kuwa hata watoto wa kike wanaweza kuongoza kwa kuwa wanawake wanaweza, hivyo, wapewe fursa kushiriki katika masuala mbalimbali yanayochochea maendeleo, badala ya kuwaachia wanaume pekee.

Katika mafunzo kwa wanahabari kupitia mradi wa Wanawake Wanaweza, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben, anasema: "Tuelewe kwamba, wanawake wanaweza isipokuwa, kuna misingi ya mila kandamizi zilizojengwa katika jamii; kuna tatizo kwamba wanawake hawajaaminiwa kuwa wanaweza kuwa viongozi halali na bora zaidi katika familia, jamii, uchumi na Taifa."

Anaongeza: "Viongozi wa dini, kimila na wachechemuzi wa masuala ya kijinsia, wakitoa matamshi ya kuisihi jamii kumuona mwanamke kuwa anafaa na anaweza kuwa kiongozi katika siasa, uchumi na kijamii, kutakuwa na mstakabali mzuri wa taifa letu."

Hata katika uzinduzi wa Bunge la 12 Novemba 2020 jijini Dodoma, Rais Magufuli anasema, Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuwaamini wanawake katika kushika nafasi mbalimbali za kiuongozi kwani wameonesha ni jinsi gani wanaweza wakiaminiwa.

"Nipende kuwaambia wanawake kuwa serikali yangu itaendelea kuwaamini na kuwapa nafasi mbalimbali za kiuongozi wanawake maana nimeona ni jinsi gani mnachapa kazi na ndio maana hata Makamu wa Rais (Samia Suluhu)  ni mwanamke na pia, nikupongeze na wewe Dk Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kuendelea kuwa Naibu Spika," anasema Rais Magufuli.

Mwandishi mmoja wa habari anasema, masuala ya kiafya yakiwamo magonjwa ya mlipuko, mila na mazoea ya ubaguzi, hayapaswi  kuachwa yawe kikwazo kwa  wanawake kushiriki siasa na uongozi badala yake, yawafanya wanawake na wanaume kuwa kitu kimoja katika maendeleo na usatwi wa jamii.

Kwa mujibu wa UN Women, vipo vikwazo viwili vikuu vinavyowazuia wanawake kushiriki kikamilifu katika maisha ya kisiasa vinavyopaswa ‘kukodolewa macho.’

Hivi ni vikwazo vya kimuundo kutokana na kuwapo sheria baguzi na taasisi zinazobana uwezo wa wanawake kugombea nafasi mbalimbali, sambamba na mianya ya kiuwezo inayotokea kwa wanawake kukosa elimu kuliko wanaume, uhusiano na raslimali zihitajikazo kuwa viongozi bora.

Ili kutimiza Lengo la 5 la Malengo ya Maendeleo Endelevu, “Kutimiza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake wote na wasichana,” lazima jamii ijizatiti kuhusisha usawa wa kijinsia katika katiba zikiwamo za vyama mifumo ya kisheria ili kuondoa aina zote za vurugu dhidi ya wanawake na kuhakikisha wasichana wanapata elimu bora.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/3feab7ecb0ef101ff3ceb5abb40fc282.JPG

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi