loader
Kikwete: Tanzania ipo mikono salama

Kikwete: Tanzania ipo mikono salama

RAIS wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ameeleza namna alivyopata ugumu kupokea taarifa kuhusu kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, lakini akasema wananchi wasiwe na hofu kwa kuwa Tanzania ipo katika mikono salama.

Kikwete aliyasema hayo jana kupitia ukurasa wake wa twitter.

Alisema jambo la faraja kubwa kwa Watanzania ni kuwa mrithi wa Hayati Magufuli, Rais Samia Suluhu Hassan, alikuwa Makamu wa Rais wa Rais Magufuli tangu mwaka 2015 hadi umauti ulipomkuta Magufuli, hivyo anajua undani wa yale yaliyofanyika na yanayohitaji kukamilishwa.

Rais mstaafu huyo alisema Rais Samia anayajua yaliyopangwa kufanyika katika miaka mitano ijayo, hivyo hana shaka kuwa Tanzania ipo katika mikono salama.

“Nampongeza Rais Samia kwa hotuba fupi na nzuri aliyoitoa baada ya kuapishwa na yenye kujenga imani na kuleta matumaini. Tumuombee Rais wetu kwa Mwenyezi Mungu amuongoze vyema kwa kila uamuzi atakaochukua na kila hatua atakayopiga,” alisisitiza Kikwete.

Aliongeza: “Niwaombe Watanzania wenzangu tumpe ushirikiano ili aweze kuongoza Tanzania kwa ufanisi na mafanikio zaidi.”

Alitoa salamu za mkono wa pole na rambirambi kwa mjane wa marehemu, Mama Janet Magufuli na familia yake nzima.                

Kuhusu namna alivyoandika ujumbe huo katika ukurasa wa twita, Kikwete alisema: “Nimepata tabu kuandika kwa kifupi kuelezea simanzi na masikitiko yangu kwa msiba mkubwa ulioukumba nchi yetu kwa kuondokewa na mpendwa wetu Mheshimiwa Rais Magufuli, nimelazimika kuyaambatanisha hapa chini, Mwenyezi  Mungu amuwekea mahali pema, peponi.”

Akaongeza: “Ni pigo kubwa, tena ni kubwa lisilomithilika. Rais wetu mpendwa John Magufuli ametutoka ghafla bila ya kutazamia. ‘I never saw this coming’ (Sikulitarajia hili). John Pombe Magufuli ametutoka wakati ambapo uongozi wake ulikuwa unahitajika sana.”

Kwa mujibu wa Rais Mstaafu Kikwete, bado Watanzania walikuwa wanamhitaji kiongozi huyo kukamilisha aliyoyaanza na kufanya mazuri mengi aliyokuwa amepanga kuifanyia nchi na wananchi wake.

“Tungetamani John Magufuli tuendeee kuwa naye leo na miaka mingi ijayo, lakini mapenzi ya Mungu hatuna uwezo wa kuyabadili… Wajibu wetu ni kumuombea kwa Mola ampe mapumziko. Daima tutamkumbuka Rais Magufuli kwa mema mengi aliyoifanyia nchi yetu. Hakika Tanzania imepoteza kiongozi mzalendo wa dhati, shupavu, mahiri na makini,” alisema.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/f20471015a86cf3122684ac627f95722.jpg

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi