loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Mto huu usiwe chanzo  kuwanyima watoto elimu’  

WILAYA ya Nyasa mkoani Ruvuma iliyoanzishwa mwaka 2012 bado inasumbuliwa tatizo la miundombinu katika baadhi ya maeneo.

 

Wenyeji wanasema wilaya hiyo ambayo wakati inaanzishwa haikuwa na barabara yoyote ya lami kwamba miaka ya nyuma walikuwa wanasafiri kwa siku tatu hadi wiki ili kufika Mbinga na Songea mjini.

 

Pamoja na serikali, hususani ya awamu ya tano kufanya juhudi kubwa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, bado yapo maeneo ambayo wakazi wa Nyasa, hususani wa maeneo ya vijijini wanapata changamoto ya kutoka eneo moja kwenda jingine.

 

Hivi karibuni nilitembelea vijiji vya Liuli, Mkali A na Mkali B katika wilaya hii ya Nyasa na kugundua kwamba Mto Mbahwa umekuwa kikwazo bado, mintarafu suala zima la usafiri na usafirishaji katika wilaya hiyo.

 

Pengine wanaoteseka zaidi na uwepo wa mto huo huku kukiwa hakuna daraja ni wanafunzi wanaolazimika kukatisha kwenye mto huo kwenda shule.

 

Mto huo ambao umeelezwa kwamba umezidi kupanuka kutokana na mabadiliko ya tabianchi, unatishia usalama na uhakika wa elimu kwa watoto wa vijijini, hususani wanaosoma Shule ya Msingi Nambila na Mkali B.

 

Wakazi wa kata ya Liuli wanasema madaraja ya kuvuka mto huo yalisombwa na maji hivyo wananachi wanaokwenda kulima na wanafunzi hulazimika kuvuka mto huo kwa miguu, hali ambayo inahatarisha maisha yao.

 

Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nambila, Neema Kawonga, anasema kukosekana kwa daraja kunahatarisha maisha yao na mahudhurio kuwa hafifu.

 

Mwanafunzi huyo anasema wana moyo wa kusoma ila changamoto ya daraja inawakatisha tama, hivyo wanaiomba Serikali iwasaidie kujenga daraja hilo.

 

Mwanafunzi huo anakiri kwamba kutokana na kero hiyo, hasa kipindi cha mvua kama sasa wanashindwa kwenda shule kwa kushindwa kuvuka maji.

 

 

 

 

Mwalimu Mkuu wa Shule Nambila, Erasimus Haule, anasema kukosekana kwa daraja hilo kuna madhara kwa wanafunzi wanoishi upande wa mashambani.

 

Haule anasema wanafunzi wamekuwa wakikosa vipindi wakati wa masika, jambo ambalo anaamini linachangia kushusha ufaulu wao, hivyo anaomba serikali kuwajengea daraja hilo.

 

"Kukosekana kwa daraja kuna athari kubwa kwa wanafunzi wangu zaidi 150 wanaoishi upande wa mashambani. Naomba Serikali ifanyie kazi hii changamoto," anasema.

 

Naye John Nombo, Mkazi wa Kijiji cha Mkali B anasema ukosefu wa daraja katika eneo hilo siyo changamoto kwa watoto pekee bali hata kwa wananchi wengine.

 

Anasema wakati wa mvua za masika hata watu wazima wanashindwa kwenda mashambani na wamashambani wanashindwa kuja mjini.

 

 

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Nyasa, Boniphace Sangana, anasema chama kitahakikisha kadhia hiyo inapata ufumbuzi.

 

Anasema CCM inataka watu wapate elimu kwa uhuru na amani hivyo watahakikisha wanashirikiana na Serikali kutatua changamoto hiyo ya muda mrefu.

 

Anasema pia kadhia hiyo inawarudisha nyuma wanavijiji wanaojihusisha na kilimo kwani mvua zikinyesha wanashindwa kwenda shamba na kurudi majumbani.

 

Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Stella Manyanya, anasema changamoto hiyo ya miumbombinu anaijua na kwamba amekuwa akiiombea pesa mara kwa mara.

 

Anasema halmashauri imekuwa ikitafuta fedha za kujenga daraja katika eneo hilo ili kuondoa adha hiyo kwa wanafunzi na wananchi.

 

"Changamoto hiyo inajulikana na tumekuwa tukiiombea fedha kuanzia ngazi ya halmashauri na bungeni ila bajeti inayotolewa kwa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) ni ndogo," anasema.

 

 

Akizungumzia kadhia hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Isabela Chillumba anasema Serikali inatambua changamoto za miundombinu ya daraja katika vijiji vya Mkali, A, B na Liuli hivyo watajitahidi kurekebisha.

 

Chilumba anasema Serikali ya wilaya inaendelea kutafuta fedha kupitia vyanzo vyake mbalimbali ili kuhakikisha miundombinu yote inakuwa salama na kupitika muda wote.

WATU hutegemea mvua ili kufanikisha shughuli mbalimbali, ikiwamo ...

foto
Mwandishi: Suleiman Msuya

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi