loader
Dstv Habarileo  Mobile
…aahidi hakuna jambo litakaloharibika

…aahidi hakuna jambo litakaloharibika

RAIS Samia Suluhu Hassan amewatoa wasiwasi Watanzania kuwa hakuna kitakachoharibika baada ya kifo cha Rais John Magufuli na kuwahakikishia kuwa taifa liko imara, na sio wakati wa kutazama mbele kwa mashaka.

Rais Samia aliyasema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam jana baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, akichukua nafasi ya Dk Magufuli aliyefariki dunia juzi saa 12 jioni katika Hospitali ya Mzena alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya umeme wa moyo.

“Niwahakikishie kuwa tupo imara kama taifa, na sisi viongozi wenu tumejipanga vizuri kuhakikisha tunaendelea pale mwenzetu alipoishia,” alieleza Rais Samia katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa.

Alisema Tanzania inayo Katiba ambayo yeye (Samia) ameapa kuilinda na kuitumikia, iliyobainisha vizuri hatua za kufuata pale inapotokea tukio kama hilo la kumpoteza Rais akiwa madarakani.

“Isitoshe nchi yetu inayo hazina nzuri ya uongozi na misingi imara ya utaifa, udugu, umoja na ustahimilivu na nidhamu ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama iliyojengwa na viongozi wetu waliotutangulia kwa kuanzia na waasisi wetu hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na hayati Abeid Amani Karume,” alisema Samia.

Alisema pia wapo marais wengine waliostaafu wakifuatiwa na Rais Magufuli. “Niwahakikishie hakuna jambo litakaloharibika… Naomba niwaase Watanzania tusimame pamoja na kushikamana katika kipindi hiki cha maombolezo, huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama taifa, ni wakati wa kufarijiana na kuoneshana upendo,” alibainisha.

Samia alisema wakati huu pia ni wa kudumisha amani, kuenzi utu, uzalendo na utanzania, na si wakati wa kutazama mbele kwa mashaka bali kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini. Alisema pia si wakati wa kutazama yaliyopita bali ni wakati wa kutazama yajayo, si wakati wa kunyoosheana vidole bali kushikana mikono na kusonga mbele.

Aidha, alisema huu ni wakati wa kufutana machozi na kufarijiana kuweka nguvu kwa pamoja za kuijenga Tanzania mpya ambayo Rais Magufuli aliitamani.

Alisema Watanzania wote wanafahamu namna Rais Magufuli alivyoipenda nchi na kujitoa kuwatumikia watu wake.

“Sote tulishuhudia kiu, dhamira na nia yake njema ya dhati ya kutaka kuibadili nchi yetu na kuipatia mafanikio makubwa,” alisema Samia ambaye alikuwa Makamu wa Rais chini ya Dk Magufuli tangu Novemba 5, 2015.

Alisema pia watu wote ni mashahidi wa namna ambavyo amebadili taswira ya nchi kwa vitendo na kwa utendaji wake imara usiotikisika wala kuyumbishwa na kwa muda wote akimtanguliza Mungu.

“Sote tulisikia matamanio na maeneo yake makubwa kwa nchi hii aliyoyatafsiri katika mipango, mikakati na ujenzi wa miradi mikubwa,” alifafanua Samia.

Aliongeza kuwa “Mimi nilipata bahati ya kuwa makamu wake (Makamu wa Rais), alikuwa ni kiongozi asiyechoka kufundisha na kuelekeza kwa vitendo vipi anataka nchi hii iwe, na yapi yafanyike. Amenifundisha mengi, amenilea na kuniandaa vya kutosha.”

Alisema Tanzania imepoteza kiongozi shupavu, madhubuti, mzalendo, mwenye maono, mpenda maendeleo na mwana mwema wa Bara la Afrika, mwana mapinduzi wa kweli aliyekuwa chachu ya mabadiliko. “Kwa kweli tumepwelea kwa kuondokewa na kiongozi wetu huyu,” alisema Samia na kuwaomba Watanzania wawe na moyo wa subira, wajenge umoja na mshikamano katika kipindi hiki kigumu.

“Leo si siku nzuri sana kwangu kuhutubia taifa maana nimeelemewa na kidonda kikubwa kwenye moyo wangu na mzigo mkubwa mabegani kwangu. Kiapo nilichokula leo ni tofauti na viapo vyote nilivyowahi kula katika maisha yangu...” alisema Samia ambaye alitangaza msiba wa Dk Magufuli, Jumatano usiku.

Aliongeza, “Tofauti na viapo vya awali ambavyo nilivila kwa faraja, nderemo, vifijo na bashasha tele, leo nimekula kiapo cha juu kabisa katika nchi yetu ya Tanzania nikiwa na majonzi tele na nchi ikiwa imetandwa na wingu jeusi la msiba.”

Alieleza kuwa amekula kiapo hicho katika siku ya maombolezo hivyo atazungumza machache na kwamba atatafuta wasaa mwingine baadaye kuzungumza na kukumbushana juu ya mambo mengi yanayohusu taifa, mustakabali wake na matarajio ya Watanzania siku za usoni.

“Mtakumbuka Machi 17, mwaka huu, nikiwa Tanga kwa mara ya kwanza nilipata fursa ya kulihutubia taifa katika hali ya udharura na kutoa taarifa ya kifo cha mpendwa wetu. Nilitumia fursa ile kuwajulisha juu ya msiba ulioifika nchi yetu kwa kuondokewa na Rais wetu mpendwa na Amiri Jeshi wetu Mkuu Rais Magufuli,” alisema Samia.

Alikiri kuwa jambo hilo hakuwa amejiandaa wala kulitazamia kwa kuwa Tanzania haina uzoefu nalo wala hakuna rejea katika historia ya nchi.

“Ni kwa mara ya kwanza tumekuwa na historia ya namna hii ya kumpoteza rais wa nchi, ni mara ya kwanza kwa aliyekuwa Makamu wa Rais kuapa kuwa rais katika mazingira ya namna hii,” alieleza.

Alitoa salamu za rambirambi kwa mjane Mama Janet Magufuli, mama mzazi wa marehemu Suzan, watoto, familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa kuondokewa na kipenzi chao na mhimili muhimu wa familia.

“Natambua ukubwa wa ombwe ambalo ameliacha katika familia. Nitumie fursa hii kuwahakikishia kuwa tunaungana nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na kuahidi kuendelea kuwashika mkono na kuwafariji,” alisema.

Alitoa salamu za rambirambi kwa wananchi kwa pigo hilo kubwa, na kuuelezea msiba huo kuwa mzito na ambao haukutarajiwa. Alishukuru mhimili wa Bunge, Mahakama pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa kuwa naye bega kwa bega katika kipindi chote cha msiba.

Pia alishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuwajibika na kuhakikisha nchi inakuwa salama wakati wote, na wanhabari kwa kupasha habari za msiba huo.

Baada ya kula kiapo na kuzungumza na wananchi, Rais Samia aliongoza kikao cha Baraza la Mawaziri na pia alipata fursa ya kumtembelea na kumfariji Mama Janet Magufuli na familia yake, na kwenda kuweka saini katika kitabu cha maombolezo katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi