loader
Marekani yampongeza Rais Samia

Marekani yampongeza Rais Samia

VIONGOZI katika mataifa mbalimbali wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuiongoza Tanzania kuchukua nafasi ya John Magufuli.

Miongoni mwa waliompongeza ni Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris.

Samia aliapishwa Machi 19, mwaka huu katika Ikulu ya Dar es Salaam.

Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, mwaka huu katika Hospitali ya Mzena alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kusumbuliwa na maradhi ya umeme wa moyo.

Kupitia ukurasa wa twitter Kamala alimhakikishia Rais Samia ushirikiano ili kuendelea kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo.

“Ninamtakia kila la kheri Samia Suluhu Hassan kufuatia kuapishwa kwake kuwa Rais mpya wa Tanzania na mwanamke wa kwanza kuongoza ofisi hiyo. Marekani ipo tayari kufanya kazi na wewe ili kuimarisha uhusiano baina ya nchi zetu,” aliandika Kamala.

Rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf alimpongeza Samia na kumtakia heri.

“Natuma salamu zangu za pongezi kwa Rais Samia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya urais nchini Tanzania, namuombea uongozi bora na kuliongoza taifa hilo katika maendeleo,”alisema.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni pamoja na kutangaza siku 14 za maombelezo, pia alimpongeza Samia kwa kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania.

“Wakati tukiwa katika kipindi hiki kigumu, naomba nimpongeze Rais Samia kwa kuapishwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania na kuwa Mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo. Tunakuombea kwa Mungu uliongoze taifa hilo vyema,” alisema Museveni.

Rais wa Nigeria, Mohammed Buhari alimpongeza Rais Samia kwa kuapishwa kuwa Rais huku akimsisitiza kuliunganisha taifa hilo na kuliongoza kwenye mafanikio.

Malkia Elizabeth alituma salamu za rambirambi kwa Watanzania kutokana na msiba huo wa Dk Magufuli.

Kupitia ukurasa wa twitter, Malkia alisema yeye na mwana mfalme Philip wamesikitishwa na taarifa ya kifo cha Rais John Magufuli na kutaka salamu zake za dhati ziende kwa wapendwa wake na raia wa Tanzania.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/48a9156d17519e29b757a620769a1480.jpg

MKUU wa Mkoa wa Geita, ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi