loader
Dstv Habarileo  Mobile
Washairi, wapenzi wa   Kiswahili wamlilia JPM

Washairi, wapenzi wa  Kiswahili wamlilia JPM

WASHAIRI nchini wamemlilia aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli na kueleza kuwa alikuwa jasiri na kiongozi aliyeipaisha lugha ya Kiswahili na watamuenzi daima kwa tungo maridhawa.

Walieleza hayo jana wakati wakizungumzia Siku ya Ushairi Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Machi 21.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza), Dk Mwanahija Ali Juma akizungumza na HabariLeo alisema Watanzania wamepata msiba mzito hasa wana Kiswahili kwani Magufuli aliienzi lugha hiyo wazi wazi hivyo watamkumbuka daima.

“Alifanya juhudi za hali ya juu sana kukipaisha Kiswahili na kukipigania ilimkiwe juu kuliko ilivyotarajiwa. Alihakikisha Kiswahili kinatumika kila eneo na kila sekta katika jamii, alikuwa mfano halisi hata katika mikutano ya kimataifa hakusita kuzungumza Kiswahili,” alisema.

 Dk Juma alisema akiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mwaka 2019/2020, Magufuli alipeleka ajenda ya kupitisha Kiswahili kuwa lugha ya nne ya jumuiya hiyo hatua iliyoleta sifa kubwa ulimwenguni.

Alisema hatua hiyo ilipelekea nchi za Afrika Kusini na Zimbabwe kuamua kufundisha   lugha hiyo katika shule na vyuo vyao.

“Alikuwa mstari wa mbele kutumia Kiswahili na kutaka kitumike katika maeneo ya utafiti, sheria na kwingineko. Alitaka hukumu za kesi zitolewe kwa Kiswahili ili mwananchi wa kawaida aweze kuelewa, hii ilidhihirisha jinsi alivyokipenda Kiswahili na kukipa hadhi.”

“Februari Mosi katika maadhimisho ya miaka 100 ya Mahakama Kuu, alimpandisha cheo Hakimu Zephrine Galeba kuwa Jaji wa Mahakama Kuu baada ya kuandika na kutoa hukumu kwa Kiswahili mwaka 2020,” alisema.

Dk Juma alisema wakati wa uhai wa Magufuli walishaanza kumuenzi kwa kutunga mashairi na kumpa nishani ya Shaaban Robert katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili mwaka huu kwa namna alivyoziunganisha kwa mara ya kwanza taasisi mbili za Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza) na Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) kuadhimisha kwa pamoja siku hiyo jijini Dodoma. Alisema mwakani maadhimisho hayo yatafanyika Zanzibar.

Alisema pamoja na mashairi na nishani hiyo, pia watatunga wimbo wa kutambua mchango wa Magufuli katika kukuza lugha ya Kiswahili na pia watatunga vitabu kumuenzi kwa vitendo kwa yale aliyofanya.

Mshairi chipukizi, Stella Nyemenohi alisema Rais Magufuli alikipaisha Kiswahili na kutoa wito kwa wapenzi wa mashairi nchini kutumia lugha hiyo kutunga mashairi kwani ndio nyenzo muhimu.

“Ushairi unafikisha ujumbe kwa jamii bila mgogoro wowote, mtu atapata ujumbe, ataumia au kufurahi, lakini ataujibu kwa ushairi hivyo hivyo. Ni Sanaa inayowasilishwa kwa Kiswahili kwa upande wa Tanzania hivyo kipindi hiki ambacho Rais Magufuli alikipa hadhi, mtu yeyote angetunga shairi kwa Kiswahili,” alisema Nyemenohi ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari.

Alisema ana uhakika Rais mpya, Samia Suluhu Hassan atakiendeleza Kiswahili.

Maadhimisho ya Siku ya Ushairi Duniani yalipitishwa rasmi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) mwaka 1999.

foto
Mwandishi: Gloria Tesha 

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi