loader
Dstv Habarileo  Mobile
Majaliwa aagiza Kilimo waanzishe minada ya chai

Majaliwa aagiza Kilimo waanzishe minada ya chai

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Marwa Rubirya afuatilie na kuchukua hatua kwa baadhi ya viwanda vya chai vinavyonunua majani mabichi ya chai ambavyo vimekuwa vikichelewesha malipo ya wakulima ahakikishe vinawalipa kwa wakati.

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo ianzishe minada ya kuuza zao la chai katika ukanda wa maeneo yanayozalisha zao hilo ili kuwarahishia wakulima kupata soko la uhakika na kuacha kutegemea minada ya nje ya nchi.

Alitoa maagizo hayo jana katika kikao na wadau wa zao la chai kilichofanyika mjini Njombe. Amesema serikali itasimamia kikamilifu zao hilo na kuhakikisha wahusika wananufaika.

Alisema dhamira ya serikali ni kuona zao hilo linapata mafanikio, hivyo amewataka watendaji wafuatilie kuhakikisha wakulima wote wananufaika na zao hilo.

“Lazima wakulima walipwe fedha zao kwa wakati ili waweze kuhudumia mashamba yao na kukidhi mahitaji yao,” alisema Majaliwa na kuongeza kuwa zao la chai ni mojawapo ya mazao ya kimkakati nchini, na serikali imedhamiria kuimarisha kilimo cha zao hilo ili liendelee kuwa na tija kwa wakulima, wenye viwanda na Taifa kwa ujumla.

“Zao la chai ni miongoni mwa mazao muhimu ya kibiashara yanayoliingizia Taifa fedha za kigeni. Zao hili huliingizia Taifa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 60 kwa mwaka. Tukiboresha mikakati yetu litatuongezea fedha nyingi zaidi,” alifafanua Waziri Mkuu.

 Alisema zao la chai limechangia kutatua tatizo la ajira nchini ambako watu zaidi ya 50,000 wameajiriwa viwandani na mashambani. Pia limetoa takribani ajira milioni mbili zisizo za moja kwa moja. “Idadi hii haitoshi kulingana na ardhi nzuri tuliyonayo,” alisema.

Kadhalika, aliwakaribisha wawekezaji waje nchini kujenga viwanda vya kuchakata zao la chai kwa kuwa nchi ina mazingira mazuri ya uwekezaji na malighafi ya kutosha pamoja na nishati ya uhakika.

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda amesema suala la ucheleweshwaji wa malipo linalofanywa na baadhi ya wamiliki wa viwanda vya chai halikubaliki, amewataka wawekezaji wote wawalipe wakulima fedha zao kwa wakati.

Kuhusu kuwepo kwa minada ya chai nchini, alisema ifikapo Mei mwaka huu wanatarajia kufungua mnada wa kuuza chai jijini Dar es Salaam hali itakayosaidia kupatikana kwa soko la uhakika.

Naye Mwenyekiti wa vikao vya wadau wa chai, Spika wa Bunge Mstaafu Anne Makinda ameiomba serikali kuiwezesha Bodi ya Chai Tanzania (TBT) na Taasisi ya Utafiti wa Zao la Chai (TRIT) kwa kuipatia vitendea kazi na wataalamu ili watimize majukumu yao ipasavyo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Njombe alimweleza Waziri Mkuu changamoto zinazowakabili wakulima wa chai mkoani humo kuwa ni baadhi ya viwanda vinavyonunua majani mabichi ya chai kushindwa kuwalipa fedha zao kwa wakati.

Zao la chai kwa hivi sasa linalimwa katika wilaya 12 zilizopo kwenye mikoa sita ambayo ni Mbeya, Njombe, Iringa, Tanga, Kagera na Kilimanjaro. Jumla ya eneo lililopandwa chai ni hekta 22,721 ambako wakulima wakubwa wana hekta 11,272 na wakulima wadogo hekta 11,449.

Wastani wa asilimia 80 ya chai yote inayozalishwa nchini huuzwa kwenye masoko ya nje. Kati ya hizo, wastani wa asilimia 40 huuzwa kupitia soko la mnada wa chai Mombasa na zilizobakia huuzwa moja kwa moja kwa wanunuzi katika nchi za Uingereza, Afrika Kusini, Ujerumani, Pakistani, Falme za Kiarabu, Urusi na Marekani.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Njombe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi