loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM alivyowatua ndoo wanawake

JPM alivyowatua ndoo wanawake

MIONGONI mwa mambo ambayo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imeyashughulikia kwa nguvu zote ni upatikanaji wa maji safi na salama kwa Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini.

Wakati analihutubia Taifa jijini Dodoma, Novemba mwaka jana, Rais Magufuli alisema serikali yake inatekeleza miradi 1,400 ya maji nchi nzima ukiwemo mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria jijini Mwanza kwenda Shinyanga- Nzega-Tabora hadi Igunga ambao pia utatoka Tabora-Itigi-Manyoni umbali wa kilometa 220 na kisha kufika Dodoma kilometa 127 pamoja na mradi wa Sh bilioni 520 mkoani Arusha na miradi mingine mingi kila mahali.

Hivi karibuni, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi wakati wa Wasilisho lake kuhusu utekelezaji wa serikali katika masuala mbalimbali, amesema Serikali ya Rais Magufuli imetumia jumla ya Sh trilioni 1.916 kutekeleza jumla ya miradi 1,845 ya maji kuanzia mwaka 2015 mpaka mauti inamkuta Machi 17 mwaka huu.

Dk Abbasi anasema Serikali ya Rais Magufuli iliweka msukumo wa dhati katika kuwapatia wananchi maji na kuwaondolea kero za miaka mingi. Anasema kwa kutambua umuhimu huo, serikali yake ilijiwekea malengo ya kuhakikisha huduma bora ya maji kwa wananchi mijini inapatikana kwa zaidi ya asilimia 95 na vijijini inapatikana kwa zaidi ya asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.

“Ili kufikia malengo, utekelezaji unafanyika kupitia mageuzi ya kimfumo na kimuundo, miradi mikubwa na midogo, uwezeshaji wa Taasisi zinazotoa huduma pamoja na kuchukua hatua za kuwawajibisha watoa huduma na watendaji pale ilipobidi,” alisema Dk Abbasi.

Dk Abbasi anasema uamuzi wa serikali wa kuziunganisha Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) na Shirika la Huduma ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO), umeongeza ufanisi wa utoaji huduma na kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza mapato.

Anasema kutokana na uamuzi huu, mapato ya DAWASA kwa mwaka yameongezeka kutoka Sh bilioni 70.19 mwaka 2015/16 na kufikia Sh bilioni 137.573 mwaka 2019/20.

“Pia uamuzi uliofanywa na Rais Magufuli wa kuwahamisha wataalamu wa sekta ya maji kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwenda Wizara ya Maji umeimarisha uwajibikaji, umeleta mafanikio na ufanisi katika utekelezaji wa miradi na usimamizi wa huduma zinazotolewa,” anasema Dk Abbasi.

Anabainisha kuwa uamuzi huo wa Serikali ya Rais Magufuli ulisaidia watendaji wazembe 98 kuchukuliwa hatua na wakandarasi 59 kusitishiwa mikataba ambapo kulikuwa na miradi chefuchefu 177 ukiwemo mradi wa Ntomoko- Dodoma ambayo ilikuwa haiishi au ikiisha maji yalikuwa hayatoki. Dk Abbasi anasema kuwa mpaka sasa miradi 85 kati ya hiyo inafanya kazi na iliyobaki itakamilika Juni mwaka huu.

Ameitaja miradi mingine iliyoanza kazi kuwa ni Nyamtukuza– Geita, Mibono–Tabora, Rugeye– Mwanza, Malinyi–Morogoro, Kinesi–Mara, Galijembe–Mbeya, Milonji–Ruvuma, Lupunga-Morogoro na Muze Group–Rukwa.

Pia anasema kuanzishwa kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mwaka 2019, kumeongeza kasi ya miradi ya maji vijijini na kwa sasa huduma za maji vijijini zimeongezeka kutoka wastani wa asilimia 47 mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa asilimia 72.3 sasa.

“Hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Magufuli ilitekeleza jumla ya miradi 1,845 yenye thamani ya Sh trilioni 1.916 na kunufaisha wananchi milioni 14.73,” anaeleza Dk Abbasi.

Anabainisha kuwa kati ya miradi hii, miradi 222 ya mijini na miradi 1,623 ya vijijini na kuongeza kuwa kwa sasa kazi inaendelea kwenye miradi 924 yenye thamani ya Sh trilioni 2.212 ambapo kwa maeneo ya mijini kuna miradi 110 na vijijini miradi 814 na inatarajiwa kuwanufaisha wananchi milioni 12.08 itakapokamilika.

Kutokana na uwekezaji huu uliofanywa na Rais Magufuli kwenye sekta ya maji enzi za uhai wake, Dk Abbasi anasema umeleta mafanikio kwenye huduma ya maji nchini kutoka wastani wa asilimia 47 kwa vijijini na wastani wa asilimia 74 kwa miji mikuu ya mikoa kwa mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa asilimia 72.3 vijijini na wastani wa asilimia 86 kwa miji mikuu ya mikoa.

Anasema uwekezaji huu umeongeza mapato yatokanayo na huduma za maji taka na maji safi katika mamlaka mbalimbali zinazosimamia huduma hizo miaka mitano iliyopita kutoka Sh bilioni 176.87 hadi kufikia zaidi ya Sh bilioni 301 kwa mwaka.

Alipofanya ziara ya kukagua Mradi wa Maji wa Pugu-Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam akiwa Makamu wa Rais Februari 13, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliwahakikishia wananchi kuwa asilimia 25 iliyobaki ya upatikanaji wa maji safi na salama nchini itakamilishwa ndani ya miaka mitano ijayo kwa kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, serikali ilifanikiwa kuwapelekea Watanzania maji safi na salama kwa asilimia 75. “Wakati wa kampeni zetu tulitoa ahadi za kukamilisha upatikanaji wa maji Tanzania.

Katika miaka mitano iliyopita tumeweza kutekeleza upatikanaji wa maji kwa Watanzania kwa asilimia 75, tumebakiwa na asilimia ndogo ambayo tunakwenda kuimalizia ndani ya miaka mitano hii, nawahakikishia Watanzania tunakwenda kumalizia palipobakia,”amesisitiza Rais Samia wakati huo.

Hivi ndiyo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli ilivyotekeleza miradi maji nchini ili Watanzania wapate majisafi na salama, kijiti hiki sasa ameachiwa Rais Samia.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/bb3bc77e26e22368e9cb3f19b43b25c5.png

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi