loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Machinga Mwanza walipozungumza lugha moja

UZALENDO, umoja na mshikamano wa dhati kwa watanzania, ambao mara kwa mara umekuwa ukihimizwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wa kidini, ulijidhihirisha kwa namna ya kipeeke siku ya kuuaga mwili wa aliyekua Rais wa serikali ya awamu ya tano, Dk John Magufuli, jijini Mwanza.

Ilionekana kama mzaha pale viongozi wa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara wadogo wadogo, marufu kama machinga, walipotangaza kwamba tarehe ya kuaga mwili itakua siku ya mapumziko kwao, na kusisitiza kwamba hakuna biashara yoyote itakayofunguliwa siku hiyo.

Siku mbili kabla ya mwili kuwasili jjini Mwanza, Gazeti hili lilishuhudia viongozi hao wakimfuata na kumsihi Mkuu wa Polis Mkoa (RPC), Jumanne Murilo, awape kibali  machinga hao wasiopungua 10,000, wakiwemo waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda, cha kuongoza msafara uliobeba mwili wa Rais Magufuli.

“Tumekubali maombi yenu. Mtakuwa sehemu ya msafara lakini sio kukaa mbele kama mnavyohitaji. Hii ni kwa sababu za kiusalama lakini vilevile kuheshimu taratibu zilizowekwa. Huu ni msiba wa kitaifa na aliyetutoka ni kiongozi mkuu kabisa, maandalizi yake ni ya kipee ni lazima tufuate taratibu zote zilizowekwa,” RCP aliwajibu.

Licha ya ombi lao kukataliwa (la kukaa mbele ya msafara) Makamu Mwenyekiti wa Bodaboda Mkoa, Joseph Samweli, alisistiza kwamba machinga wote watafunga biashara na kuwa sehemu ya msafara kuanzia uwanja wa ndege hadi mwili utakapoondoka kwenye ardhi ya Mwanza.

“Tumekubaliana na sababu alizotupa Kamada wa polisi kwani usalama ni kwa ajili yetu sote. Hata hivyo, azma yetu iko palepale na tutakua na matukio mbalimbali kabla ya mwili kuwasili, ikiwemo kufagia barabara kuanzia uwanja wa ndege hadi uwanja wa CCM Kirumba utapoagiwa mwili. Tumepewa ruksa pia ya kutandika nguo zetu katika barabara mbalimbali utakapopita msafara,” alisema Makamu Mwenyekiti na kusistiza:

“Sisi tunasema Rais Magufuli alikua ni kiongozi namba moja wa machinga. Kitendo cha kutupatia vitambulisho vinavyoturuhusu kufanya biashara zetu eneo lolote nchini, na kuagiza tusibughudhiwe ni ishara tosha kwamba alikua wetu, tuna kila sababu ya kufunga biashara zetu na kumuaga rasmi. Serikali ilitangaza siku mbili za mapumziko lakini sisi tunaongeza ya tatu, ambayo ni ile ya kuaga mwili wake hapa Mwanza.”

Alisema kwamba wale machinga waliokuwa wameuzunguka uwanja wa Kirumba wakiuza khanga, fulana na vibebeo vya funguo pamoja na picha za Dk Magufuli ilikuwa ni sehemu ya maombolezo na kumuenzi marehemu, na kwamba ndiyo biashara pekee waliyokubaliana machinga wote, na kwamba ifanyike uwanjani tu na si kwingineko.

Gazeti hili lililipita mitaa mbalimbali ya jiji na kukuta kweli biashara zote zilifungwa huku wakazi wakimiminika kandokando ya barabara zote zilizopangwa kupitishwa mwili wa Rais Magufuli.

Katika umoja wao pia ilishuhudiwa machinga hao wakifagia barabara na kutandika nguo, kama ilivyoelekezwa na kamanda wa polisi kwamba shughuli zao zote zifanyike saa kadhaa kabla ya msafara kuingia barabarani.

Na ni kwa umoja na mshikamano huohuo machinga hao walijipanga nyuma ya msafa na kutembea nao kwa mwendo wa mchakamchaka hadi uwanja wa CCM Kirumba na katika mitaa yote ulipopita mwili wa Rais Magufuli.

Askari wa usalama barabarani walionekana wakiliongoza kundi hilo la machinga lililoongozwa na bodaboda ili kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa.

Katibu wa Machinga Wilaya ya Nyamagana, Hidaya Juma, alisistiza kwamba kila machinga aliguswa kwa namna na kuwiwa kushirikia utaratibu waliojiwekea wa kumuenzi Rais Magufuli bila kujali chama au kabila, ikizingatiwa kwamba moyo wa huruma wa marehemu kwa watanzania wa chini haukubagua mtu.

“Hata mwenye hisia za uchama au ukabila leo zimewekwa pembeni. Tumekua kitu kimoja, tunazumgumza lugha moja na kufanya kila jambo kwa pamoja. Tembelea mitaa yote ya jiji hutakuta machinga hata mmoja kwenye biashara mpaka pale mwili wa mpendwa wetu utakapokua umevuka kwenda Geita. Na tutausindikiza hadi kivuko cha Busisi na kurudi kama wamoja,” alisistiza Katibu huyo.

Mbali na barabara ulipopitishwa mwili, HabariLeo pia lilitembelea mitaa mingine ya jiji ikiwemo Lumumba, Liberty, Rwagasole na Uhuru na kukuta maduka na biashara zote zimefungwa.

Kwa sauti ya pamoja pia viongozi hao wa machinga walimuomba Rais mpya, Mama Samia Suluhu Hassan kuendeleza mazingira bora kwa machinga, si tu kwa kumuenzi hayati Magufuli bali pia kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwao na jamii kwa ujumla.

Rais Magufuli aliaga dunia tarehe 17 mwezi huu jijini Dar es Salaam na serikali kutangaza siku 21 za maombolezo.

Kwa kipindi chote hicho serikali na viongozi wa dini wameendelea kuwataka watanzania kudumisha umoja na mshikamo, mojawapo ya tunu za nchi ya Tanzania kwa miongo kadhaa.

Watanzania waliitikia wito huo na kushiriki shughuli za maombolezo kwa utulivu ambapo mwili wa hayati Magufuli ulizungushwa maeneo mbalimbali ya nchi ili kuwapatia nafasi Watanzania kumuaga mpendwa wao huyo.

Ulinzia Dar es Salaa, ukapelekwa Dodoma, Zanzibar, Mwanza na hatimaye Geita wilaya ya Chato alikozaliwa hayati Magufuli ambako ndiko alizikwa.

Katika maeneo yote hayo watanzania waliendelea kuonesha umaoja, uzalendo na mshikamo wao na kuonesha kuweka mbali tofauti zao za kisiasa.

 

Swali: Nia ya kufunga ...

foto
Mwandishi: Abela Msikula

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi