loader
Dstv Habarileo  Mobile
Samia anaweza, Tanzania Samia anaweza, Tanzania haitarudi nyuma’

Samia anaweza, Tanzania Samia anaweza, Tanzania haitarudi nyuma’

WACHAMBUZI wa siasa na uchumi wamesema hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Mazishi ya Kitaifa ya Rais John Magufuli imewahakikishia Watanzania kasi ya maendeleo haitapungua kwa kuwa anafahamu siri ya mafanikio ya uongozi wa mtangulizi wake.

Rais Magufuli aliiongoza Tanzania kwa miaka mitano na miezi mitano tangu Novemba 5, 2015 hadi Machi 17, mwaka huu alipofariki dunia Dar es Salaam kwa tatizo la mfumo wa umeme wa moyo.

Profesa wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Humphrey Moshi, alisema kauli ya Rais Samia kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kwamba ameandaliwa, ameiva na sasa yeye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imebeba ujumbe kwa Watanzania kwamba nchi haitarudi nyuma kimaendeleo na kimsimamo.

Profesa Moshi alisema Watanzania wasiwe na hofu kuwa baada ya Dk Magufuli kufariki dunia, nchi itarudi nyuma bali watambue Rais Samia amekuwa naye kwa miaka mitano hivyo si tu alikuwa mwanafunzi, bali alikuwa mfuasi wake.

“Wakati Rais Magufuli anaishi, wananchi wamejua kama kiongozi anaweza kufanya mambo gani na wanajua kiongozi wao ni yupi, ndiyo maana Rais Samia aliwahakikishia kwamba hatatetereka katika kuendeleza mambo ambayo Magufuli aliyafanya,” alisema Profesa Moshi.

Aliongeza, “Yeye (Samia) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ni kikosi kilichoteuliwa na Magufuli na aliwateua aliwateua akijua watafanya kazi vizuri, kwa hiyo Samia alikuwa anawahakikishia Watanzania wasiwe na mashaka, na mimi naamini anaweza.”

Aliyewahi kuwa Mbunge wa Kigoma Kusini na Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, David Kafulila, alisema juzi Rais Samia aliwahakikishia Watanzania kwamba anafahamu siri ya mambo makubwa yaliyofanikishwa na Serikali ya Rais Magufuli, lakini pia anajua mtangulizi wake alikuwa akifanya nini kufanikisha mambo hayo.

“Rais Samia anajua nini walikuwa wanapanga na Magufuli na kufanikisha, anajua siri za kufanikisha na kutokufanikisha mambo mbalimbali katika uendeshaji wa serikali, kwa hiyo anatosha kuvaa viatu vya Rais Magufuli,” alisema Kafulila. Alisema kwa kuwa Rais Samia alifanya kazi na Magufuli tangu mwaka 2015 na alikuwa mtu wa pili kimamlaka baada ya Rais, anafahamu ukubwa wa jukumu la kuendesha serikali.

Kafulila alisema hoja ya kwamba Samia ni Rais mwanamke haina mashiko kwa sababu nchi kadhaa ikiwemo Ujerumani inayoongoza kwa uchumi wa Ulaya inaongozwa na Kansela Angela Merkel.

Alisema pia Shirika la Fedha Duniani (IMF) liliwahi kuongozwa na mwanamke Christine Lagarde, Margaret Thatcher na Theresa May waliiongoza Uingereza kwa nafasi ya Waziri Mkuu na kwa nchini, Anne Makinda alikuwa Spika wa Bunge la Tanzania, na sasa Naibu Spika wa Bunge hilo ni Dk Tulia Ackson.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda alisema hotuba ya Rais Samia ilidhihirisha ana uwezo wa kuiongoza nchi.

Dk Mbunda alisema japo Rais Samia ameingia kuvaa viatu vya Dk Magufuli aliyefanya kazi kubwa ikiwemo ya kurudisha nidhamu katika utumishi wa umma, mapambano dhidi ya rushwa, kujenga miradi ya kimkakati, kusimamia rasilimali za nchi na kuacha alama kubwa, anaamini atakonga nyoyo za Watanzania kwa sababu ana uwezo wa kutosha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Demokrasia na Utawala Bora Afrika (ForDIA), Bubelwa Kaiza alisema Rais Samia juzi alilenga kuimarisha watu waamini kwamba baada ya Rais Magufuli kufariki dunia, atakuwa na mwelekeo uleule.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimba Madini Tanzania (FEMATA), John Bina alisema anaamni Rais Samia atayaendeleza mambo mazuri aliyoyaanzisha Rais Magufuli. Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam, Godwin Amani alisema urais ni mamlaka hivyo Rais Samia aliwakumbusha Watanzania kuwa kwa sasa yeye ndiye Rais na ana mamlaka kamili, hivyo watulie na wasiwe na hofu

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi