MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Burundi na klabu ya Yanga, Fiston Abdul Razack anatarajiwa kurudi uwanjani Jumatatu kushishiri mazoezi na timu yake ya Yanga baada ya kupona majeruhi ya misuli ya paja aliyopata katika mchezo wa mwisho dhidi ya Polisi Tanzania uliomalizika kwa sare ya 1-1.
Nyota huyo wa zamani wa Mamelod Sundowns, alipata majeruhi katika mchezo huo ambao ndio alifungua akaunti yake ya mabao katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara mtanange uliopigwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Juma Mwambusi alisema hivi sasa Razack anaendelea vizuri na anatarajiwa kuungana na wenzake Jumatatu kwa ajili ya maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Nafurahi kumuona Fiston akiwa amerejea tena kikosini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya KMC tutakuwa nyumbani,” alisema.
Mwambusi alisema hivi sasa akili yote iko katika mchezo wa KMC ili waendelee kuongeza wigo wa pointi katika mbio za kulisaka taji la Ligi Kuu Tanzania Bara ambalo kwa misimu mitatu mfululizo limechukuliwa na watani wao wa jadi Simba.
Yanga ndio vinara wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikiwa kileleni huku ikiwa wamejikusanyia pointi 50 baada ya kushuka uwanjani mara 23 ikiizidi Simba inayoshika nafasi ya pili kwa alama nne huku ikiwa nyuma kwa michezo mitatu.