loader
Dstv Habarileo  Mobile
Magufuli kupitishwa kwa mkewe, darajani ‘kwake’  . Atazikwa katika makaburi ya familia

Magufuli kupitishwa kwa mkewe, darajani ‘kwake’ . Atazikwa katika makaburi ya familia

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mwili wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Magufuli utasafirishwa kwa gari kutoka Mwanza kupelekwa Chato mkoani Geita atakapozikwa keshokutwa.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema jana mjini Zanzibar kuwa kutoka jijini Mwanza mwili wa Dk Magufuli kesho utapitishwa kwenye Daraja la Kigongo- Busisi lenye urefu wa kilometa 3.2 alilolibuni Rais Magufuli.

Majaliwa aliyasema hayo kwenye Uwanja wa Amaan ambako Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aliongoza maelfu ya wananchi na viongozi kuuaga mwili wa Dk Magufuli.

“Lakini mji unaofuata baada ya mto ule au ziwa lile ni nyumbani kwa mama au mke wa marehemu. Kwa hiyo pale mwili utasimama kwa dakika kumi ili wazee maarufu walioko pale waweze kusema neno. Na pale panaitwa mji wa Busisi,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Alisema dakika hizo 10 pia zitatoa fursa kwa ndugu wa mjane wa Dk Magufuli, Mama Janet Magufuli kushuhudia mwili ukipita hapo kwenda Sengerema, Geita mjini, mji wa Katoro kabla ya kuingia katika Jimbo la Chato lililoongozwa na Magufuli kwa zaidi ya miaka 20 na hatimaye utafikishwa mjini Chato.

Tofauti na ilivyokuwa Dodoma, Majaliwa alisema wananchi Zanzibar wangepita lilipowekwa jeneza ili watoe heshima za mwisho.

“Tunaamini kwa idadi hii haiwezi kutuchukua hata masaa mengi, lakini tutakuwa hapa hata kama tutamaliza saa sita usiku ili mradi kila mmoja anamaliza kiu ya kumuaga kiongozi wetu,” alisema.

Aliongeza kwamba kwa kuwa Dk Magufuli alikuwa ni Rais wa Tanzania, jana mwili wake ungelala Ikulu ya Zanzibar na leo asubuhi utapelekwa Mwanza.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema baada wananchi kuaga, mwili wa Rais Magufuli utapitishwa katika Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza kabla ya kupelekwa Chato.

Majaliwa alimpa pole Rais Mwinyi kwa kufiwa na kiongozi huyo waliyeshirikiana kwenye mambo mengi.

“Lakini niendelee kutoa salamu za pole kwa Watanzania wenzangu wote na sisi tuliopo hapa tukiwemo. Jambo hili ni zito, tumeona watu walivyoguswa. Watu wamejipanga kutoka uwanja wa ndege mpaka hapa. Hakuna nafasi hata moja. Tumeona makundi mbalimbali ya watu,” alisema Majaliwa.

Alisema Magufulli ameaga dunia wakati Watanzania bado wanatamani kuwa naye hivyo waendelee kumuombea.

Mongella aliwataka wananchi Mwanza wajiandae kuupokea mwili wa Dk Magufuli leo asubuhi. Alisema baada ya mwili kuwasili utapelekwa katika Uwanja wa CCM Kirumba kwa ajili ya misa, dua, na kutoa heshima za mwisho.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi