loader
Mawaziri waeleza Magufuli alivyowaimarisha

Mawaziri waeleza Magufuli alivyowaimarisha

BAADHI ya mawaziri wameeleza walivyomudu kufanya kazi na Rais John Magufuli kwa kusema aliwajenga, kuwaimarisha na kuwafundisha kuchapa kazi wakiweka mbele maslahi ya Watanzania wanyonge.

Wakizungumza katika shughuli ya kuaga mwili wa Magufuli jana Dar es Salaam, mawaziri hao wamebainisha utayari wao wa kuchapa kazi zaidi chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwaa kuendeleza aliyoacha mtangulizi wake na mapya atakayoanzisha.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo, alisema kifo cha kiongozi huyo ni pigo kubwa.

“Kwangu pia ni pigo nimefanya kazi kama msaidizi wa Rais kwa kipindi chote, alinipa wizara ngumu na yenye changamoto nyingi pamoja na hayo alinipa dhamana hiyo kipindi cha kwanza na cha pili,” alisema Jafo.

Alisema atamuenzi kwa kufanya kazi zaidi kuhakikisha anatimiza Magufuli aliyotarajia kufikia kiongozi huyo.“Ninafahamu Mama Samia ni mzoefu si mtu mgeni na anajua maono yote Rais alikuwa anataka. Watanzania tunaenda njia sahihi,” alisema Jafo.

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu alisema Rais Magufuli alimfundisha kuipenda Tanzania na wananchi.

“Hata unapokuwa waziri ana ku-challenge, je haya maamuzi unayotaka kuyatoa yana maslahi ya Watanzania wanyonge? Ina maana hata mipango yako lazima izingatie maslahi ya wanyonge,” alisema Ummy.

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema chini ya Rais Magufuli, alijifunza uwezo wa kiongozi kufanya uamuzi. “Alisisitiza kuwa mtu asiogope kufanya maamuzi ni heri ukosee kufanya maamuzi kuliko kutofanya kabisa maamuzi,” alieleza Bashe.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-Tamisemi, David Silinde alimuelezea Dk Magufuli kuwa alikuwa  mtu mwenye uthubutu na kwamba nchi imepoteza mwamba, kiongozi, baba na mtu aliyetumia muda wake kujenga na kutetea taifa.

“Tunamuombea Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) Mungu ampe ujasiri na kwa kuwa walifanyakazi pamoja kuhakikisha anaendeleza yale yote aliyoyaanzisha na kuyaacha,” alisema Silinde.

Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mwita Waitara alisema hawawezi kumsahau Magufuli kutokana na nafasi alizompa kitendo kilichoonesha kuwa alimwamini.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe alisema kwa mara ya kwanza Rais Magufuli alimteua mwaka 2016 kuwa Mkuu wa Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, nafasi aliyoishika kwa kipindi cha miezi 10 na baadaye alimteua kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

 “Namshukuru kwa kuniamini…Alikuwa anajali utaalamu na ushauri na mimi kama mchumi katika eneo la biashara na uchumi wa kimataifa nilimshauri na nashukuru hata nilipoamua kugombea Masasi Mjini aliniruhusu na ndani ya chama nilipitishwa,” alisema Mwambe na kuongeza kuwa anamshukuru kwa imani yake kwa kuteua mara nne tofauti.

Msemaji wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi alisema ni ngumu kwa viongozi vijana ambao Dk Magufuli aliwapatia nafasi kuonesha uwezo.

“Ni mapema sana kuzungumzia yale ambayo yapo mioyoni mwetu. Tukipata nafasi hapo baadaye tutasema. Ila kwa uchache alikuwa ni kiongozi mwenye maono na mwana mageuzi na mpenda mageuzi. Katika eneo lako unalofanyia kazi alitaka utekeleze usimamie sheria na uwe mtekelezaji,” alisema Dk Abbasi.

 

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/438fc9ebe81a5f6b3eab8b78b6bacb4e.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi