loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Magufuli na msingi imara wanawake katika uongozi

RAIS wa kwanza wa Tanzania aliyemaliza muda wake mwaka 1985, Julius Kambarage Nyerere, alikuwa mwanaume. Akafuatiwa na Ali Hassan Mwinyi (1985- 1995).

Aliyemfuatia katika Awamu ya Tatu, naye alikuwa mwanaume; Benjamin Mkapa (Hayati) mwaka (1995-2005). Hata Awamu ya Nne, iliongozwa na mwanaume, Jakaya Kikwete (2005 -2015).

Katika awamu hii, mabadiliko ya kifikra mintarafu mwanamke katika siasa na uongozi yalianza kuonekana nchini Tanzania. Kwa mara ya kwanza mwaka 2010, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, likaongozwa na mwanamke; Spika Anne Makinda.

Ikumbukwe kuwa wakati wote huo nchini, hakuna mwanamke yeyote aliyekuwa amewahi kushika wadhifa wa waziri mkuu, makamu wa rais, jaji mkuu, spika wa bunge wala kuwa rais wa nchi.

Mfumo dume uliokuwa umetamalaki ukasikia na kutii amri ya ‘Nyuma geuka!” kutoka kwa aliyekuwa Mgombea Urais wa Chama Cha Mapindunzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, John Magufuli (alichaguliwa na kuwa Rais wa Tanzania).

Magufuli akamteua mwanamke; Samia Suluhu Hassan, kuwa mgombea mwenza na baada ya ushindi kupitia sanduku la kura, akawa mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais nchini Tanzania.

Kazi na umakini wa Samia Suluhu ambaye sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama tunda la Katiba ya Tanzania baada ya Rais wa Awamu ya Tano, Magufuli, kufariki dunia Machi 17, 2021, ilianza kuonekana wazi katika mikutano ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 namna alivyozunguka bila kuchoka na namna alivyojenga hoja nzito na makini katika majukwaa.

Kimsingi, uwezo wa Rais Samia umethibitisha kuwa, wanawake wanaweza isipokuwa, kulikuwa na misingi ya mila kandamizi dhidi ya wanawake zilizojengwa katika jamii na bado hazijaisha.

Haya yote ni matunda ya msingi na nguzo imara alizozijenga Magufuli kuhusu nafasi, umuhimu na uwezo mkubwa walio nao wanawake katika siasa na uongozi. Katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, yupo mwanamke mwingine aliyeonesha uwezo na uthubutu kwa kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira.

Kutokana na misingi hiyo imara aliyoijenga Magufuli na kutaka iendelee kwa kuwapa nafasi wanawake, Rais huyo ambaye Tanzania na mataifa mengine wanaomboleza kifo chake akitarajiwa kuzikwa keshokutwa Ijumaa Machi 26, 2021 Chato mkoani Geita, akamteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Kupitia uwezo wa mwanamke huyo katika uongozi, Mghwira amethibitisha kuwa ‘Wanawake Wanaweza’ katika siasa na uongozi maana wapo wengine wanaozidi kuthibitisha hilo wakiwamo akina Dk Rehema Nchimbi (Mkoa wa Singida), Zainab Telack (Mkoa wa Shinyanga) na Christina Mndeme (Mkoa wa Ruvuma).

Hata katikia Uchaguzi Mkuu wa Mwaka Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akila kiapo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Machi 19, 2021 Ikulu Dar es Salaam.

Magufuli na msingi imara wanawake katika uongozi 2020, vyama viwili pia vilitoa wanawake kuwa wagombea urais. Ingawa kura zao hazikutosha, wanawake hao Queen Sendiga (Naibu Katibu Mkuu wa ADC) na Secilia Mmanga (Demokrasia Makini), walionesha njia na mfano bora kuwa, wanawake wanaweza.

Kutokana na uwezo wa wanawake katika uongozi, Februari 12, 2017 wakati akimuapisha Dk Anna Makakala kuwa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Ikulu Dar es Salaam, Rais Magufuli ‘alianika bayana’ sababu ya kuteua mwanamke katika nafasi hiyo kuwa ni bidii, uaminifu na uadilifu mkubwa walio nao wanawake wengi hata katika masuala ya fedha.

Katika moja ya hotuba zake baada ya kuwa Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM kitaifa, Magufuli aliwahi kukiri uwezo mkubwa wa wanawake katika uongozi aliposema, “Muelewe ndugu zangu, ukishindana na mwanamke, ujue utashindwa tu na wakinamama siku zote wanatushinda sisi wanaume na wanatushinda kwa mambo mengi...” Msingi huo alioujenga Magufuli, umezifanya taasisi mbalimbali zikiwamo zisizo za kiserikali kuingiwa matumaini zaidi ya Tanzania kuelekea kuwa miongoni mwa nchi vinara wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia hata katika masuala ya siasa na uongozi.

Juhudi hizo na matunda ya ulinzi na heshima kwa Katiba ya Tanzania, ndizo zimewezesha kwa mara ya Kwanza, Tanzania kumpata rais ambaye ni mwanamke kama ilivyoongoza Katiba.

Kifungu cha 37 (5) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 kinasema, endapo rais wa nchi atarafiki dunia, makamu wa rais ataapishwa kushika wadhifa huo kwa muda uliobaki kabla ya uchaguzi.

Sasa ni Samia Suluhu Hassan aliyevaa viatu’ vya JPM aliyemaliza safari yake duniani akiwa Rais wa Kwanza Tanzania, kufariki dunia akiwa madarakani. Watanzania wana imani kubwa na nafasi ya mwanamke katika Uongozi; wana imani kubwa kwa uongozi mpya wa Rais Samia Suluhu kwani amekuwa msaidizi na “mwanafunzi” wa JPM.

Spika Mstaafu Makinda akiwa katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam kuaga mwili wa Hayati Magufuli alinukuliwa akisema kuwa, kilichobaki kwa Watanzania ni kumpa ushirikiano wa dhati Rais Samia ili afanye kazi ipasavyo na kwamba, hakuna mantiki kuanza kujadili masuala ya jinsia.

“Hakuna sababu ya kusema rais ni mwanamke maana mbona hatukusema makamu wa rais mwananmke na ameweza na kila mtu akaona ameweza…” alisema Makinda siku ya kwanza ya kuaga mwili mkoani Dar es Salaam.

Kuthibitisha kwamba Rais Samia yupo vizuri kiuongozi na wanawake wanaweza, muda mfupi baada ya kiapo chake, aliwaambia Watanzania: “Tuko imara kama taifa… nimeapa kulinda na kuisimamia Katiba, hakuna jambo litakaloharibika.”

Juzi wakati akihutubia taifa katika mazishi ya kitaifa ya magufuli jijini Dodoma alisema: “… Mimi ndiye rais;… hakuna kilichoharibika.” Katika kipindi cha kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofikia kilele chake Machi 8, 2021, akiwa bado ni Makamu wa Rais, Samia alisema: “Huko tunakokwenda kwa kuondoa mifumo kandamizi, inawezekana Tanzania kuwa na rais mwanamke… Kama imewezekana kuwa na makamu wa rais mwanamke, hata rais inawezekana kwa kuwa mifumo kandamizi inazidi kuondolewa.”

Baada ya Samia kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben, ameonesha imani kubwa akisema: “Tunampongeza Rais huyu wa Sita wa Tanzania, tukiamini kuwa ni kiongozi anayestahili, makini na anayekwenda kusimamia maadili, kusimamia katiba na kuzisimamia haki za wanawake na watoto.”

Rose akaongeza: “Tamwa inaamini ‘Wanawake Wanaweza’ na si kwa kuwezeshwa pekee, bali waliaminika tangu enzi kwa kupewa madaraka ya kuwa wasimamizi wakuu wa familia, kuanzia hatua ya malezi, jambo linalowafanya kuwa imara, wanyenyekevu, wavumilivu na makini zaidi hata katika nafasi za kisiasa na uongozi katika maeneo mengine.”

“Jambo hili litaacha alama kwa vizazi vijavyo na kisha kuulinda na kuuheshimisha mfumo wa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi kwa kuwa ‘wanawake wanaweza,” alisema.

Hali hii imewatia moyo Watanzania wengi na taasisi za ndani na nje ya nchi kuunga mkono juhudi hizo za kuchochea usawa wa kijinsia katika masuala ya siasa na uongozi ili kuwapa wanawake fursa ya kushiriki kikamilifu.

Mfano bora ni shirika la kimataifa la UNWomen (Tanzania) linalofadhili mradi wa Wanawake Wanaweza kupitia Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) na taasisi nyingine washirika.

Katika mradi wa Wanawake Wanaweza, Tamwa kimeendesha mafunzo mbalimbali kwa waandishi wa habari nchini kuhusu kubaini changamoto zinazowakumba wanawake katika harakati za kushiriki siasa na uongozi hata katika vyama vya siasa sambamba na kubainisha mambo yanayopaswa kufanyika ili kukabili changamoto hizo.

Kupitia mradi huo unaozilishirikisha taasisi nyingine kama Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) na African Women Leaders Network (AWLN), wanahabari wanahimizwa kuwaibua wanawake katika ngazi mbalimbali kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Kadhalika, Wanawake Wanaweza ni mradi unaolenga kuhamasisha jamii kubadili mtazamo kuhusu uwezo na ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi na kuwafanya wajitokeze kuwania nafasi za uongozi ama wa kuchaguliwa, au kuteuliwa katika kada mbalimbali kadiri ya sifa na uwezo

WATU hutegemea mvua ili kufanikisha shughuli mbalimbali, ikiwamo ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi