loader
Dstv Habarileo  Mobile
Samia: Nimeandaliwa, msihofu

Samia: Nimeandaliwa, msihofu

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Dk John Magufuli amemwandaa vizuri katika kuongoza nchi na hivyo Watanzania wasiwe na wasiwasi hakuna jambo litakaloharibika.

Akizungumza wakati wa Mazishi Rasmi ya Kitaifa ya Rais wa Awamu ya Tano, Dk Magufuli kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini hapa jana, Rais Samia alisema ameandaliwa vizuri kuongoza nchi hivyo ataendeleza pale alipoishia na kuhakikisha anafikisha nchi mahali alipotamani ifikie.

“Mimi nimeandaliwa vizuri nitaendeleza pale aliopoishia na kukamilisha na tutahakikisha tunafanikisha na kufika Tanzania mahali alipotaka Tanzania ifike,” alisema Rais Samia akihutubia taifa kwa mara ya pili kwa wadhifa huo tangu kifo cha Rais Magufuli, Jumatano ya Machi 17, mwaka huu mkoani Dar es Salaam.

Alisema kwa wale wenye mashaka na yeye wajue kwamba aliyesimamia hapo akilihutubia Taifa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, lakini mwenye maumbile ya kike, hivyo yupo imara kuendeleza pale alipoishia Dk Magufuli.

Samia alisema ameandaliwa vizuri na Watanzania wanatakiwa kuondoa wasiwasi na hakuna jambo litakaloharibika, nchi ipo mikopo salama na tutaendeleza alipofika na kufikisha mahali alipotamani kufika.

“Tumepikwa, tumeiva haswa na tumeiva sawa sasa, tupo tayari kuendeleza kazi alizoacha na kufikia pale alipotamani kufika kwa nguvu, kasi na ari ile ile,” aliahidi Rais Samia mbele ya viongozi wa mataifa kadhaa ya Afrika na maelfu ya Watanzania waliojazana kwenye uwanja huo wa michezo kumuaga kipenzi chao.

Samia alisema ni kweli taifa limepoteza kiongozi jasiri, mchapakazi, hodari, imara, mtetezi wa wanyonge, mwanamwema wa Afrika na mwanamageuzi na mtumishi wa wote ambaye alisimamia rasilimali za umma na kutekeleza miradi ya kimkakati akilenga kujenga Tanzania ya viwanda kwa kufungamanisha na ukuaji wa uchumi na kuboresha huduma za jamii kama afya, elimu maji na miundombinu ndiyo maana akabatizwa jina tingatinga au chuma.

Alisema atamkumbuka Dk Magufuli kwa mengi kwani wote wakiwa mawaziri, amekuwa kiongozi, mlezi na amekuwa mchapakazi katika wizara zote alizopitia, akimkumbuka katika Wizara ya Ujenzi ambako alisema alizijua barabara kwa majina, urefu na kiasi cha fedha pamoja na kujua samaki idadi yake alipoongoza Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Samia alisema Dk Magufuli amemwinua kwani kupitia yeye ameimarisha masuala ya usawa na uwiano wa kijinsia na kutokana na hiyo, kumfanya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais na sasa amekuwa Rais.

Msaidizi huyo wa karibu wa Dk Magufuli kwa miaka takriban sita iliyopita, alisema amejifunza mengi ya kufanya kazi kwa juhudina na alichokuwa akiangalia ni kupata matokeo wala si visingizio au lawama.

Aliongeza kuwa Dk Magufuli alikuwa hapendi kwenda nchi za nje, lakini alimpa nafasi hiyo yeye kusafiri katika nchi mbalimbali na yeye akabaki anatumia muda mwingi kusaidia wananchi katika kutatua kero zao za maisha yake.

Alisema alikuwa kipenzi cha watu na atakumbukwa na vizazi kwa vizazi kwani tangu Dar es Salaam watu wamejitokeza kwa maelfu hadi jana Dodoma kuulaki mwili wake na hata kutandika nguo barabarani. Anaamini itakuwa hivyo pia katika kuaga mwili huo leo Zanzibar, kesho Mwanza na nyumbani kwake Chato keshokutwa.

Alisema kutokana na Dk Magufuli kuwa kipenzi cha watu, ndio maana hata Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alisema alifanya kila analoweza iwe iwavyo lazima afike katika kumuaga Dk Magufuli.

Alifafanua kuwa Dk Magufuli alikuwa mnyenyekevu na mcha Mungu, na alikuwa na huruma iliyojificha chini ya taswira ya kula katika matamshi yake.

“Magufuli alikuwa mchapakazi, mtetezi wa wanyonge, mwenye hofu ya Mungu ndio maana hata katika ziara zake siku ya Jumapili alihakikisha kwamba anakwenda kanisani liwe kanisa lake Katoliki au madhehebu mengine,” alieleza.

Alibainisha kuwa mara mwisho kuzungumza naye ni kabla ya kwenda ziara ya mkoani Tanga, alimwambia asiwe na wasiwasi anaendelea vizuri aende kuangalia miradi ili kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM.

“Kwa maneno hayo sikujua kwamba hatapiga simu tena asubuhi, sitasoma mwandiko wake tena, na sitashauriana naye tena,” alisema Samia, mwanamke wa kwanza Tanzania kushika wadhifa wa huo wa juu kabisa katika nchi.

 

Kwa nchi jirani, Rais Samia alisema Tanzania itaendeleza ushirikiano mzuri na wema walionesha marais tisa, makamu wa rais wawili na mawaziri wakuu wawili kufika kumuaga Dk Magufuli.

 

Aliahidi kuendelea kuwa karibu na familia ya Dk Magufuli, mjane Mama Janet Magufuli na watoto wake, na atahakikisha serikali inawasaidia na kuendelea kuwashika mkono.

 

Alisema Dk Magufuli ameondoka mapema lakini amefunga hesabu zake hapa duniani ameacha sadaka ambayo rehemu zake zitamfuata kadiri wananchi wanakavyokuwa wanatumia huduma mbalimbali kama za hospitali kwa ajili ya kujenga afya zao, za maji kuwatua ndoo wanawake vichwani, barabara kupata usafi na elimu kufuta ujinga.

 

Rais Samia alimwaga Dk Magufuli kwa kusema, “Nenda Baba, umepigana vita na mwendo umeumaliza, lala salama kaka, pumzika mwanamwema wa Afrika.”

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi