loader
Dstv Habarileo  Mobile
Watanzania kifo cha JPM

Watanzania kifo cha JPM

TANZANIA imeandika historia ya kuwa na rais mwanamke wa kwanza kwenye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Huyu ni aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Aliapishwa Machi 19, 2021 kushika wadhifa huo kutokana na kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli kilichotokea Machi17, 2021.

Baada ya kuapa, Rais Samia aliyeonekana kujawa majonzi na alizungumza kwa kifupi na kutoa ratiba ya mazishi ya mwili wa aliyekuwa Hayati Magufuli.

Akasema kutakuwa na vituo vinne (Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Zanzibar na Chato mkoani Geita) vitakavyotumika kwa kuaga ili wananchi wengi watoe heshima za mwisho kwa mpendwa wao kabla ya mazishi Machi 26, 2021.

“Leo si siku nzuri ya kwangu kusema, kutokana na kidonda kikubwa moyoni na mzigo mzito nilio nao. Nimekula kiapo katika mazingira tofauti, nimezoea kula kiapo katika hali ya nderemo na furaha, lakini leo nimekula kiapo katika hali ya huzuni na masikitiko,” alisema Rais Samia.

 

Kama ilivyotarajiwa na Watanzania wengi kuona faraja kubwa na kupata matumaini kutoka kwa Rais huyu mpya ndivyo ilivyokuwa baada ya Rais Samia kusisitiza kuwa, katika kipindi hiki cha maombolezo ni taifa halina budi kuzika tofauti zozote.

 

“Kipindi hiki cha maombolezo, ni kipindi cha kuzika tofauti zetu; huu ni wakati wa kuwa wamoja na si wakati wa kutazama yaliyopita, huu si wakati wa kunyosheana vidole, bali wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kuweka mbele nguvu kwa pamoja ili kujenga Tanzania ambayo Magufuli aliitamani, na zaidi sana tuungane kumwombea Hayati Magufuli alale pema peponi,” alisema.

 

Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Samwel Malecela,  amesema Taifa linapitia katika kipindi kigumu jambo la muhimu  ni kuendelea kushikamana kama Watanzania ili kupita kwenye kipindi hiki kwa umoja na upendo.

 

Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, katika ukurasa wake wa twita ameandika: “Nimesikiliza hotuba ya Mheshimiwa Rais Samia, ni hotuba nzuri ambayo ndani yake ina tiba, inafuta machozi, inaunganisha, inatibu tofauti zetu na kuendeleza mazuri yaliyoasisiwa na viongozi waliopita.” 

 

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro, anaona kuwa pamoja na kuondokewa na Jemedari Mkuu Hayati John Magufuli, Mungu ataivusha nchi na Tanzania itaendelea kuwa imara.

 

“Taifa hili ni imara, Mungu amelipendelea sana, halikuwahi kuyumba wala kutetereka katika nyakati zote za changamoto; yalipotokea maasi ya kijeshi mwaka 1964, alipofariki Mzee Karume mwaka 1972, nyakati mbaya za njaa, nzige na vita ya Uganda miaka ya 1970 na 1980, alipofariki Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine mwaka 1984 na alipong’atuka madarakani na kufariki Mwasisi na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,” alisema.

 

Mtatiro akaongeza: “Tusiogope na tusitetereke, sisi ni taifa imara siku zote, nyakati zote.” 

 

Rais Samia aliyashukuru makundi ya watu mbalimbali kwa kuendelea  kushikamana na serikali yake, makundi hayo ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi, viongozi wakuu wastaafu, vyombo vyote vya ulinzi na usalama na viongozi wa dini.  

 

Kwa namna ya pekee, amewashukuru wasanii na waandishi wa habari kwa kuendelea kutumia taaluma zao kuwaunganisha Watanzania katika kipindi hiki cha maombolezo.

 

Baadhi ya wasanii wakongwe wa muziki na waandishi wameonekana kuguswa na hotuba hii na kutoa yaliyo mioyoni mwao.

 

“OOOh, No. ungekuwepo wakati tunaangalia hii hotuba ilibidi tukae tuangalie kwenye luninga, mimi binafsi nilikuwa ninanena kwa lugha nakumbuka nilikuwa nimezungukwa na vijana nikawaamuru watulie kwa sababu sasa huu ndiyo wakati wa Bwana, nikawaambia Mungu alipotaka kuwakomboa Taifa la Isirael kutoka utumwani, alimtumia mwanamke na kwamba aliweka hekima ndani ya mwanamke na wakati huu Mungu ameweka mwanamke kwa maana kuna jambo ambalo Mungu anataka kutuingiza,” amesema Christina Shusho, mmoja wa waimbaji wakongwe wa nyimbo za Injili nchini.

 

Shusho anasema: “Katika hali hiyo, nimewaambia wenzangu kuwa sijui naona nini kwa kuwa nilikuwa natazama katika mtazamo wa kiroho, nikasema nahisi Tanzania sasa tunakwenda kwenye viwango vingine, viwango ambavyo mtu yeyote wa nchi jirani kama alikuwa na mpango wa kutucheka, basi watafikiri mara mbili tena.”

 

“Hii ni kwa sababu tumevunja rekodi kwa namna ya tofauti kwani haijawahi kutokea kiongozi mwanamke kushika nafasi hii ya juu kabisa tena kwa namna yake kwa hiyo, Mungu ametupaisha hata kama ni katika hali ya maumivu, lakini haijalishi.”

 

Anaongeza: “Mimi napenda kwenda na Neno la kinabii; Rais Samia ametuheshimisha sana wasanii wa Tanzania maana kuna makundi mengi, lakini wasanii tumependelewa tumetajwa katika hotuba ya kwanza; natambua makundi mengine yataendelea kutajwa.” 

 

Kuhusu kifo cha Dk Magufuli, anasema: “Kama kuna watu walioumizwa na kifo chake, mimi ni mmoja wao; nimepokea kwa mshituko mkubwa kwa kuwa Rais  Magufuli alikuwa mtu wa mfano wa kuigwa kwa kuwa alikuwa ni mtu anayefikiria, anaamua nakuanza kulifanyia kazi mara moja na mara zote  anapoanza kufanya vitu vyake, amekuwa akimtanguliza Mungu.”

 

Anasema mafunzo aliyoyaacha kwake kama msanii na mwananchi wa kawaida, lakini kama Mkristo ni kwamba mahali popote, ni muhimu kuwa na ujasili na kwa kujiamini unapotaka kufanya jambo na siku zote, usifikirie kufanya jambo dogo.  

“Nimekuwa, nikiwaambia watu hata hapa kanisani kwangu kama kuna wakati ambao Mungu ametuletea, kiongozi basi kilikuwa kipindi cha huyu baba (Magufuli) kwa sababu haogopi kufanya jambo analoamini lina manufaa kwa jamii na ni jema mbele ya Mungu; hapo haogopi mazingira anachoona ni kwamba tukishafanya, hiki tuamini kuwa Mungu atatenda,” amesisitiza Shusho.

 

Amesema jambo lingine kubwa ni kuwa Magufuli hakuona haya kumtambulisha Mungu wake katika kila hatua aliyopita pamoja na nafasi aliyokuwa nayo.

“Kuna watu ambao tunampenda Mungu tunamjua Mungu tunapokuwa chini, tukiinuliwa hivi kama mimi wa ‘Bwana Yesu Asifiwe,’ unakuta vinapungua kwa sababu ya nafasi niliyoipata, lakini Rais Magufuli hakuacha kumsema Mungu wake wakati yeye ndiye alikuwa Kiongozi Mkuu Namba Moja katika nchi,” alisema.

 

Msanii mwingine nguli nchni, Mrisho Mpoto, anasema wasanii na wanamziki wataendelea kumkumbuka Magufuli kwa kuwa hakuwabagua, bali kila msanii alimfanya sawa na mwingine kiasi cha kumfanya kila msanii ajione anapendwa na rais wanchi.

 

“Utakumbuka mtindo wake wa kuwavisha kofia yake, alijitahidi sana kwa kadiri alivyoweza kufanya hivyo kwa kila msanii,” alisema Mpoto.

Akaongeza: “Mimi binafsi aliwahi hata kunitambulisha kuwa ni mwanamziki bora kabisa na alikuwa shabiki wangu; alikwenda mbai zaidi kwa kuimba baadhi ya nyimbo zangu mbele ya umati wa  watu.”

 

Mwandishi wa habari wa kujitegemea, Dotto Mwaibale, anasema falsafa ya Magufuli ya kuthamini sanaa na utamaduni wa nchi yake imewafanya wasanii wengi kujiamini na kufanya mambo makubwa tofauti na zamani kwani watu wengi waliamini kuwa, wasanii wa nchi jirani waliokuwa wakiimba kwa kutumia lugha za kigeni ndio  bora.

 

Anasema falsafa ya Hayati Magufuli ya kuenzi lugha ya Kiswahili duniani, imewafanya hata viongozi wakuu barani Afrika kufikiria kuanza Kiswahili kama lugha rasmi katika nchi hizo.

 

Anasema waandishi wa habari watamkumbuka kwa mapinduzi makubwa aliyoyafanya kuboresha sheria za vyombo vya habari nchini.

 

Mwandishi wa Makala haya ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo anapatikana kwa jmapepele1@ gmail.com au 0784441180.

foto
Mwandishi: John Mapepele

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi