loader
Mwinyi, Kikwete wasaini kitabu cha Magufuli

Mwinyi, Kikwete wasaini kitabu cha Magufuli

MARAIS wastaafu akiwemo Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete wameungana na wananchi kusaini kitabu cha maombolezo ya kifo cha Rais wa John Magufuli.

Rais mstaafu Mwinyi alifika katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam na kusaini kitabu hicho akafuatiwa na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania Mohamed Gharib Bilali, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, na Mkurugenzi wa Mashitaka Biswalo Mganga.

Akizungumza mara baada ya kusaini kitabu hicho katika viwanja vya Karimjee, Dk Kikwete alisema kifo cha Magufuli hakikutarajiwa na taifa lilimuhitaji.

“Kwa kweli kifo chake hakikutarajiwa, tulitegemea kwa kweli aendelee kuliongoza taifa kwani katika mhula wake wa kwanza aliliongoza taifa vizuri sana…….naamini kuwa yale ambayo hayakukamilika, Rais wa Jamhuri ya Tanzania mhe. Samia Suluhu Hassan atayaendeleza kikamilifu,” amesema Dk Kikwete na kuwasihi watanzania kuendelea kudumisha uzalendo, fikra na maono aliyokuwa nayo Hayati Dk Magufuli.

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alifika na kusaini kitabu hicho akifuatiwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zubeir Ali Maulid alisema, Rais Magufuli katika kipindi kifupi cha uongozi wake alifanya mambo mengi yatakayobaki kuwa historia Tanzania.

“Msiba huu ni wetu sote watanzania na umetugusa sana kwani  hayati Magufuli ameyafanya mengi katika mhula wake wa kwanza ambapo mengi hayo tumekuwa tukinufaika nayo sisi watanzania…kwa sasa tushikamane kudumisha umoja wetu ili kuweza kusonga mbele kimaendeleo,” alisema Maulid.

Viongozi waandamizi wa serikali na mabalozi waonaziwakilisha nchi zao nchini wamesaini kitabu hicho na kuwataka Watanzania kuendelea kudumisha uzalendo, fikra na maono ya Magufuli ili kuiwezesha Tanzania kukua kimaendeleo.

Naibu Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Prefere Ndayishimiye alisema msiba wa Magufuli umewagusa kwa kuwa alikuwa kiongozi aliyependwa na kujulikana na bara la Afrika.

“Amefanya maendeleo makubwa ambapo naamini kuwa vizazi vijavyo vitayaona na kuendeleza pale alipoishia Dk Magufuli,” alisema Ndayishimiye.

Wananchi pia walijitokeza kwa wingi kusaini kitabu hicho na kumuelezea Magufuli kuwa alikuwa kiongozi aliyeweka maslahi ya nchi mbele kwa manufaa ya Watanzania.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi