loader
Magufuli alivyofanya mageuzi makubwa CCM

Magufuli alivyofanya mageuzi makubwa CCM

NDANI ya kipindi cha miaka karibu sita ya uenyekiti wa Rais John Magufuli, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa na mageuzi makubwa ya kimuundo, kiutendaji na kiuchumi.

Dk Magufuli alishika wadhifa huo wa uenyekiti kutoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Julai, mwaka 2016 baada ya kupitishwa na wanachama wa chama hicho kwa kishindo.

Mageuzi hayo ni pamoja na muundo wa uongozi wa chama hicho, kuondolewa kwa wanachama waliokuwa wakijali zaidi maslahi yao na pia kuweka uwazi katika michakato ya kutafuta viongozi, watakaokiwakilisha chama hicho.

Dk Magufuli alisema wakati wa uhai wake kwamba baada ya kuwaondoa mafisadi waliokuwa wanatafuna mali za chama hicho, thamani ya mali za chama hicho ilipanda huku mapato yake yakifikia Sh bilioni 59.8 kwa mwezi.

Alipochukua uenyekiti, chama hicho kilikuwa kikiingiza mapato ya Sh bilioni 191 kwa mwaka na mali nyingi zilikuwa chini ya watu wachache, hali iliyokifanya chama kuwa hoi kiuchumi na kuwa ombaomba licha ya kuwa na mali nyingi.

Dk Magufuli alisema hayo jijini Mwanza mwaka jana wakati akifungua semina ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM.

“Nilipopewa ridhaa ya kuongoza chama, nilitambua haja ya kufanya mageuzi makubwa ndani ya chama, kimuundo, kiutendaji na kiuchumi lengo ni kuondoa urasimu na kuongeza ufanisi na kukijenga chama kiuchumi,” alieleza.

Alisema mageuzi hayo yalikuwa hayaepukiki ili kujenga imani ya chama kwa wanachama, lakini pia kujenga serikali imara, hali ambayo pia itazaa taifa imara.

Alisema hali ya chama hicho kiuchumi na hata kimuundo, haikuwa inafurahisha. 

Alisema kuwa ilikuwa vigumu kwake kuzungumzia mageuzi makubwa ndani ya serikali, ilihali chama tawala kiko hoi.

Alitaja mageuzi aliyoyafanya kwenye chama hicho kuwa ni: Kupunguza idadi ya wajumbe katika Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC) kutoka 342 hadi 168 na kuwaondoa makatibu wa mikoa katika orodha ya wajumbe wa NEC kwa sababu ni watendaji.

Mabadiliko mengine yalikuwa ni kuondoa kada ya Katibu Msaidizi na Mhasibu wa Wilaya na Mkoa na majukumu yao kutekelezwa na katibu mmoja wa wilaya  na katibu wa mkoa.

Aidha, alisema aliamua kuunganisha utumishi wa chama na jumuiya ili uwe chini ya Sekretarieti ya NEC; na kufuta nafasi ya Katibu wa NEC wa Mkoa hadi Tawi.

Magufuli alifafanua kuwa pamoja na wingi wa mali za CCM, mapato ya chama hicho yalikuwa kidogo sana, kiasi cha chama kushindwa kujiendesha.

“Mali nyingi ziliwanufaisha wachache na baadhi ya viongozi walijimilikisha mali hizo. Chama kilibaki kuwa ombaomba na kutegemea fedha za matajiri wachache waliojiita wafadhili wa chama,” alieleza.

Alisema matajiri hao wachache, ndio walikuwa na maamuzi makubwa ndani ya chama na hakukuwa na mtu aliyefurukuta. “Tukasema haiwezekani kamwe uozo huu uendelee chini ya uenyekiti wangu na uongozi wenu, tukachukua hatua,” alisema Magufuli.

Alifafanua kuwa hiyo ndio sababu ya kuunda Tume ya Kuhakiki  Mali za CCM chini ya Dk Bashiru Ali (Katibu Mkuu wa CCM ).

“Tume hiyo ilifanya kazi kwa weledi na kubaini kuwa kwa miaka mingi CCM ilikuwa ni shamba la bibi, kila mtu alikuwa akitafuna mali za chama mahali alipo.

“Tukaanza kazi ya kurejesha mali za chama ikiwemo vyombo vya habari kama Channel 10, ambayo pamoja na kuwa mali ya CCM lakini haikuwa chini ya CCM, tukarejesha majengo, vituo vya mafuta, vitalu”. 

Aidha, alisema katika mageuzi hayo, pia walipitia upya mikataba ya uwekezaji ikiwemo Vodacom, jengo la makao makuu ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Dar es Salaam na kuanzisha mfumo wa eletroniki wa usimamizi wa mali na rasilimali za chama hicho.

Alisema jitihada hizo za udhibiti wa mapato ya chama kupitia makao makuu ya CCM, ziliongeza mapato ya chama hicho kutoka Sh bilioni 46.1 mwaka 2015/16 hadi Sh bilioni 59.8 mwaka 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia 30.

Alisema pia baada ya kuthaminisha upya mali za chama, thamani yake imeongezeka kutoka Sh bilioni 41.033 mwaka 2016/17 hadi Sh bilioni 974.66 sawa na ongezeko la asilimia 2,275.2.

“Nimearifiwa zoezi la tathmini limefanyika katika mikoa 13 tu. Nina uhakika mikoa mingine nayo itafanyika tathmini na mali za chama zitakuwa ni mabilioni kwa mabilioni,”alisema.

Alisema endapo wataendelea na jitihada hizo, CCM itaweza kujitegemea kwa asilimia 100 na kuachana na kutegemea fedha za wafadhili. Pia maslahi ya watumishi wa chama yataongezeka.

Akizungumzia mafanikio ya wanachama ndani ya chama hicho, alieleza kuwa chama hicho kimepokea wanachama mbalimbali kutoka upinzani na hali hiyo imeongeza ruzuku kutoka serikalini kutoka Sh bilioni 12.4 mwaka 2015/2016 hadi Sh bilioni 13.5 kwa mwaka hivi sasa.

Alieleza kuwa mwelekeo wa Sera za CCM kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2010 hadi 2020, ilijielekeza kujenga uchumi wa kisasa na kuwawezesha wananchi. “Ilani ya uchaguzi 2015/20 iliandaliwa kuelekea mwelekeo huo.

Hata hivyo, alikiri kuwa serikali haikutumia ilani kama Msahafu au Biblia, kwani pamoja na kutumia ilani hiyo katika kutekeleza mambo mengi, lakini serikali haikujizuia kufanya jitihada nyingine zenye maslahi kwa taifa.

“Tuliona kuna umuhimu wa kuangalia mahitaji halisi ya watanzania na kuchukua hatua mwafaka na kukubaliana kuwa kuna baadhi ya hatua zinapaswa kuchukuliwa hata kama hazipo kwenye ilani,”alisisitiza.

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole anasema katika mageuzi hayo chama hicho kinaangalia idadi ya watumishi na uwiano wa uzalishaji kama vinaendana, weledi na mahitaji ya rasilimali watu, kiwango cha elimu pamoja na taarifa za wote wanaopokea mshahara kwani amedai kuwa CCM ndio chama pekee chenye watendaji wenye mishahara.

Anasema CCM ndio chama kikubwa Afrika, na kina watumishi wilaya zote nchini hivyo, mageuzi hayo yatakuwa na msaada wa kupata taarifa sahihi za uhakiki wa watumishi wake ndani ya chama.

Mageuzi ya Chama hicho kwa wafanyakazi wake, sawa na ule uliofanywa kwa watumishi wa serikali tangu mwaka 2016 ambao uliwabaini zaidi ya watumishi hewa 19,000.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/c5b17669186b351a87a7aa8693d2b70b.jpg

MATUMIZI mengi ya bidhaa za tumbaku ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi