loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Samia atoa salamu za Magufuli Tanga

RAIS John Magufuli amewatumia salamu wananchi wa Tanga kupitia kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na kuwaeleza kuwa nchi ipo salama hivyo washikamane, wawe na umoja na wafanye kazi kwa bidii.

Makamu wa Rais alitoa salamu za Rais jana katika maeneo tofauti ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo.

Samia alisema Rais Magufuli anawashukuru wananchi wa Handeni na Mkoa wa Tanga kwa kukipigia kura za kutosha Chama Cha Mapinduzi na kukiwezesha kushinda katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka jana.

“Huu ni wakati wa kusikiliza maneno yanayotoka nje nasi yakatuparaganya vichwa. Nawaomba wote tushikane kwa umoja, kwa mshikamano wetu kama Watanzania. Tuendelee kuchapa kazi kama sisi tulivyokuja tunachapa kazi, tunaangala miradi,” alisema Makamu wa Rais wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Msata wilayani Handeni.

Samia alisema ni kawaida ya mwanadamu kupata changamoto za kiafya ikiwemo homa na mafua hivyo aliwataka Watanzania kuendelea kuomba dua ili nchi iendelee kubaki salama.

Alisema uimara wa Tanzania unaleta maneno mengi hivyo aliomba wananchi washirikiane na wafanye mambo yao kujenga taifa wakiwa wamoja na walioshikamana.

Akiwa Kabuku, alihimiza wananchi wafanye kazi kwa bidii na kusisitiza kuwa serikali itatekeleza yote iliyoahidi kwa wananchi. Aliwataka wananchi waache maneno maneno na mabishano yasiyo na msingi na badaya yake watumie muda wao kuzalisha kwa faida yao na nchi yao.

Baada ya kufungua kiwanda cha kuchakata mahindi kilichopo Michungwani, Segera, aliwaeleza wananchi kuwa Rais Magufuli anawasalimu na anawashukuru kwa kumchagua yeye na wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita.

“Kwa hiyo anawasalimia sana, anasema tupo salama, tuchape kazi twende vizuri, tujenge upendo na mshikamano wa Watanzania ili taifa letu likue liwe na tija zaidi,” alisema Makamu wa Rais.

Aliwapongeza wananchi wa hapo kwa kutoa eneo kwa mwekezaji na alimuagiza Mtanzania huyo kati ya ajira 600 za kudumu, wengi wawe ni wananchi kutoka eneo hilo. 

“Ndugu yetu John Kessy ni mzalendo wa Tanzania. Bilioni 21 anazoziweka hapa angeweza kuziweka popote kwingine ndani nje ya nchi. Kaamua kuzileta Michungwani, wana- Michungwani hii mali ni yenu… kwa maana hiyo niwaombe sana mkilinde hiki kiwanda, lindeni hiki kiwanda kwa sababu kiwanda hiki kitakupeni ajira,” alisema Samia.

Mkurugenzi wa kiwanda hicho, John Kessy alisema uwekezaji huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2025 na mradi wote utagharimu sh bilioni 21.3. Alisema wanatarajia kuajiri wafanyakazi 600 wa kudumu na litakuwa soko la uhakika la maelfu ya wakulima wa mahindi. 

“Kwa upande wa soko la mahindi tuna capacity (uwezo) ya kuweza kuhifadhi tani 10,000 za mahindi kwa wakati mmoja na tutasaga pia unga tuna capacity ya 100 kwa siku kwa kweli tunaomba sapoti ya wananchi kwa ujumla,” alisema Kessy.

Aidha, Makamu wa Rais alisema katika ziara yake ataangalia utekelezaji wa majengo ya halmashauri ambazo zimepelekewa fedha kwa ajili ya kujenga majengo ya utawala.

“Nimetoka kuona jengo la Halmashauri (ya Handeni) na hospitali kilichonivutia pale ni kwamba ujenzi unasimamiwa kwa umakini mkubwa, ni imani yangu kwamba zile fedhs tutakazo zishusha zitasimamiwa vema, katika kukamilisha majengo yaliyokusudiwa,” alisema.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela akizungumza wakati wa ufunguzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Vijijini, alisema serikali imepeleka jumla ya Sh bilioni 7.2 kujenga majengo ya halmashauri za Bumbuli, Handeni Mjini na Vijijini.

Mbunge wa Handeni Vijijini, John Salu alimuomba Makamu wa Rais kusaidia jitihada za wananchi wa Handeni ili wajengewe barabara za Mkata – Kwamsisi hadi Pangani na Handeni mpaka Turiani kwa kiwango cha lami pamoja na barabara yenye changamoto kubwa ya Handeni – Kibirashi hadi Singida.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ambaye pia ni Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu alimweleza Makamu wa Rais kuwa wizara imejipanga kuhakikisha maendeleo ya viwanda mkoani Tanga yanaenda sawa na uboreshaji wa mazingira.

Alisema mkoa umebarikiwa tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere kuwa na viwanda ambapo Rais Magufuli ameamua pia kwa nia moja kuufanya kuwa wa viwanda, hivyo ofisi yake itahakikisha mazingira yanaendelea kutunzwa.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alimwambia Makamu wa Rais kuwa serikali chini ya Rais Magufuli imedhamiria kumaliza tatizo la maji katika Wilaya ya Handeni na Mkoa wa Tanga kwa ujumla. 

Awali Makamu wa Rais aliweka jiwe la msingi katika jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 40 likitumia Sh bilioni mbili kati ya Sh bilioni 5.3 zinazotarajiwa kutumika kukamilisha ujenzi.

Miradi mingine ambayo Samia aliweka jiwe la msingi na ujenzi wake ni kiwanda cha kuchakata mahindi kilichopo Segera pamoja na Kiwanda cha kuchakata matunda kilichopo wilayani Korogwe.

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi