loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Natamani JPM uamke, uone Watanzania wanavyohamanika

S AA tano usiku wa Machi 17, 2021. Mama Samia Sulu Hassan alitutangazia Watanzania kuhusu kifo cha mpendwa wetu, Dk Joh Magufuli, baada ya kuwepo na maneno maneno kuhusu hali yake.

Ilikuwa ni taarifa ngumu kuipokea, ukweli uliouma sana na kuleta maumivu! Siku hiyo nililala mapema lakini niliposhtuka usingizini, nikapokea ujumbe wa simu kutoka kwenye chanzo cha uhakika ukinitaarifu juu ya tangazo hilo la la Mama Samia la kusikitisha sana na kutisha.

Kwa jinsi nilivyoshtuka, ikanibidi nizime simu kwanza. Nikatafakari, nikawaza na kuazuwa kwa sauti juu ya tukio hilo. Nililala baada ya muda mwingi kupita huku akili yangu ikigoma kuamini kama ni kweli jembe limeondoka.

Asubuhi nilipofuatilia kwenye vyombo vya habari ndipo nikaanza kuamini kwamba baba ameenda angalau kwa mbali. Niliposhuhudia kuapishwa kwa Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mama yetu mpendwa, Samia Suluhu Hassan Machi 19, 2021, kisha ratiba ya kuomboleza na kuaga mwili hadi mazishi, ikitolewa, nikaamini kwa asilimia 100 kwamba Tanzania tumeshaumbuka.

Jembe limekwenda. Umeenda jembe! Umeenda chuma! Umeenda jiwe! Umeenda mpambanaji! Umeenda mzalendo wa Afrika! Umeenda shujaa wa Afrika! Umeenda mwanaharakati namba moja wa Afrika na mtetezi wa Waafrika! Ulijitoa maisha yako, kutetea maskini na wanyonge – wasakatonge.

Umejitoa kiasi kwamba hadi unakufa ulikuwa unawapambania wanyonge, umewahakikishia ajira machinga, umesikia kilio chao na kuwaenzi! Baba, ulikataa nchi kuendelea kuwa shamba la bibi. Uliuchukia umaskini wa Watanzania na ukapambana nao kwa dhati.

Kila mara ulituomba tukuombee. Labda hatukujua vizuri vita halisi uliyokuwa unapambana nayo. Najiuliza, kweli tulikuombea au tulijisahau! Kumbe, ndio ulikuwa unatuaga siku ile uliposema tutakukumbuka kwa mazuri? Shughuli za kuaga mwili ilipoanza; nilishuhudia misururu ya watu njiani na uwanjani.

Watu wakiwa wamejaa pomoni. Wengi wakitokwa machozi, na vilio huku na huko. Nikaendelea kufikiri, kutafakari na kuwaza kwa sauti juu ya mambo makubwa ambayo umeifanyia nchi yetu, ndani ya muda mfupi tu: takribani miaka mitano na miezi minne pekee ya utawala wako.

Haya ni mambo ambayo mzee wetu, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi aliwahi kukiri hadharani kwamba, umefanya mambo ambayo wao, yaani marais waliopita hawakuweza kufanya.

Mwinyi alimaanisha mengi ikiwa na ukweli kwamba unapozungumzia makao makuu ya nchi kuhamia Dodoma kutoka Dar es Salaam ulibaki kuwa mfupa mgumu uliowashinda wengi, wewe umeuweza.

Unapozungumzia mradi mkubwa wa kufua umeme wa maji wa Mwalimu Nyerere utakaozalisha takribani megawati 2115 unazungumzi mtu mwenye maamuzi magumu hasa ikizingatiwa kwamba huu ni mradi ambao mabeberu na vibaraka wao wa ndani waliupinga sana.

Unapozungumzia usafiri wa anga tayari kuna ndege 11 zimenunuliwa, ambapo ndege tisa tayari zipo nchini na zinafanya kazi. Huku kukiwa na matarajio ya kuongeza ndege zingine takribani nne hivyo kuwa na idadi ya ndege 15 za abiria.

Kwamba ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme, ambayo ilikuwa ni kama ndoto kuwa nayo unaendelea kama kawaida kutokana na juhudi zako. Ujenzi wa reli hiyo kati ya Dar es Salaam na Morogoro ujenzi wake umefikia asilimia 98.

Ujenzi kutoka Morogoro kwenda Dodoma umeanza na huku ujenzi wa reli hiyo kuanzia Mwanza mpaka Isaka, Shinyanya mkataba umeshafungwa.

Matarajio ikiwa ni kuunganisha reli hiyo kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza, kisha kwenda Kigoma na kuunganisha nchi za Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na nyinginezo kadri itakavyohitajika.

Huu ni usafiri utakaorahisisha na kuharakisha shughuli za kiuchumi na kijamii. Yaani, utarahisisha usafirishaji wa mizigo mingi na au abiria kwa wakati mmoja haraka.

Inasemwa kwamba itachukua saa nane mpaka tisa pekee kutoka Mwanza mpaka Dar es Salaam, hivyo, kuharakisha shughuli. Huu huwezi kulinganisha na treni ya kawaida inayotumia takribani siku tatu kutoka Mwanza mpaka Dar es Salaam huku mabasi yakitumia siku moja na nusu katika safari hiyo hiyo.

Nikawa natafakari juu ya udhibiti wa wizi na utorojashaji wa rasilimali za Taifa (mfano, madini, wanyama, na miti) kwenda nje ya nchi uliokuwa nafanywa na wenyeji kwa kushirikiana na wageni. Tukio la mwaka 2016 la makanikia, likanijia kichwani.

Nikaanza kukumbuka juu ya mchakato mzima ulivyokwenda huku akina Tundu Lissu na Zitto Kabwe wakitutisha kwamba nchi itashitakiwa, itakimbiwa na wawekezaji na mengine mengi lakini mwisho, Magufuli akashinda.

Na sasa, japo tuna hisa asilimia 16 kwenye kampuni tanzu kati ya Serikali na Barick ya Twiga, kampuni iliyoundwa kutokana na makubaliano mapya ya uchimbaji madini.

Sasa tunagawana faida ya asilimia 50 kwa 50. Makubalino hayo yameweka msingi mzuri, hata kwa makampuni mengine yanayokuja kuchimba madini nchini, kufuata mkondo huo.

Mfano, uchimbaji wa madini ya ‘nickel’ pale Kabanga; makubaliano yamekuwa hivyo hivyo, kwamba kugawana asilimia 50 kwa 50 kati ya Serikali na wawekezaji chini ya kampuni tanzu iliyopewa jina la Tembo.

Nikawa ninakumbuka utiwaji saini wa usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda kwenda Chongoleani pale Tanga ili kupelekwa nje ya Afrika kwa hatua zaidi.

Huu ni mradi ambao sisi tutanufaika kwa kupata asilimia 60 ya mauzo ya mafuta hayo, huku Uganda ikibaki na asilimia 40 ya faida ya mauzo ya mafuta hayo.

Ni wewe baba Magufuli ndiye uliyefanikisha mradi huo, upitie kwetu Tanzania badala ya kupitia nchini Kenya kwenye bandari ya Mombasa. Sikusahau kwamba uamuzi wako wa kujenga ukuta wa kuzunguka migodi ya madini ya Tanzanite, pale Mererani mkoani Manyara umekuwa wa faida kubwa.

Sasa mauzo na mapato yatokanayo na madini hayo na mengineyo yameongezeka. Sasa India sio nchi ya Kwanza duniani kwa mauzo ya Tanzanite, wala Kenya sio nchi ya pili.

Ilikuwa ni kichekesho kuona Tanzania I ya kwanza kuuza madini hayo wakati yakipatikana Tanzania pekee. Kwamba kufunguliwa kwa masoko ya madini karibu kila mkoa, ni hatua chanya kwa maslahi ya Taifa.

Nikawa naendelea kutafakari na kuwaza kwa sauti; jinsi ulivyokusanya kodi na kubana matumizi Serikalini. Tumeshuhudia makusanyo yakiongezeka kutoka takribani bilioni 800 kwa mwezi mnamo mwaka 2015 ulipoingia madarakani, na kufikia takribani trilioni 1.5 kwa mwezi unapoondoka duniani.

Mapato ambayo ndio yamekuwa yakitumika kujenga miundombinu mbalimbali: barabara za juu na chini, vivuko vya maji, meli mbalimbali, chelezo, bandari, viwanja vya ndege, madaraja ya nchi kavu na majini, na kadhalika.

Mapatao hayo yamekuwa yakitumika kugharimia huduma za afya, elimu bila malipo kuanzia shule za awali, msingi, na sekondari ya chini (kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne).

Kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu: vyuo na vyuo vikuu. Pia, kwenye makundi maalumu: vijana, wanawake, na walemavu. Bila kusahu kulipa mishahara kwa wakati kwa watumishi wa Serikali, na mambo kadha wa kadha.

Nikakumbuka juu ya vita ya rushwa na ufisadi; bila kusahau dawa za kulevya. Nikawa nawaza kuwa vita hii ilikuwa haijafika mahali pake, japo kwakweli ulijitahidi kupigana. Tulipofikia, ni hatua ya kujivunia.

Maana mengine ulisema tusifukuwe makaburi. Tulikuelewa. Juu ya changamoto ya kupumua ambayo imeitikisa dunia. Nilipenda sana msimamo wako na jinsi ulivyosimamia suala hilo.

Kwa kutusisitiza kuchukuwa tahadhari zote zinazotolewa na wataalamu wa afya. Ukatusisitiza juu ya kuomba na kumtegemea Mungu, na ukatushauri tutumie tiba zetu za asili, mfano kujifukiza (kupiga nyungu) na nyinginezo.

Haukuruhusu tujifungie ndani, kama wengine walivyofanya, isipokuwa nchi chache kama Sweden. Umetahadharisha juu ya kutumia chanjo zinazoletwa kutoka nje, kwamba ni lazima tujiridhishe juu ya ufanisi wake kabla hatujazitumia.

Ukweli ni kwamba, matokeo hasi ya chanjo hizo yameanza kujitokeza, karibu kila mahali walipoanza kuzitumia. Nikawa nawaza kwa sauti namna ulivyoanza kutubadilisha kimtizamo kuwa kuwa sisi, Tanzania; sisi Afrika ni matajiri wala sio masikini.

Maana tunazo rasilimali za kutosha hata kuliko hao tunaoita matajiri. Kwamba tatizo lipo kwenye usimamizi wa rasilimali hizo kwa masilahi ya Taifa na Afrika kwa ujumla na si vinginevyo.

Ukawa unatuasa kuwa wazalendo kivitendo, kwa kuhakikisha tunasimamia vyema rasilimali zetu. Kwamba tusiruhusu wageni kuendelea kutupora na kutunyonya rasilimali tulizonazo tele.

Mbona umeondoka mapema, kabla ya muda wako? Miradi mingi umeacha hata haijakamilika! Au umeamua kususa kwa chokochoko za wajomba? Natamani uamke ujionee mwenyewe Tanzania inavyolia – wanyonge uliotetea wanavyohamanika.

Natanamani uamke ujionee mwenyewe marafiki wa ukweli na adui zako wa kweli. Natamani uamke umalizie muda wako! Natamani uamke japo useme kwa heri! Kila la heri baba yetu, kipenzi chetu.

Imempendeza Mungu akichukue, lakini bila shaka huyu uliyetuachia Mama yetu, Samia Sukuhu Hassan atakamilisha vyema ndoto zako kama wewe ulivyotekeleza ndoto za Mwalimu Nyerere.

Kama kulikuwa na upungufu kwa upande wako, yeye atajazia bila shaka. Kwaheri baba yetu. Mwendo umeumaliza. Mwandishi wa makala haya ni mcangiaji wa gazeti hili.

 

Mawasiliano yake ni+255 762

ZANZIBAR, katika visiwa vyake viwili vya ...

foto
Mwandishi: Gorwe Machage

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi