loader
Bilioni 103/- kusambaza maji Songea

Bilioni 103/- kusambaza maji Songea

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme amesema serikali inajiandaa kutekeleza mradi unaofadhiliwa na Serikali ya India ili kumaliza kero ya maji katika Manispaa ya Songea.

Akizungumzia maadhimisho ya Wiki ya Maji yanayoanza leo hadi Machi 22, mwaka huu, Mndeme alisema ofisini kwake mjini hapa kuwa mradi huo unagharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 45.3 (Sh bilioni 102.91).

“Kinachoendelea hivi sasa kupitia wizara yetu ya maji ni hatua za manunuzi ya wakandarasi wa kutekeleza mradi huo mkubwa ambao utahusisha ujenzi wa bwawa la kuhifadhia maji ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji lita bilioni tano,” alisema Mndeme.

Alisema mradi huo pia utahusisha upanuzi wa mtambo wa kusafisha maji na kutibu maji safi zaidi ya lita milioni 51.4 kwa siku,ujenzi wa matanki manne ya kuhifadhi maji yenye uwezo wa lita milioni 18.2 na ulazaji wa mabomba yenye uwezo wa kusafirisha maji kilometa 190.3.

Alisema mradi huo utakapokamilika zaidi ya asilimia 95 ya wakazi wa Manispaa ya Songea watakuwa wanapata maji safi na salama.

Alisema wananchi wa Manispaa ya Songea wasio na huduma ya maji, kupitia mradi huo watapata maji na kuwezesha asilimia ya usambazaji maji kwenye manispaa hiyo kuongezeka kutoka asilimia 86.2 hadi 95 na kwamba lengo ni kufikia asilimia 100 ya kutoa maji katika miji ya Songea, Tunduru na Mbinga.

Mndeme alisema katika miji ya Mbinga na Tunduru serikali inatenga fedha kwenye bajeti ya kila mwaka kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kusambaza huduma ya maji kwa wananchi.

Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Ruvuma (RUWASA), Rebman Ganshonga alisema ili miundombinu ya maji iwe endelevu, wananchi wanatakiwa kuilinda na kuvitunza vyanzo vya maji kwa sababu serikali inawekeza fedha nyingi kwenye miradi hiyo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/bf85f6842244fc450658434982b10820.jpeg

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mradi wa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Songea

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi