loader
Viongozi Afrika wamtaja JPM mzalendo wa kweli

Viongozi Afrika wamtaja JPM mzalendo wa kweli

VIONGOZI wa Afrika wameeleza masikitiko yao kwamba bara hili limempoteza mzalendo wa kweli, Dk John Magufuli ambaye alisimama kidete kuongoza watu wake huku akitetea maslahi ya watu wake na bara hili.

Wametoa kauli hizo jana wakati wa mazishi ya kitaifa ya Rais wa Awamu ya Tano, Dk Magufuli kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Dk Magufuli alifariki dunia Machi 17, mwaka huu kwa maradhi ya moyo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema Dk John Magufuli kwa miaka aliyoiongoza Tanzania alionesha kuwa Waafrika wana uwezo wa kujitegemea kiuchumi bila watu wa nje.

“Kwa muda mfupi tumeona kazi za barabara, umeme na ujenzi wa viwanja vya ndege na vingine kwa manufaa ya Tanzania na EAC, itakayosaidia kuongeza na kuzidi kufanya kazi pamoja na wananchi wa EAC kuwa kitu kimoja kujisimamia na kuendeleza mambo yako kulingana na haki ambazo Mwenyezi Mungu ametupatia,” alisema Uhuru.

“Muda wa miaka michache aliyokaa madarakani Dk Magufuli ameonesha Waafrika tuna uwezo wa kujitoa kwenye utegemezi, kama Afrika tuna uwezo wa kujitegemea wenyewe na kuzisimamia rasilimali zetu wenyewe,” aliongeza.

“Nikupe neno moja dada yangu Samia, umeshika nchi kipindi kichungu cha majonzi, hata Joshua alipoachwa na Musa alijiuliza nitaweza kweli, lakini Mungu alimwambia usiogope, kuwa na moyo mkuu, nawe usiogope mungu yu pamoja nawe. Dada yangu Samia, kuwa na moyo mkuu usiogope, Mungu yu pamoja nawe kila uendapo, watanzania wapo nyuma yako,” aliongeza Rais Uhuru.

Alisema Rais Magufuli alikuwa rafiki yake hivyo kifo hicho ni pigo kubwa kwake. “...sisi kama Wakenya na mimi binafsi nikasema lile liwalo lazima nije kuungana pamoja kumsindikiza ndugu yetu,” alieleza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Felix Tshisekedi alisema Afrika imempoteza mwanasiasa aliyelenga kutetea na kulinda mali za Afrika na watu wake.

“Ni masikitiko makubwa yaliyojaa uzuni kwa kuondokewa na ndugu na rafiki yangu John Magufuli. Msiba huu ni mzito, hauwagusi Watanzania peke yake, kupotea na kuondoka kwa Dk Magufuli kumetingisha Bara la Afrika,” alisema Rais Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

“Afrika tumepoteza mwanasiasa mkongwe aliyelenga kutetea na kulinda mali za Afrika na watu wake. Tutabaki na kumbukumbu mpiganaji wetu na mzalendo wa kweli, sio tu kwa maslahi mapana ya Watanzania, bali ya Umoja wa Afrika, mtetezi wa uhuru na Bara la Afrika aliyelenga kutimiza ndoto za mshikamano za waasisi wetu wa Bara la Afrika,” aliongeza Rais Tshisekedi.

Rais wa Msumbiji ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Filipe Nyusi, alisema Dk Magufuli ataendelea kuishi kwenye mioyo ya watu. 

Alisema Rais Magufuli alipokuwa Mwenyekiti wa SADC, aliiongoza jumuiya hiyo kwa kujitolea na alikuwa na tamaa ya kuiona SADC ikiwa huru kutoka katika utegemezi wa kiuchumi.

“Magufuli mwanadamu mwenye uwezo imara kama wako hafi kamwe, kwa kaulimbiu yako ya hapa kazi tu, wewe utaendelea kuwa hai kwenye mioyo ya Watanzania, wewe upo nasi, pumzika kwa amani ndugu mpendwa John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Nyusi.

Alisema Dk Magufuli atakumbukwa kama kiongozi thabiti, aliwafikiria Waafrika wote na ana imani kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ataendelea kuwaunganisha Waafrika.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa alisema Rais John Magufuli atakumbukwa kwa mambo matatu ikiwemo kuwa shujaa kupambana na ufisadi na rushwa, kutafuta maendeleo ya wananchi na kutaka mila, desturi na tamaduni vitumike kutatua changamoto. 

“Pia namshukuru kwa juhudi zake za kuelekea ukombozi na mafanikio ya kiuchumi kwa nchi yake, kikanda na bara zima, alikuwa kiongozi aliyetaka masuala ya tamaduni, mila na desturi yatumike kutatua changamoto mbalimbali zilizopo,” alisema Rais Ramaphosa.

Alisema Rais Magufuli hakupenda kusafiri sana na badala yake alipenda kubaki ili Tanzania aendelee kuwatumikia Watanzania.

Kuhusu Afrika, alisema umoja wa familia ya Afrika unaomboleza kwa kuondokewa na kiongozi mahiri aliyekuwa na maono ya kulikomboa Bara la Afrika.

“Tumempoteza mwanamajumui wa Afrika aliyesimama kidete kulitetea Bara la Afrika. Nikikumbuka toka amenialika hapa kwa mwaliko wake rasmi wa kitaifa, wakati nilipohudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za SADC, nakumbuka ukarimu mkubwa aliotupatia pamoja na Mama Janet Magufuli katika harakati za kuimarisha uhusiano wetu Tanzania na Afrika Kusini,” alisema Rais Ramaphosa.

Alisema anakumbuka pia Rais Magufuli alipokwenda Afrika Kusini kushuhudia kuapishwa kwake na walikuwa na majadiliano yaliyomsaidia kupata maono na dira yake kuhusu Tanzania.

“Nilipokuwa hapa pia nilimshukuru Rais Magufuli kwa msaada ambao Tanzania ilitupatia nyakati zile za giza tulipokuwa tukipambana na ubaguzi wa rangi. Nataka kurudia kile nilichomwambia kwa kusema ‘Asanteni, asanteni Tanzania kwa kutusaidia katika mapambano dhidi ya ubaguzi nchini mwetu,” alisema Ramaphosa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/028b43bb18934e2d26a5a1f0769992c5.jpeg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi