loader
Dstv Habarileo  Mobile
Watanzania watenda  haki kumuaga JPM

Watanzania watenda haki kumuaga JPM

MAELFU ya wakazi wa Jiji la Mwanza na mikoa ya jirani wamejitokeza kuuaga mwili wa Dk John Magufuli katika Uwanja wa CCM Kirumba na mitaa ya jiji hilo wakati ulipokuwa ukipita kwa safari yake ya mwisho kabla ya kesho kupumzishwa katika nyumba yake ya milele kwao Chato mkoani Geita.

Wakazi wa Mwanza wakiongozwa na mkuu wao wa mkoa, John Mongella, waliupokea mwili wa Rais Magufuli saa 1.30 asubuhi ukitokea Zanzibar ambako jana wananchi wa visiwa hivyo walipata fursa ya kumuaga shujaa huyu.

Baadaye mwili huo mwili huo uliondoka uwanja wa ndege kwenda CCM Kirumba, na ukiongozwa na vikosi maalumu vya jeshi huku ukisindikizwa na helikopta za kijeshi zilizokuwa juu angani.

Wakiwa wamefurika barabarani kuanzia uwanjani hapo, wananchi walionekana wakikimbia sambamba na mwili huo huku baadhi ya vijana wa kike na wa kiume, wamachinga wakisikika wakiimba “Magufuli Jeshi, nenda Baba!” Biashara zafungwa

Aidha, mitaa ya Jiji la Mwanza na vitongoji vyake biashara zote zilifungwa ili kuwapisha wananchi kutoa heshima zao za mwisho na kuuaga mwili wa Rais Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, mwaka huu mkoani Dar es Salaam.

Eneo la Sabasaba ambako maduka yote yalifungwa, maelfu ya wananchi wakiwa barabarani mama mmoja mtu mzima alilala barabarani na kuondolewa na watu wa usalama.

Kwenye daraja maarufu la Furahisha lililojengwa kwa uamuzi wa Dk Magufuli baada ya kusitishwa kwa sherehe za Uhuru na fedha zilizotengwa kwa maadhimisho ya sherehe hizo zikajenga daraja hilo, maelfu ya wananchi walisimama barabarani huku wakisukumana kwa lengo la kuushuhudia mwili wa mpendwa wao.

Katika maeneo ya barabara ya Nyasaka-BuzurugaBuswelu ambayo ilijengwa ilijengwa na Rais Magufuli wakati wa uhai wake akiwa Waziri wa Ujenzi, wananchi wengi waliangua vilio huku wakinyanyua juu matawi ya miti na kuweka khanga barabarani katika maeneo ya Nyasaka-Buzuruga- SinaiUstawi-Mabatini- Mjini, kama ishara ya kumuenzi Eneo la mjini kati kwenye barabara maarufu ya Nyerere, wamachinga walikuwa wakilia huku wengine wakiimba wimbo wa Magufuli Jeshi.

CCM Kirumba ‘yatapika’ CCM Kirumba ambako kulifurika maelfu ya waombolezaji wakiwamo viongozi wa serikali (mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na wabunge), walionekana wenye simanzi kubwa, huku baadhi ya wananchi wakiangua vilio.

Dada aliyevalia gauni jeupe alionekana akishikiliwa na wenzake huku akilia, na akisema, “Rais wetu umetuacha.

” Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza, Renatus Nkwande alisema kupitia utumishi wa Dk Magufuli umewafundisha wananchi na viongozi wa Tanzania kujitolea kwa ajili ya wengi kwa kuchapa kazi ili taifa liendelea na kuimarika kiuchumi.

Shehe wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke alisema Dk Magufuli alikuwa Rais mchapakazi na alikuwa ni zawadi kwa Watanzania.

“Alifanya kazi usiku na mchana akiwatumikia Watanzania huku akimtegemea Mungu, nasema siku zote atabaki kwenye nyoyo za maisha ya watu,” alisema Shehe Kabeke.

Mwenyekiti wa Kitaifa wa Kamati ya Mazishi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema ibada iliyofanyika jana ilikuwa ni mwendelezo wa ibada nyingine zilizofanyika katika mji wa Dodoma na Zanzibar za kuuaga mwili wa Dk Magufuli.

Alisisitiza kuwa jiji na Mkoa wa Mwanza ni sehemu ya kihistoria kwa Dk Magufuli ambaye wakati wa uhai wake aliishi, alisoma na kufanya kazi jijini Mwanza.

Alifanya kazi Chama cha Ushirika cha Nyanza jijini humo.

 “Amefanya mambo makubwa ya kimaendeleo katika jiji hili la Mwanza, lakini pia Rais Magufuli ameacha alama kila mahali katika nchi yetu na kila mahali Watanzania wanamlilia,” alisema Majaliwa.

Busisi wamuombea Baada ya Mwanza, mwili wa Dk Magufuli ulianza safari ya kwenda katika kituo chake cha mwisho Chato, ambako njiani ilisimama Busisi nyumbani kwao Mama Janet Magufuli; Sengerema ambako Dk Magufuli alifundisha katika sekondari ya Sengerema; Geita, Buseresere, Katoro, Bwanga na kisha Chato.

Busisi ulisimama kwa dakika 10 na kuombewa na viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislamu kutokana na ukweli kuwa ndiko anakotoka mkewe au ukweni kwake Dk Magufuli.

Awali, msafara wake ulivuka Ziwa Victoria, lakini haukutumia daraja analolenga lenye urefu wa kilometa 3.2 ambalo halijakamilika, ila ulivukakwa kutumia kivuko.

 Njiani humo hali ilikuwa ya majonzi na mwili ulipofika Geita, baadhi ya watu walijaribu kuzuia msafara wake hadi kulazimika watu wa usalama kuingilia kati na kuwatawanya ili kuruhusu msafara uendelee na safari, Dar ilianzisha safari Mkoani Dar es Salaam, wakazi wake walifurika kwa wingi katika Uwanja wa Uhuru kuanzia Machi 20 na 21, mwaka huu kutokana na mkoa huo kupewa siku mbili.

Katika jiji hilo, safari ya kutoa heshima za mwisho ilianzia kanisani St Peters ambako alikuwa akisali wakati wa uhai wake, kwa ibada na baada ya hapo ulipelekwa Uhuru kwa ajili ya viongozi kutoa heshima zao za mwisho.

Jiji la Dar es Salaam lilizizima baada ya wakazi wake kujitokeza kwa wingi barabarani kuuaga kwa vilio na nyimbo za maombolezo mwili ukipitishwa kutoka St Peters kwenda Uwanja wa Uhuru.

Takribani njia nzima ulikopitishwa, barabara zilijaa mafuriko ya watu waliojikusanya pembezoni wakipunga mkono wa kwaheri, wakitandaza khanga, kurusha maua na majani, wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali na wengi waliangua vilio.

Ulipowasili Uwanja wa Uhuru hali ilikuwa ni ya simanzi na huzuni kutokana na sauti za vilio kila kona ya uwanja huo ambako baada ya ibada kufanyika, viongozi waliaga na baadaye wananchi.

Siku ya pili yake hali ilikuwa mbaya uwanjani hapo kutokana na mafuriko ya wananchi kujitokeza wakitaka kumuaga mpendwa wao kiasi cha kulazimika kusitisha kutoa heshima za mwisho kwa mtu mmoja mmoja na kuzungusha gari iliyobeba mwili wa kiongozi huyo mara tano uwanjani hapo.

Jijini Dodoma, mwili huo ulianza kuagwa rasmi Machi 21 ulipowasili saa moja jioni ambako njia zote ulikopita kutoka Uwanja wa Ndege wa Dodoma, kwenda Ikulu ya Chamwino ulipokelewa na watu waliojikusanya kuuaga kwa vilio.

Shughuli ya kutoa heshima na mazishi ya kitaifa zilifanyika Machi 22 kwenye Uwanja wa Jamhuri mbele ya viongozi wa kitaifa, kimataifa wakiwamo wakuu wa nchi tisa, mabalozi, viongozi wa mashirika ya kimataifa na wananchi.

Awali, kabla ya shughuli hiyo ya mazishi ya kitaifa, mwili huo uliagwa bungeni ambako Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema wabunge wana majonzi kwa sababu wamefiwa na mwenzao, wamezidiwa, na wamechanganyikiwa na wanamshukuru Mungu kwa maisha ya Dk Magufuli aliyekuwa mbungte tangu mwaka 1995.

Katika mazishi hayo ya kitaifa, Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza kuwa Tanzania ipo salama na kuwataka Watanzania kuwa wavumilivu katika kipindi cha maombolezo ya kifo cha Dk Magufuli.

Baada ya mazishi hayo ya kitaifa, wananchi wa Zanzibar juzi walipata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho kwa Dk Magufuli ambako Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alisema ni nadra kumpata kiongozi wa aina ya Magufuli akimtaja kuwa ni mwanamapinduzi wa karne ya sasa aliyejipambanua kuleta maendeleo na kuwatetea wanyonge.

 

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi