loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JOHN POMBE MAGUFULI Kwaheri Rais wa maono, mtekelezaji

“SIKU moja mtanikumbuka, na mimi ninajua mtanikumbuka kwa mazuri si kwa mabaya. Kwa sababu mimi nime-sacrifi ce maisha yangu kwa ajili ya Watanzania maskini. Kwa hiyo tusimame pamoja, tusibaguane kwa vyama, tusibaguane kwa ajili ya dini zetu, tusibaguane hata kwa makabila yetu, sisi tuijenge Tanzania.”

Kauli hii katika moja ya hotuba za Rais John Magufuli imedhihirisha hilo tangu aliyekuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alipolitangaza taifa na dunia kwa ujumla kifo cha Dk Magufuli usiku wa Machi 17, mwaka huu.

Umma wa Watanzania umepigwa na butwaa na vilio na simanzi ndio vimetawala tangu tangazo hilo lilipotolewa, na kwa siku takriban sita za kuaga mwili wa shujaa huyu, upendo wa Watanzania kwa Rais wao kipenzi umeonekana wazi kwa jinsi maelfu walivyojitokeza katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mwanza, Geita na nyumbani kwao Chato kumuaga kiongozi huyu aliyejitoa sadaka kwa ajili ya Watanzania.

Hakuna shaka msemo wake huo wa kujitoa sadaka kwa ajili ya Watanzania umekuwa ni ushahidi tosha wa jinsi kwa miaka mitano na miezi mitano ya kuongoza taifa, alivyojitolea mchana na usiku ‘kuisuka’ Tanzania kwa ajili ya maslahi ya Watanzania wenzake, tena mamilioni ya wanyonge ambao jina lake wataliandika kwa herufi za dhahabu.

Wengi walimfahamu Dk John Magufuli kwa uchapakazi wako alipokuwa Waziri wa Ujenzi katika utawala wa Rais Benjamin Mkapa na kisha Rais Jakaya Kikwete. Wengi hawakumfahamu sana alipokuwa mwalimu kule Sengerema mkoani Mwanza au alipokuwa mkemia wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza jijini Mwanza.

Akiwa Ujenzi, Dk Magufuli alikuwa miongoni mwa mawaziri wa kupigiwa mfano. Akiwa kinara katika kusimamia kujenga barabara za Tanzania chini ya Mzee Mkapa na baadaye Mzee Kikwete, kiasi kwamba alifahamika kwa wananchi wa kutunza kujua barabara zote kwa urefu wake na hata gharama za ujenzi.

Hata alipohamishiwa kwa muda mfupi Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, nako alikuwa hodari katika kujua idadi ya samaki na mifugo iliyokuwapo nchini kwa kichwa, kiasi akabandikwa jina la ‘Waziri wa Kitoweo.’

Lakini Watanzania wamemfaidi Dk Magufuli ambaye siye mwalimu wa sekondari ya Sengerema, mkemia wa Nyanza, mbunge wa Biharamulo Mashariki au Chato, Naibu Waziri wa Ujenzi, Waziri wa Ujenzi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, bali wamemfaidi Magufuli aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano kuanzia Novemba 5, 2015 hadi Machi 17, 2021.

Huyu ndiye Magufuli yule ambaye alisema kwa maneno yake kwamba, “siku moja mtanikumbuka, na mimi ninajua mtanikumbuka kwa mazuri si kwa mabaya.” Naam, Tanzania na dunia inamkumbuka Magufuli kwa mazuri na si kwa mabaya. Watanzania kwa mamilioni yao bila kujali umri wala jinsi wala rangi, kila mmoja analia akimlilia mtu aliyejitoa sadaka kwa ajili yao.

Tangu siku ile ya kwanza aliposhtukiza Wizara ya Fedha na Mipango na kisha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili hadi alipofanya kazi yake ya mwisho hadharani ya kuzindua nyumba pale Kurasini mwishoni mwa Februari mwaka huu, Rais Magufuli amekuwa kipenzi cha Watanzania, Watanzania wanyonge na wale wote wasiopenda rushwa, wizi, dhuluma, ufisadi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya madaraka, wavivu na wazembe.

Akajipambanua kuwa mtetezi wa wanyonge, akawa kimbilio lao na wale wazembe na wabadhirifu wakakaa mbali naye. Kila alikopita aliacha alama, alama ambayo itadumu milele hadi vizazi vijavyo. Akatibu majeraha ya watu wengi walioumizwa kwa namna moja au nyingine na madhila mengi ya utendaji usiojali misingi ya utumishi na sheria.

Alitatua migogoro iliyoonekana haiwezekani lakini kwake ilikuwa kazi nyepesi. Akafukua kila uozo bila kujali uozo huo ulivyo. Na hapa ndipo aliposema mwenyewe kuwa ameamua kuwa mtumbuaji majipu. Sote tunajua jipu lilivyo.

Watumishi wazembe, wabadhirifu na wasiozingatia sheria na taratibu wakakumbana na tumbuatumbua yake. Wakawekwa kando kupisha kwani wameshindwa kumudu kasi yake.

JPM hakutaka kuona hadithi nyingi, alitaka kuona matokeo ambayo ndiyo leo yameacha alama zisizoweza kufutika katika utawala wake. Hilo linathibitishwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Mtu aliyedumu naye kwa miaka yote ya uongozi wake akiwa Makamu wa Rais. Samia anasema amejifunza mengi kutoka kwa Rais Magufuli ikiwamo kufanya kazi kwa juhudi na alichokuwa akiangalia ni kupata matokeo wala si visingizio au lawama. Hakutaka watendaji wake wazungumze, bali watende. Hakupenda maneno maneno mengi, alitaka vitendo.

Aliamini Watanzania wamesikia maneno mengi sana, hivyo ni wakati wa kutenda. Alikuwa mtekelezaji. Ndio maana alipoona mradi fulani umekwama na fedha zimetolewa, hakuacha kuwatumbua wahusika. Hakulea uzembe. JPM pia alikuwa mwenye maono. Maono yake ndiyo yameifanya Tanzania ipigiwe mfano kimataifa.

Alisisitiza Tanzania siyo nchi masikini, ni nchi tajiri. Na hilo pia limedhihirisha katika uongozi wake hasa maboresho makubwa katika sekta ya madini ambako leo hii Tanzania inaweza kutembea kifua mbele ikijivunia rasilimali hiyo.

Na katika hili la umasikini, ameonesha kuwa Tanzania na nchi za Afrika zinaweza kujitegemea kwa kutumia rasilimali zake wenyewe. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya wakati wa mazishi ya kitaifa jijini Dodoma, amelisema hili.

Amekubali uthubutu uliofanywa na Rais Magufuli, ambao umethibitisha Afrika inaweza kujitegemea kwa rasilimali zake bila kutegemea misaada ya nje ambayo huja na masharti ya hovyo.

Amejenga Reli ya Kisasa (SGR), Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), kununua ndege 11 (nane tayari) bila ya senti ya kutoka nje. Na ameacha miradi mingine mingi ambayo inaendeshwa bila kumtegemea ‘beberu’ yeyote. Hatua yake hii haikuwapendeza wengi hasa mataifa ya Magharibi ambayo yalimkejeli na kumpa majina ya kuonesha alikuwa akiongoza Tanzania kwa ‘mkono wa chuma.’

Lakini hilo halikuwa kweli. Watanzania wanafahamu ukweli. Wanajua jinsi nchi hii ilivyokuwa imegeuzwa shamba la bibi, kila mtu anajichotea anavyotaka. Hata wakati wa janga la corona lilipoikumba dunia kuanzia Desemba 2019, na kuingia rasmi Tanzania Machi 2020, nchi za Magharibi zilijaribu kuonesha kuwa hayuko sahihi katika mbinu zake za kukabili ugonjwa huo. Lakini ukweli ukasimama.

Rais Magufuli akaivusha nchi salama katika janga hili na akapigiwa mfano hata na wale waliombeza. Rais Magufuli ambaye kwa utendaji wake alipachikwa majina mengi ya kuonesha umahiri wake kama jemedari, chuma, jembe, tingatinga, mwamba, shujaa, jeshi kubwa; hakuwa mtu wa simile. Aliwanyoosha wazembe bila kujali umaarufu wao, ukaribu wao na yeye, urafiki na mengineyo.

Hakuwa na rafiki katika kazi. Lakini pia alikuwa mtu wa utani mwingi. Hotuba zake licha ya kujaa maneno ya kutoa maagizo, lakini pia zilijaa utani. Alitaniana na kila mmoja. Spika wa Bunge, Job Ndugai na Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, ni miongoni mwa waliotaniwa sana.

Alizungumza lugha nyingi za Tanzania, hivyo kutaniania na watu. Rais Samia amethibitisha hili kuwa Dk Magufuli alikuwa mtu wa utani mwingi. Watanzania watazikosa hotuba zake hizo. Watamkosa Rais aliyekuwa anapenda sana safari za kutembea kwa barabara ambazo alizitumia kusalimiana na wananchi njiani, akitatua kero zao.

Mikutano hii ilikuwa maarufu sana. Kubwa jingine, Rais Magufuli alikuwa mcha Mungu. Alisisitiza sana Watanzania kumtegemea Mungu. Katika moja ya hotuba zake za mwisho, alisisitiza kuwa Watanzania wamtumainie Mungu, wasiogope kufa, kwani hakuna anayejua atakufa kwa ugonjwa gani. Hata yeye alisema atakufa.

Kama alivyosema Rais Samia, Dk Magufuli ameondoka mapema, lakini amefunga hesabu zake hapa duniani ameacha sadaka ambayo rehemu zake zitamfuata kadiri wananchi wanakavyokuwa wanatumia huduma mbalimbali kama za hospitali kwa ajili ya kujenga afya zao, za maji kuwatua ndoo wanawake vichwani, barabara, na elimu kufuta ujinga.

Kwaheri John Joseph Magufuli (JPM). Rais wa maono na mtekelezaji. Tanzania, Afrika na dunia itakukumbuka daima. Jina lako limeandikwa kwa herufi za dhahabu. Nenda shujaa. Kapumzike chuma.

WATU hutegemea mvua ili kufanikisha shughuli mbalimbali, ikiwamo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi