loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Maboresho yanavyonyanyua bandari ya Tanga

KIFO cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli, kilimkuta Mama Samia Suluhu Hassan akiwa mkoani Tanga ambako, pamoja na mambo mengine, alikagua maendeleo ya Bandari ya Tanga.

Serikali ilikuwa inaongozwa na Magufuli iliamua kuweka nguvu katika maboresho ya bandari zake ikiwemo ya Tanga kwa kuzipanua na kuzipa vifaa vya kisasa ili kuvutia shehena nyingi kupitia kwenye bandari zetu na hivyo kuboresha uchumi wa nchi yetu.

Bandari ya Tanga inahudumia shehena mbalimbali za mizigo kwa mikoa ya kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa na mizigo zinazotoka au kwenda nchi za jirani za Kenya, Uganda na Rwanda.

Ni bandari ambayo shehena kubwa inayohudumiwa na bandari huyo kwa sasa ni malighafi za viwandani pamoja na mazao ya kilimo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Deusdedit Kakoko (kwa sasa amesimamishwa), alimwambia Mama Samia (sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) kuwa maboresho makubwa yamefanyika katika bandari hiyo kwa kukarabati maghala ya kuhifadhia mizigo, ujenzi wa gati pamoja na ununuziwa vifaa.

Alifafanua kwamba wameweza kufanya marekebisho ya maghala namba 7/6 ya bandari hiyo kwa gharama ya zaidi ya Sh milioni 422 na kwamba kabla ya ukarabati huo maghala hayo yalikuwa hayafanyikazi kwa muda mrefu na hivyo sasa yataweza kuhifadhi shehena za mizigo.

Alisema kuwa mara na baada ya ukarabati huo Bandari ya Tanga imeanza kupokea wateja wakubwa wa tani zaidi ya 55,000 ambao wanaleta shehena nyingi ya malighafi inayotumika kwa shughuli za ujenzi ikiwemo kutengeneza simenti iitwayo clinker kwenda nchi jirani ya Rwanda.

"Awali wateja hao wakubwa wa sheheba hiyo walikuwa wanakwenda bandari ya nchi jirani lakini kwa maboresho ya bandari ya Tanga tumeweza kuwashawishi na sasa wameanza kuhamia huku kidogo kidogo," alisema Kakoko.

Kwa upande wa ujenzi wa gati Kakoko alisema wameweza kuchimba eneo la kugeuzia meli awamu ya kwanza huku awamu yapili ikiwa ni kujenga gati kwa mita 100 zilizobaki ili kuruhusu meli kubwa kuweza kutia nanga karibu na bandari hiyo.

"Tunajenga gati yenye urefu wa mita 450, ambayo itakuwa na uwezo wa kuingiza meli mbili kwa wakati mmoja, na hivyo kuongeza uwezo wa kutoa huduma mara 15 ya sasa hivi," alisema Kakoko.

Alisema kuwa katika awamu ya kwanza mkandarasi ambaye ni kampuni ya Check anatarajiwa kujenga eneo la kugeuzia meli kwa sababu mradi ulikuwa kwenye majaribio, hivyo ameweza kuchimba eneo la kuingizia meli na sasa linatumika kushusha mzigo kwenye eneo la km100.

“Awamu ya pili ya sasa hivi mkandarasi yupo eneo la mradi, anatazamiwa kujenga gati yenye urefu wa meta 150, na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwisho mwaka huu.

“Kwa sasa meli zenye urefu wa meta 80 ndio zinafika hadi hapa kwenye gati lakini kipande hicho kinachomaliziwa kujengwa kikimalika meli itaweza kuhudumiwa hapa karibu na bandari,” alisema Kakoko.

Aidha alisema kuwa kwa mwaka wa fedha tunaoenda kuuanza mkandarasi atakuwa amekamilisha ujenzi wa gati hiyo hadi kufikia meta 300 na hivyo kuendelea kutumiwa wakati akitarajiwa kumaliza eneo lililobaki ifikapo mwishoni mwa mwaka 2022.

“Hili eneo litakuwa na uwezo wa kuingiza meli mbili kwa wakati mmoja, kutakuwa na eneo la kugeuzia meli pamoja na gati hivyo shehena ya mizigo itaweza kuhudumiwa kwa haraka katika eneo hilo,” alibainisha Kakoko.

Alisema kuwa maboresho hayo yanalenga kuhakikisha bandari ya Tanga nayo inaweza kuhudumia meli yenye urefu wa mita hadi 230 kwa wakati mmoja kama ilivyo sasa kwa bandari ya Dar es Salaam.

Kadhalika alisema kuwa maboresho hayo yanakwenda sambamba na kupunguza mrundikano wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam na hivyo kwa wateja walioko katika nchi za jirani za Uganda, Rwanda na sehemu ya DRC watakuwa wanapata huduma kupitia Bandari ya Tanga.

Akizungumzia uboreshwaji wa vifaa katika bandari hiyo, Kakoko alisema kuwa serikali imeweza kuleta mitambo ya kisasa kwa ajili ya kuhudumia sheheha ya mizigo kwa wingi katika kipindi kifupi kama ilivyo katika bandari ya Dar es Salaam.

“Sasa lile tatizo la uhaba wa mitambo linakwenda kumalizika katika bandari ya Tanga kwani mradi huu wa ujenzi unakwenda sambamba na ufungaji wa mitambo ya kisasa ya kuhudumia shehena ya mizigo,” alisema Mkurungenzi huyo.

Bandari ya Tanga ilianzishwa mwaka 1888 na wakoloni. Licha ya kuwa miongoni mwa bandari kongwe nchini ambazo zimekuwa zikifanya shughuli za upakuaji na upakiaji wa shehena za mizigo, inatajwa kuwa bandari kongwe zaidi kuliko zote Afrika Mashariki.

Shughuli za huduma za kibandari katika banadari hii huwa zinafanywaa katika maeneo mawili ambapo meli zenye uzito wa tani 1,200 huhudumiwa nangani ambapo ni umbali wa mita nane hadi 18 kwenye kina kirefu cha bahari.

Lakini meli zenye uzito wa chini ya hapo huhudumiwa kwenye gati bandarini. Kwa sasa gati la bandari hii lina urefu wa meta 381 na kina cha maji kimekuwa kikiongezwa kutoka meta tatu za awali maji yanapokupwa na meta 4.4 yanapojaa hadi takribani meta 13.

Mwaka 2017, wakati wa kuzindua ujenzi bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani Tanga, Mkuu wa Mkoa huo, Martine Shigela, alimwomba hayati Dk Magufuli kuipanua bandari hiyo, ombi ambali alilikubali.

Katika mahojiano na gazeti hili, Shigela alisema alitamani kirefushwe hadi kufika mita 12.

“Tukifikia kiwango hicho, meli kubwa zinaweza kuanza kuja hapa Tanga, kutua mzigo ya hapa na mikoa ya jirani au kutoa hapa mizigo na kusafirisha katika maeneo mengine duniani,” alisema.

Alisema kwamba tatizo lilipo ni kwamba, kwa sasa kutoa mzigo Tanga kuupeleka Dar es Salaam ni ghali kuliko kutoa Dar es Salaam kwenda Uarabuni.

“Kontena moja kutoka hapa Tanga kwenda Dar es Salaam ukachajiwa Dola 1,000 kwa mfano, kontena hilo hilo ukilitoa Dar es Salaam kwenda Riyadh (Saudi Arabia) unaweza kuambiwa Dola 300 au 400 tu,” alisema.

Alisema hiyo ni kutokana na Tanzania kutokuwa na meli Tanzania na badala yake kutegemea makampuni ya meli bnafsi.

“Watu wengi wanaona ni vyema kupeleka mizigo Dar es Salaam kwa malori kwani wakija hapa bandarini kwa hali ilivyo sasa wanaona kama ni hasara. Kwa hiyo kama tutarefusha kina, meli nyingi zitaleta mizigo hapa Tanga badala ya kuipeleka Mombasa au Dar es Salaam moja kwa moja na kisha kuletwa hapa na mikoa ya jirani kama Kilimanjaro, Arusha na Manyara kwa malori,” alisema.

Akaongeza: “Kwa mantiki hiyo bandari ya Tanga haitakuwa na sababu ya kuendela kuwa kama ya kulisha (feeder port) bali bandari inayoweza kupeleka na kutoa meli moja kwa moja katika nchi zingine.”

Alisema meli kubwa zikija hapa Tanga zinalazimika kusimama mbali, kwenye kina cha wastani wa mita 12 na hivyo kushushia mizigo huko kama vile makontena kwenye tishari (barge).

“Halafu lile tishari ndilo linaleta makontena hayo kwenye bandari. Na wakati wa kupakia mizigo ni hivyo hivyo hivyo. Sasa ile watu wengi hawapendi kwa sababu inaongeza gharama na inachukua muda mwingi kuliko kuleta mzigo moja kwa moja kwenye gati,” alisema.

Alisema wafanyabiashara wengine wanaona kama ni hatua inayoweza kusababisha hasara kwani inaweza kutokea kontena likatumbukia baharini.

“Kumbuka meli nazo zinabadilika siku hizi kulingana na urefu, upana na kina na hata kizazi cha sasa cha meli kreni zake siyo kama za zamani. Kwa hiyo kusema labda itakuja na kreni yake, ishushe hapa ipeleke kule unaweza kukuta kitu hicho hakuna,” alisema.

 

Swali: Nia ya kufunga ...

foto
Mwandishi: Amina Omari

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi