loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Zawadi JPM alizowaachia Watanzania

ILIKUWA Novemba 5, 2015 ambako Tanzania ilipata Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli baada ya kuapishwa rasmi siku hiyo kuwatumikia.

Unaweza kusema kuchaguliwa na Watanzania kwa Rais huyo ilikuwa ni neema na zawadi kwao, kwani hata baada ya kifo chake kilichotokea Machi 17, mwaka huu, aliwaachia zawadi lukuki zilizotokana na mafanikio ya utendaji wake.

Akiyazungumzia mafanikio hayo katika shughuli ya mazishi ya kitaifa iliyofanyika Jumatatu wiki hii kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi anasema kiongozi huyo amewaachia mafanikio lukuki Watanzania.

Dk Magufuli ambaye ni Rais wa Awamu ya Tano, alifariki dunia Machi 17, saa 12 jioni katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa baada ya kusumbuliwa na tatizo la umeme wa moyo.

Profesa Kabudi anataja zawadi na mafanikio hayo kuwa ni kuhamisha Makao Makuu ya Serikali mkoani Dodoma mwaka 2016 uamuzi ambao ulikuwa haujatekelezwa kwa miaka mingi tangu mwaka 1973.

Rais Magufuli akitumia mamlaka aliyopewa na Katiba alivunja iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), alisaidia kuondoa kero za ardhi zilizokuwa kilio kwa wananchi.

Baadaye alipandisha hadhi mji wa Dodoma na kuwa Jiji, hatua iliyoubadilisha mji huo na kuwa kivutio kwa wengi. Tayari soko kubwa la kisasa limeshajengwa ambalo linaitwa Soko la Job Ndugai linalotarajiwa kuwavutia wengi na kuifanya Dodoma kuongeza nguvu za kiuchumi.

Mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato-Dodoma ni zawadi nyingine aliyoacha Magufuli na ambayo inaaminika Rais mpya Samia Suluhu Hassan atakamilisha ndoto hiyo.

Vilevile ndoto ya ujenzi wa Mradi wa Barabara ya njia nne ya kilometa 112.3 ambayo inatarajiwa kupamba Jiji la Dodoma. Ujenzi wa uwanja wa michezo wa kisasa wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 80,000 unatarajiwa kuwa kimbilio la watu wengi ndani na nje ya nchi.

Upanuzi wa Ikulu ya Dodoma wenye eneo la mita za mraba 34,000 ni mradi mwingine ambao utakumbukwa kufanywa na Magufuli nchini mwake.

Aidha, anasema pia alirejesha nidhamu ya utendaji kazi na uadilifu wa umma kwa kuondoa watumishi wasiokuwa na maadili na utendaji mzuri serikalini; aliimarisha utumishi wa umma kwa kuondoa watumishi wasiokuwa na sifa ambao walighushi vyeti vya elimu na kuondoa watumishi hewa katika orodha ya mishahara ya watumishi wa umma.

“Pia alihimiza utendaji kazi wenye kujali matokeo, matumizi bora ya rasilimali za umma na utoaji wa huduma bora kwa wananchi kupitia kaulimbiu yake ya Hapa Kazi Tu,” anaeleza Profesa Kabudi.

Anasema kiongozi huyo aliimarisha utawala wa sheria na utoaji wa haki sawa kwa wote na kwa wakati na kuimarisha mfumo wa mapambano dhidi ya rushwa, usimamizi wa maadili ya viongozi wa umma, usimamizi wa masuala ya haki za binadamu na ustawi wa demokrasia nchini.

Anasema pia aliimarisha mapambanno dhidi ya rushwa kwa kuanzisha Mahakama ya Rushwa na Makosa ya Uhujumu Uchumi maarufu kama Mahakama ya Mafisadi, kubadilisha muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuanzisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuimarisha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Pamoja na hayo, Profesa Kabudi anafafanua kuwa Dk Magufuli aliimarisha ushirikiano baina ya serikali na mihimili ya Bunge na Mahakama na kuimarisha ushirikiano wa Afrika Mashariki kikanda na kimataifa. Katika eneo la kuongezeka kwa Pato la Taifa, anasema Rais Magufuli aliimarisha ukusanyanyaji wa mapato ya serikali na kusimamia matumizi ya fedha za serikali na hivyo kuwezesha kuongezeka kwa pato la serikali hadi kufikia wastani wa asilimia 6.8 mwaka 2019.

Anasema pia alifanikisha kuifanya Tanzania kuingia kwenye kundi la nchi za uchumi wa kati mwaka jana, miaka mitano kabla ya muda uliopangwa ambao ni mwaka 2025.

Kwa upande wa sekta ya viwanda, anaeleza kuwa aliongeza fursa za kiuchumi na biashara kwa makundi mbalimbali hususani Watanzania wenye kipato cha chini, kukuza sekta ya viwanda kwa kuhamasisha ujenzi wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa nchini ambapo katika utawala wake jumla ya viwanda 8,477 vilijengwa. Katika sekta ya madini, anasema alidhibiti upotevu wa mapato yanayotokana na usafirishaji wa madini kwa kutunga sheria mpya ya madini iliyowezesha kupitia upya mikataba yote ya madini.

“Alianzisha masoko ya madini katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini, kujenga ukuta wa Mirerani ili kudhibiti upotevu wa madini ya tanzanite na kupanua umiliki wa hisa za serikali kwenye kampuni za madini kuanzia asilimia 16 inayoweza kufika hadi asilimia 50,” anasema Profesa Kabudi.

Aidha, aliwezesha lugha ya Kiswahili kuwa moja ya lugha za mawasiliano katika mikutano ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Rais Magufuli atakumbukwa kwa ushirikiano na nchi kama vile Ethiopia, Afrika Kusini na Morocco ambazo zilihitaji wataalamu wa lugha hiyo ili kutoa elimu kwa wananchi wao.

Alisaini makubaliano na Afrika Kusini ya kutoa wataalamu wa Kiswahili. Kwa upande wa nishati, anasema Rais Magufuli alianzisha utekelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme ukiwemo Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere, Rufiji na Rusumo katika mpaka wa Tanzania, Rwanda na Burundi.

Pia alisitisha ukodishaji wa mitambo ya dharura ya umeme inayotumia mafuta mazito ambayo ilikuwa ikigharimu serikali fedha nyingi.

“Alipitia upya na kusitisha baadhi ya mikataba kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na wazalishaji binafsi wa umeme ambayo ilikuwa haina tija kwa taifa,” anaeleza.

Anasema pia kiongozi huyo wakati wa utawala wake aliongeza kasi ya kusambaza umeme vijijini kwa kutumia vifaa vilivyotengenezwa nchini na kuimarisha mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja na hivyo kupunguza gharama zinazotokana na meli kuchelewa kushusha mafuta bandarini.

Dk Magufuli pia aliongeza kasi ya ujenzi wa barabara za lami na kuifanya nchi kuwa na jumla ya mtandao wa barabara za lami wenye jumla ya kilometa 12,964, kujenga madaraja makubwa 13 likiwamo Daraja la Magufuli mto Kilombero na Daraja la Nyerere Kigamboni, Dar es Salaam.

Pia, alijenga barabara za juu za Mfugale na Kijazi mkoani Dar es Salaam, kujenga barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha ambayo hadi mauti inamfika ujenzi wake unakaribia kukamilika.

Pia alijenga daraja jipya la Salender ambalo likikamilika litajulikana kama Daraja la Tanzanite mkoani Dar es Salaam. Alinunua meli na vivuko ambavyo vimesaidia kuondoa adha ya usafiri kwa Watanzania na kuanzisha Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) katika kuhakikisha ujenzi wa barabara zilizo kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa unatekelezwa kwa ufanisi.

Katika eneo la uchukuzi, pia alinunua ndege mpya nane na kuongeza idadi ya wasafiri wa anga nchini na hivyo kuongeza huduma za usafiri wa anga, kujenga na kukarabati viwanja vya ndege nchini ili kuimarisha ubora wake.

Pia kujenga kukarabati bandari zikiwemo za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga. Pia alifufua na kuimarisha kampuni ya meli hatua iliyowezesha ukarabati wa meli na chelezo kufanyika kwa ufanisi.

Kuimarisha huduma za usafirishaji kwa njia ya meli kwa kuanzisha Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC). Alianzisha na kusimamia ujenzi wa reli kwa kiwango cha kimataifa (SGR), kufufua reli ya Tanga hadi Arusha na kurejesha huduma hiyo iliyokuwa imesimama muda mrefu na kununua mabehewa na vichwa vya treni ili kuboresha usafiri huo.

Anasema katika upande wa huduma za jamii, alisimamia miradi ya maji, kuanzisha utoaji wa elimu bila ada hadi kidato cha nne ili kuwezesha watoto wote kupata elimu.

Kuboresha mazingira ya kufundishia kwa kujenga shule na maabara zaidi, kukarabati shule kongwe na kujenga nyumba za walimu na kuajiri walimu. Kwa upande wa uhusiano wa kimataifa aliimarisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi nyingine duniani na alifungua balozi nane mpya katika nchi za Algeria, Cuba, Korea Kusini, Namibia, Sudan na Uturuki.

Profesa Kabudi anaeleza kuwa Rais Magufuli alitunukiwa tuzo mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa kutambua mchango wake katika maeneo mbalimbali.

Swali: Nia ya kufunga ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi