loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wachache kumzika Magufuli makaburi ya familia

Wachache kumzika Magufuli makaburi ya familia

MKUU wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel amesema watu wachache watahudhuria maziko ya Dk John Magufuli hivyo wananchi wilayani Chato wabaki nyumbani siku hiyo Machi 26, mwaka huu.

Gabriel jana aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kabla ya maziko kutakuwa na misa ya kumuombea marehemu katika Uwanja wa Michezo wa Magufuli.

Alisema uongozi wa mkoa unatambua wananchi wanatamani kushiriki ibada na maziko ya Dk Magufuli, lakini eneo la uwanja ni dogo na kwamba Ijumaa si siku ya kuaga ila maziko.

“Kwa hali halisi ilivyo, eneo la ibada hiyo, ni la kupokea watu wachache, kwa hiyo niwaombe wana Geita, popote pale walipo wakae majumbani mwao wasikilize matukio yote yanayoendelea kupitia luninga, uwanja wetu utawapokea viongozi wa dini, viongozi wa kitaifa, na wana Chato na wana Geita wachache sana watawakilisha,” alisema Gabriel.

Alitoa mwito kwa watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo wazee, watoto na wagonjwa wabaki nyumbani na waepuke misongamano leo jioni wakati mwili utakapowasili ukitoka jijini Mwanza.

“Chato hapatoshi, ni padogo mno kuliko pote walipopita, kunapokuwa kuna tukio kubwa kama hili na mtu akawa na changamoto za kiafya, kwa foleni kubwa itakayokuwepo inawezekana tukashindwa kutoa huduma stahiki kwa kila mmoja kwa wenye changamoto, hivyo niwasihi tuchukue tahadhari,” alisema mkuu wa mkoa.

Aliwasihi wakazi wa Geita watambue kesho imetengwa kwa wananchi kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi huyo hivyo ni vyema wazingatie utaratibu utakaotolewa wakiwa watulivu.

foto
Mwandishi: Yohana Shida, Chato

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi