loader
Dstv Habarileo  Mobile
Dk Mpango kuapishwa kesho Chamwino-Dodoma

Dk Mpango kuapishwa kesho Chamwino-Dodoma

PUNDE baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumpitisha Dk Philip Mpango kuwa Makamu wa Rais Mteule wa Tanzania, Dk Mpango ataapishwa kesho Jumatano Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Katika taarifa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilisema kuwa hafla hiyo itafanyika Kesho majira ya saa 9:00 alasiri.

Mapema leo bunge hilo lilimdhibitisha Dk Mpango kwa jumla ya kura 363 zilizopigwa na kufanya apate kura zote.

Spika wa Bunge Job Ndugai akitangaza kura hizo alisema jumla ya wabunge waliopiga kura ni 363 ambapo Dk Mpango alipata kura zote za ndio na hakuna kura hata moja iliyoaribika wala kumkataa hivyo amepata asilimia 100 ya kura zote.

Baada ya zoezi hilo Spika pia alisema kufuatia na Ibara ya 49 Makamu wa Rais kabla ya kushika madaraka yake ataapishwa na Jaji mkuu kiapo cha uadilifu na kiapo cha utendaji kazi wake.

 

Ndugai alisema, “Kabla Dk Mpango hajaondoka hapa nitoe taarifa ifuatayao katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 71 inaorodhesha mambo ambayo mbunge atakoma kuwa mbunge  ambayo ni iwapo atachaguliwa au kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais.

“Muda sio mrefu bunge limedhibitisha uteuzi wa Dk Mpango kuwa Makamu wa Rais, udhibitisho huu unamuondolea sifa Dk Mpango kuwa Mbunge wa Buhigwe, hivyo kwa mujibu wa Kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa sura ya 343 ninawajibika kuitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwamba kiti cha ubunge jimbo la Buhigwe sasa kipo wazi,” alisema Ndugai

Awali akizungumza mchakato wa kumdhibitisha Dk Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema “Mheshimiwa Spika, mapendekezo ambayo jina limeletwa kwako ambalo umelisoma na kwa maelekezo yote, linahitajika kuingia kwenye bunge lako zoezi ambalo limekamilika, kulitangaza zoezi limekamilika, hatua inayofuata ni jina hilo lipitishwa kwa asilimia 50.

 “Utaratibu uliotumika alipofariki Makamu wa Rais Omary Ali Juma ndio utumike ule ule,” alisema Majaliwa ambapo hoja hiyo iliungwa mkono na zoezi la kupiga kura likaanza ambapo Dk Mpango amedhibitishwa kwa asilimia 100.

Dk Mpango atakuwa Makamu wa 14 wa Rais tangu Tanzania ipate uhuru, na Makamu wa tano wa Rais baada ya uchaguzi mkuu wa vyama vingi wa 1995. 

 Kwenye hotuba yake ya kukubali wadhifa huo, Dk Mpango ambaye amekuwa Waziri wa Fedha kwa miaka mitano amesema, “kazi zote njema ni kazi za Mungu."

Aidha, Dk Mpango amesema alifadhaishwa na kifo cha Rais Dk John Magufuli na kuwa alilia mara kwa mara. Pia amesema anaamini jambo moja muhimu sana la kumtendea haki Hayati Dk Magufuli ni kuishi ndoto yake ya kuibadilisha Tanzania na kusimamia rasilimali za nchi.

“Tutoke sasa kuwa ‘lower-middle-income country’  (nchi ya uchumi wa chini- kati) twende kuwa ‘high income country’ (nchi ya uchumi wa juu) katika kipindi kifupi, inawezekana kwa pamoja tukiamua,” amesema wakati akiwaomba wabunge kumuidhinisha. 

 

IMEBORESHWA....

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro na Alfred Lukonge

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi