loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wachambuzi wamsifu Mangula kutoa hofu Watanzania

Wachambuzi wamsifu Mangula kutoa hofu Watanzania

WACHAMBUZI wa siasa wamempongeza Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Magula kwa kutoa hofu Watanzania kwa kuwaeleza kwamba kasi ya maendeleo itakuwa ileile kama alivyokuwepo Rais John Magufuli.

Mangula alisema jijini Dodoma kuwa, Samia na Magufuli walipita kwa wananchi kuinadi Ilani ya uchaguzi ya CCM hivyo hivyo anaamini ahadi zote zitatekelezwa.

Wachambuzi hao walisema jana kuwa, ingawa katika utendaji kuna suala la utashi wa mtu lakini yote kwenye Ilani ya CCM ni mali ya chama husika.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Samson Mwigamba alisema kauli ya Mangula imetolewa wakati mwafaka kwa kuwa inatoa mwelekeo thabiti kuhusu serikali iliyopo hasa ikizingatiwa kuwa aliyefariki dunia ni Mwenyekiti wa CCM taifa.

“Mimi binafsi nimeridhika na nina imani Chama hiki kimejipanga chini ya Rais Samia kwa kuwa ilani iliyopo ni yake na itaendelea kutekelezwa vyema,” alisema Mwigamba.

Alisema kauli ya Mangula imeondoa hofu waliyokuwanayo Watanzania kutokana na kifo cha Rais Magufuli.

“Sasa watu wanajiuliza haya aliyoyaanzisha Rais Magufuli yataendelezwa? Mfano miradi mikubwa ambayo bado iko kwenye utekelezaji kama vile ujenzi wa reli ya kisasa SGR, ujenzi w mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere lakini pia watu wanajiuliza hii elimu bila ada itaendelea?” Alihoji.

Alisema kauli ya Mangula ni sahihi ili kuwaondoa hofu Watanzania pia imewatia moyo kuwa mipango iliyokuwa inatekelezwa na serikali ya Magufuli itaendelea kutekelezwa kwa kuwa ipo kwenye ilani.

Alitoa mfano namna hata katika hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan alivyowaeleza Watanzania kuwa amepikwa na kuiva na Rais Magufuli na kwamba yuko vizuri kuendelea kuwatumikia.

“Ni kweli Rais Samia hawezi kuwa kama Dk Magufuli kutokana na kila mtu kuwa na kaliba yake jambo la msingi atatekeleza ile misingi iliyoanzishwa na Rais Magufuli na mengine mengi zaidi,” alisisitiza.

Mchambuzi wa masuala ya siasa na diplomasia, Abbas Mwalimu alisema Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa wanapozungumzia ilani, hiyo ni mali ya chama na si mali ya mtu binafsi.

Alisema maandalizi ya ilani huhusisha watalaamu wa chama ambao hufanya utafiti na kubaini maeneo yenye shida na kuandaa ilani na kisha kukabidhiwa kwa Rais aliyeshinda kwenye uchaguzi pamoja na makamu wake.

“Ndio maana Mzee Mangula alisema kasi ilele ya Dk Magufuli itaendelezwa kupitia Rais Samia. Kwani ilani kama ilani ni mkata wa chama na wananchi isipotekelezwa ipasavyo wananchi hao wanaweza kutafuta option nyingine,” alisema Mwalimu.

Alimuelezea Samia kuwa ni kiongozi wa kuaminiwa kwa kuwa ni shupavu, mbunifu na asiyeyubishwa kutokana na historia yake ya uongozi nchini.

Alisema hata Magufuli baada ya kupata ridhaa ya CCM kuwania nafasi ya urais, mwaka 2015 alipoambiwa achague mtu atakayemsaidia alimchagua Samia kwa kuwa alimuamini.

Mwanasiasa maarufu nchinin David Kafulila, alisema kauli ya Mangula ni sahihi kutokana na ukweli kwamba kwanza; maisha ya urais ya Magufuli ni shule yenye siri ya namna serikali inaweza kufanikisha ndoto kubwa.

“Historia ya uimara wa mifumo ya dola na Chama ni hakika. Aidha rekodi yake Samia ya uimara wa kusimamia mambo kabla na wakati akiwa Makamu ni hakikisho kwamba atamudu na hana sababu ya kushindwa kuvaa viatu hivyo ikizingatiwa alikuwa Kiongozi namba mbili,” alisema Kafulila.

Juzi katika shughuli ya mazishi ya kimataifa Mangula aliwahakikishia Watanzania kwamba pamoja na Taifa kuondokewa Rais Magufuli mambo yataenda kama yalivyopangwa chini ya Rais Samia.

Alisema Watanzania wanatakiwa kuondoa wasiwasi kwani viongozi hao wawili, Magufuli na Rais Samia walizunguka nchi nzima wakiinadi Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 na ile ya mwaka jana, 2020-2025, hivyo Rais Samia anajua mipango yote ya chama na serikali.

“Mambo yote yataenda kama yalivyokuwa yamepangwa, niwatoe wasiwasi Watanzania mambo yataenda vizuri kwani walikuwa wakizunguka nchi nzima wakipeperusha bendera ya CCM na kunadi ilani ya chama, mambo yataenda vizuri,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe.

Mangulla alisema Samia ana uzoefu wa kutosha kutokana na ukweli kwamba kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, alizunguka nchi nzima pamoja na Dk Magufuli katika nchi nzima akidadi Ilani ya Uchaguzi.

foto
Mwandishi: cHalima Mlacha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi