loader
Dstv Habarileo  Mobile
Majaliwa: Kifo cha JPM ni msiba Afrika

Majaliwa: Kifo cha JPM ni msiba Afrika

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kifo cha Rais John Magufuli si msiba wa Tanzaniam pekee, bali wa Afrika tu kwa kuwa alikuwa mmoja wa viongozi katika Bara la Afrika.

Majaliwa alisema jana jijini Dodoma kuwa, kuja kwa viongozi 17 wa Afrika kumuaga Rais Magufuli ni ishara kuwa anakumbukwa kwa mema aliyotenda.

Aliyasema hayo katika viwanja vya Bunge muda mfupi kabla ya wabunge kuuaga mwili wa Rais Magufuli. Mwili wa kiongozi huyo ulifikishwa Dodoma juzi saa moja usiku na ukapelekwa Ikulu ya Chamwino.

“Binafsi inanipa shida kusema kiongozi wetu akiwa hapa kwa sababu wakati wote naona kama vile anazingumza na mie, ananipigia simu, maagizo, kwa hiyo inanipa shida kidogo kwa hiyo naomba mnivumilie,” alisema.

Alisema jana ilikuwa siku ngumu kwa wabunge hasa kwa kutambua namna walivyofanya kazi na Rais Magufuli na alivyoweka alama majimboni, vijijini, kata, halmashauri, na mikoani.

Majaliwa alisema Magufuli alifanya mema mengi na ushahidi ni namna maelfu walivyojitokeza Dar es Salaam na Dodoma kumuaga, hivyo Watanzania na wenye mapenzi mema wamwombee.

Alisema ratiba ya kuaga imebadilishwa ili kila mmoja aone hata jeneza tu kwa kuwa watu ni wengi wanaotamani kumuaga kiongozi wao. 

“Badala ya kwenda kuangalia na kuaga kwa kumuangalia, tutakachokifanya ni kuzungusha angalau mara mbili tatu uwanjani halafu baadaye tutapita kwenye mitaa maarufu ili angalau wengi wapate nafasi,” alisema Majaliwa

 Akongeza: “Tumeshuhudia watoto wadogo, wa umri wa kati, mpaka wazee, tukiruhusu kila mmoja kwenda pale hatutamudu kwa saababu familia imetutaka mwili huu ulale siku ya tarehe 26.”

Alisema utaratibu huo utatumika leo Zanzibar, kesho Mwanza, na Chato ambako atazikwa Ijumaa wiki hii. 

“Waheshiwa wabunge tuna jambo kubwa la dua, leo tupo nae hapa ametutangulia mbele za haki, mama yake mzazi yuko kitandani kwa miaka miwili. Tuwaombee wote wawili, mama apate nguvu ainuke, nae pia alazwe mahala pema,” alisema Majaliwa.

Awali, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi, alisema jijini Dodoma kuwa katika viwanja mikoani baada ya viongozi kuaga jeneza litapitishwa walipokaa mwananchi majukwaani wampungie na pia litapitishwa kwenye barabara zilizopangwa.

“Watanzania tuendelee kumuombea dua kiongozi wetu, alikuwa mwanamageuzi, mwana maono na mtekelezaji makini. Tumuenzi kwa amani na kwa utulivu”alisema Dk Abbasi.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi