loader
Serikali yawatuliza wafanyabiashara wa mahindi

Serikali yawatuliza wafanyabiashara wa mahindi

SERIKALI imewatoa hofu Watanzania na wafanyabiashara kuhusu kuzuiwa kwa mahindi mpakani kwenda nchini Kenya na kusema hali itakuwa shwari hasa baada ya Serikali ya Kenya kubainisha kutozuiwa kwa mahindi hayo.

Imeeleza kuwa ingawa bado mahindi yaliyo mpakani hayajaanza kuingia nchini humo, lakini baada ya vikao na majadiliano wanaamini kuwa biashara hiyo itaendelea.

Hatua hiyo inatokana na kuzuiwa kwa mahindi kutoka Tanzania na Uganda kuingia nchini humo kutokana na kuwa na Sumu jambo ambalo jumuiya ya Afrika Mashariki limepinga hatua hiyo kuwa haikufuata utaratibu.

Katika barua yake ya Machi 5, mwaka huu, Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA), ilibainisha kuwa mahindi kutoka katika nchi hizo mbili yamekuwa na kiasi kikubwa cha sumu.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Profesa Siza Tumbo akizungumza na Kituo cha Televisheni cha Azam, alibainisha kuwa wizara itahakikisha unapatikana ufumbuzi wa masoko ya nafaka zote zinazouzwa nje ya nchi.

Alisema kwa sasa wanamalizia mkakati wa masoko kwa mazao ya kilimo ndani na nje ya nchi kwa kuangalia mipango ya mbali na wanategemea katika mikakati hiyo changamoto ya masoko itaisha.

“Sisi kama serikali tunajua kinachoendelea mipakani kama ndiyo maana hatuna wasiwasi...na ndiyo maana wafanyabiashara hawapigi kelele,” alisema Profesa Tumbo.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Kenya, John Simbachawene alionesha kuwatoa hofu Watanzania kuwa majadiliano ya suala hilo katika ngazi mbalimbali yanaendelea.

“Ingawa bado hatujapata taarifa rasmi lakini mazuio yaliyokuwa mipakani yameondolewa kwa mujibu wa taarifa na tunatarajia hivi karibuni mahindi yanaendelea kuingizwa Kenya kama kawaida,” alisema Balozi Simbachawene.

Mwishoni mwa wiki, Katibu wa Baraza la Mawaziri la Kilimo, Peter Munya alionekana kupinga barua ya AFA iliyopiga marufuku uagizaji wa mahindi.

“Hatujaacha kuingiza mahindi kutoka Uganda na Tanzania. Kile AFA imefanya ni kuangalia ubora wa mahindi yanayokuja nchini,” alisema Munya Jumatano ya wiki iliyopita.

Munya alisema  malori yaliyokwama kwenye mpaka wa Namanga yangesafilishwa baada ya kufanyiwa majaribio zaidi, kwani mtu akikausha mahindi kwa viwango vya kuondoa Sumukuvu ataendela na biashara.

Naye,Mkurugenzi Mkuu wa EAC anayeshughulikia Forodha na Biashara Keneth Bagamuhunda aklisema Kenya kwa sasa ni Mwenyekiti wa EAC na ikiwa imeanza kwa mtazamo huo basi bahati mbaya sana.

“Kuna utaratibu wa jinsi ya kupiga marufuku uingizaji wa bidhaa katika hali yoyote. Lakini hatujaona onyo au lalamiko lilioandikwa. Kwa hivyo hatua hiyo haijafuata utaratibu,” alieleza.

Kulingana na EAC, utaratibu sahihi ni Kenya ilipaswa kuibua jambo kutoka kwa Wizara ya Kilimo na kisha kuratibu malalamiko ya maandishi kupitia Wizara ya Afrika Mashariki.

Akizungumzia suala hilo, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, alisema Uganda haitalipa kisasi kwa sababu kufanya hivyo haitakuwa suluhisho la kudumu kwa shida.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e53f88bd5e5c4975deeda91efc10f54d.jpeg

UMOJA wa Vijana wa Chama ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi