loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

MAGUNOMICS: JPM alivyorekebisha ndani kujenga uhusiano bora nje

Tunaendelea kuangalia sera za mageuzi ya kiuchumi zilizotekelezwa na serikali ya awamu ya tano chini ya Hayati Rais John Magufuli miaka michache baada ya kuingia madarakani.

Kwa wale wanaoanza kusoma mfululizo huu, tulisema ‘Magunomics’ ni neno tuliloamua kulitumia linatokana na maneno mawili: Magu (Magufuli) na nomics (economics-uchumi), yaani uchumi uliojengwa na Magufuli.

Tumeshaangalia namna serikali za awamu zilizopita zilifanya mambo mengi mazuri na makubwa lakini kwa bahati mbaya zikaruhusu ‘uholela’ ambao ulisababisha kuwa na rushwa na ufisadi wa kutisha.

Tuliangalia hali ilivyokuwa nchini mwetu ambapo siasa iligeuka kuwa shughuli ya kuukata na kula nchi na watu wengi wakakimbilia kwenye siasa. Halikadhalika rushwa pia ilitamalaki kila sehemu huku wakati mwingine takribani asilimia 20 ya bajeti ya serikali ikipotea kila mwaka kutokana na ufisadi.

Pia tukaona namna umaskini ulivyoota mizizi huku uwajibikaji katika sekta ya umma ukiwa hauridhishi. Jana tulianza kuangalia Utekelezaji wa Magunomics, yaani Sera za Mageuzi za Rais John Magufuli.

Tuliona kwamba serikali ya Awamu ya Tano iliingia madarakani ikiwa na picha ya hali mbaya iliyokuwepo na wakati huo huo ikiwa na nia ya kukuza uchumi wa viwanda ili hatimaye nchi iweze kuboresha maisha ya wananchi, kujitegemea na kutetea maslahi yake.

Ili kutimiza malengo hayo, serikali iliweka mikakati ya aina nne: kwanza, kujenga mahusiano na mataifa ya nje yenye manufaa; pili, kupambana na rushwa na ufisadi; tatu, kutekeleza sera za kibajeti za kuongeza mapato, kudhibiti matumizi yasiyo na tija na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na mwisho, kutekeleza sera za kifedha za kuongeza fedha kwenye mzunguko.

Leo tunaendelea kuangalia namna viongozi thabiti wa awamu ya tano walivyoweza kufanya mambo kadhaa muhimu yafuatayo: Uhusiano na mataifa ya nje Japokuwa kwa miaka mingi tumekuwa na uhusiano mzuri na mataifa mengi ya nje, hatukufanikiwa sana katika kujenga uhusiano na mataifa ya nje wenye tija au manufaa kwa taifa.

Kwanza, ni ukweli ulio wazi kwamba nchi haiwezi kuwa na uhusiano wenye tija/manufaa kama hali ya ndani ya nchi sio ya kuridhisha. Kwa sababu hiyo, serikali ya Awamu ya Tano iliamua kujishughulisha zaidi na mambo ya ndani - kusafisha nyumba.

Maana yake ni kwamba hali ya ndani ndiyo inaamua aina ya uhusiano na kama uhusiano huo utakuwa na tija au hapana. Kwa mfano, kama ndani ni kuchafu, uhusiano utakuwa mchafu - rejea mikataba mibovu.

Mtazamo huu unakubaliana na ule wa wanazuoni wengi wanaoamini kwamba matatizo mengi ya Tanzania yanatokana na masuala ya ndani badala ya yale ya nje.

Pili, ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na ulinganifu kati ya manufaa yatakayopatikana kutokana na safari za nje na pesa zitakazotumika (value for money), serikali ya Awamu ya Tano iliratibu safari zote za nje.

Hii ilimaanisha kwamba maofisa wa serikali walitakiwa kuomba kibali cha kusafiri nje. Ili muombaji apate kibali ilimlazimu aeleze madhumuni ya safari, kiasi cha fedha kitakachotumika, anayegharamia safari hiyo na manufaa kwa nchi yatakayopatikana kutokana na safari hiyo.

Hatua hii iliwafanya waombaji wawe makini kwa kuwa suala lilikuwa sio tu kwenda kula bata bali manufaa yatakayotokana na safari hiyo. Tatu, mabalozi walikumbushwa wajibu wao kwamba hawakutumwa kwenda nje kunywa mvinyo kama alivyosema Rais Magufuli bali kuhakikisha nchi inanufaika na uwepo wao huko.

Maana yake ni kwamba mabalozi walitakiwa wawe watu wa matokeo (results oriented) - yaani, kila baada ya muda fulani waweze kueleza wameleta wawekezaji wangapi, wamepanuaje masoko kwa bidhaa zinazozalishwa Tanzania, wameleta watalii wangapi, wamesaidiaje kupata misaada na teknolojia ya kisasa.

Pia, mabalozi walitakiwa kuiwakilisha nchi kwa kuhudhuria mikutano itakayofanyika kwenye nchi walizopo au nchi jirani.

Nne, serikali ya Awamu ya Tano ilifungua ofisi za ubalozi kwenye nchi za Israel, Cuba, Uturuki, Sudan Kusini, Algeria, Qatar na Korea Kusini. Hizi ni nchi za kimkakati ambazo Tanzania imekuwa ikinufaika na inaweza kunufaika zaidi (kwa biashara, uwekezaji, misaada, teknolojia, ulinzi na usalama na watalii) kwa kuwepo kwa ofisi za kibalozi katika nchi hizo.

Tano, Serikali ilifanya mabadiliko makubwa kwenye sheria zinazohusiana na uvunaji wa rasilimali zetu ili ziwe na manufaa kwa taifa. Mazungumzo yalifanyika na kukubaliwa kuongeza asilimia ya mgawo na faida itakayopatikana kwenye uchimbaji na mauzo ya madini.

Pia, serikali ilikataa kuingia kwenye makubaliano/mikataba ya kibiashara (kama EPA) ya kinyonyaji na ambayo haina manufaa kwa taifa.

Tanzania pamoja na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki zilikusudia kuzuia biashara ya mitumba kwa sababu inaonekana kukwamisha dhamira ya nchi hizo kuanzisha uchumu wa viwanda.

Mwisho, serikali iliweka wazi kwamba haitapokea misaada yenye masharti na badala yake ikajizatiti kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani. Ujumbe ambao serikali ya Magufuli ilituma dunia nzima ni kwamba kwenye meza ya chakula (mgawanyo wa utajiri duniani) Watanzania tunataka kuwa walaji wa chakula badala ya kuwa wahudumu au chakula cha kuliwa.

Mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi Kama ilivyooneshwa kwenye andiko hili hapo awali, rushwa na ufisadi ni adui namba moja wa maendeleo, hivyo, nguvu za ziada zilihitajika kukabiliana nao.

Akiunga mkono hoja hiyo, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alisema, “Ninafikiri ni lazima ufisadi ushughulikiwe kwa ukali bila huruma kwa sababu ninaamini ufisadi ni adui wa usalama wa nchi wakati wa amani zaidi ya vita”.

Japokuwa serikali za awamu zote zimekuwa zikipambana na rushwa na ufisadi, ni serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ndiyo ilionesha kuchukua hatua kali zaidi na waziwazi kukabiliana na janga hilo.

Ili kukabiliana na rushwa na ufisadi, serikali ya awamu ya tano ilianzisha mahakama maalumu zitakazowashughulikia wala rushwa na mafisadi na wahujumu uchumi.

Tayari viongozi na wafanyakazi wa awamu zilizopita na wa awamu hii wameshafikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya rushwa na ufisadi. Japokuwa awamu zilizopita pia zilipambana na rushwa na ufisadi, lakini serikali ya awamu ya tano chini ya JPM ilionesha nguvu ya pekee hasa nguvu ya kutoka ikulu na dhamira ya dhati kupambana nao.

Matokeo yake, mabilioni ya fedha yaliokolewa na kuelekezwa kwenye matumizi ya muhimu. Japokuwa ni mapema sana kujisifia kuhusu suala hili, jambo la msingi ni kwamba kila kulipoibuka harufu ya rushwa na ufisadi ulishughulikiwa kwa guvu zote.

Tunajua wazi kwamba rushwa na ufisadi mkubwa ndio vinasinyaza bajeti kwa kiasi kikubwa na ndiyo inayochepusha fedha ambazo zingetumika kwenye maendeleo ya wananchi kuzielekeza kwenye matumizi binafsi.

Pia, rushwa na ufisadi ndivyo vinapoteza imani ya wananchi kwa serikali yao, ndivyo vinaathiri uhusiano wa kiuchumi wa serikali na mashirika ya kimataifa, ndiyo unaathiri biashara na uwekezaji... Madhara yake ni mengi na makubwa.

Kwa hiyo, wakati tukianza uongozi wa Rais wa Sita wa nchi yetu Mama Samia Suluhu Hassan inatupasa kila Mtanzania kuunga mkono mapambano dhidi ya rushwa.

Kesho tutaendelea kuangalia hatua zilizochukuliwa na viongozi thabiti wa awamu ya tano katika kuimarisha uchumi wa Tanzania. Profesa Kitojo Kagome Wetengere ni mchumi na mshauri binafsi wa masuala ya uchumi, hususani katika eneo la Diplomasia ya Uchumi.

WATU hutegemea mvua ili kufanikisha shughuli mbalimbali, ikiwamo ...

foto
Mwandishi: Profesa Kitojo Wetenge

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi