loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

MAGUNOMICS Matokeo chanya uchumi wa Magufuli

JANA katika mfululizo wa makala haya tulimaliza kuangalia maeneo ambayo pesa zilizookolewa na uongozi wa Dk John Magufuli kupitia mapinduzi makubwa ya kiuchumi aliyoyafanya zilipelekwa, hususani kwenye sekta na miradi muhimu ya kimkakati. 

 

Baadhi ya sekta hizo ni afya, elimu (bure), ujenzi wa miundombinu (barabara, madaraja mtambuko, Kigongo-Busisi nk), mitambo ya umeme, ujenzi wa viwanda nk. 

 

Leo katika makala haya yanayoangalia sera za mageuzi ya kiuchumi zilizotekelezwa na Hayati Dk Joh Magufuli (JPM), tunaangalia matokeo ya sera hizi. 

 

Kumbuka katika makala haya tumeziita sera hizi ‘Magunomics’ kwa maana ya Magu (Magufuli) na nomics (economics) yaani uchumi uliotekelezwa na JPM. Kama ilivyoelezwa awali, lengo la "Magunomics" lilikuwa kujenga uchumi imara - uchumi wa viwanda.

 

Ilitazamiwa sera hizi ziweze kuifikisha Tanzaia kwenye Uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025; kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya Watanzania na kuiwezesha nchi kujitegemea na kutetea maslahi yake. 

Lakini kutokana na kasi ya Magufuli, nchi yetu iliingia kwenye uchumi wa kati kabla ya muda huo na kuishangaza dunia.

 

Mbali ya hilo kubwa, matokeo ya utekelezaji wa Magunomics yamekuwa makubwa na yajayo yanafurahisha na hasa kama serikali ambayo sasa inaongozwa na Rais wa Sita, Samia Suluhu Hassan itakayatekeleza:

 

 

 

Kukua kwa uchumi

 

Kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita uchumi wa Tanzania umeendelea kukua kwa wastani wa aslimia saba. Kiwango hicho kinaifanya Tanzania kuwa na uchumi unaokua kwa kasi miongoni mwa nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuia ya Kusini mwa Afrika (SADC). 

 

Aidha, Tanzania iliendelea kuwa miongoni mwa nchi tano katika bara la Afrika ambazo uchumi wake umekua kwa kasi katika nusu ya kwanza ya mwaka 2018, ikijumuisha: Ethiopia (asilimia 8.5), Ivory Coast (asilimia 7.4), Rwanda (asilimia 7.2), Tanzania (asilimia 7.0), na Senegal (asilimia 7.0). 

Pamoja na ukuaji huo ambao unatia moyo, bado uchumi uko chini ya kiwango kilichotarajiwa cha wastani wa asilimia 8-10 ili kutuwezesha kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa. 

 

 

Sekta zilizokua kwa kasi zaidi na hivyo kuchangia kiwango kikubwa kwenye ukuaji wa uchumi ni kwa takwimu za mwaka 2018: ujenzi (asilimia 15.7), uzalishaji viwandani (asilimia 12.0), habari na mawasiliano (asilimia 11.2), na uchukuzi na uhifadhi mizigo (asilimia 8.2). 

 

Kwa bahati mbaya sekta hizi hazina mchango mkubwa kwenye kuondoa umaskini kwa sababu: kwanza, zinatumia teknolojia ya mitambo au mashine zaidi hivyo, hazina uwezo wa kuajiri watu wengi; pili, shughuli zake zimejikita zaidi maeneo ya miji mikubwa na midogo; tatu, hazina uhusiano wa moja kwa moja na sekta ya kilimo, kwa maana ya kuwa soko la bidhaa za kilimo na kuzalisha pembejeo kwa ajili ya kilimo. 

Aidha, sekta ya kilimo ambayo inatoa mchango mkubwa kwenye pato la Taifa (asilimia 34.5) ilikua kwa asilimia 3.6 tu.

 

Mfumuko wa bei uliendelea kupungua kutoka wastani wa asilimia 4.3 mwaka 2017/18 hadi kufikia kiwango cha chini kabisa kuwahi kutokea katika miaka ya karibuni cha asilimia 3.0. Lengo la kipindi cha muda wa kati ni asilimia 5. Kati ya Julai hadi Novemba 2018, Tanzania ilikuwa na kiwango kidogo zaidi cha mfumuko wa bei ikilinganishwa na Uganda (asilimia 3.3) na Kenya (asilimia 4.8).

 

Sababu zilizochangia mfumuko wa bei kuwa chini ni pamoja na upatikanaji mzuri wa chakula katika masoko ya ndani na nchi jirani; kutengemaa kwa bei za mafuta katika soko la dunia; na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na za bajeti.

 

 

 

Kuboreka maisha ya Watanzania

 

Kwanza, kasi kubwa na endelevu ya ukuaji wa uchumi imepelekea kuimarika kwa hali ya maisha ya wananchi: wapo wananchi wengi ambao wamepata fursa za ajira (hivyo kuongeza kipato) katika shughuli za kiuchumi ambazo zimetekelezwa na serikali ya Awamu ya Tano. 

 

Ajira zimetokea kwenye ujenzi wa miradi mingi kama ya reli ya kisasa, bwawa la umeme, madaraja mtambuko, upanuzi wa bandari, ujenzi wa meli, ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, uanzishwaji wa viwanda (zaidiya viwada 8,000) na kadhalika.

 

Pia kumekuwa na kuongezeka kwa ujenzi wa nyumba bora za kuishi, umiliki wa mali zisizohamishika na vyombo vya usafiri, na vifaa vya kudumu vya majumbani (consumer durables) vinaashiria kuimarika kwa hali ya maisha ya wananchi. 

 

Vilevile, kuimarika kwa miundombinu ya barabara na mawasiliano kumerahisisha muingiliano wa watu na usafirishaji wa bidhaa, hivyo kuimarisha biashara na shughuli nyingine za kijamii. 

 

Hata hivyo, ukuaji wa uchumi ambao ungekuwa na manufaa zaidi kwa nchi husika ni ule unaochangia moja kwa moja katika kuboresha maisha ya watu wengi maskini. Hii ina maana kwamba, watu maskini washirikishwe kwenye sekta zinazokua kwa kasi. 

Maana yake ni kwamba, mahusiano kati ya ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya watu wengi maskini ungekuwa kama mahusiano kati ya amira na mkate, kwa maana kwamba amira ni sehemu ya mkate na ndiyo inayotengeneza au inayofanya mkate ukue - bila amira unapata ugali wa ngano - badala ya mahusiano kati ya siagi na mkate, ambayo siagi haina mahusiano yoyote na utengenezaji wa mkate - siagi inapakwa kwenye mkate baada ya kutengenezwa. Maana yake ni kwamba wananchi maskini washirikishwe kukuza uchumi!

 

 

 

Sekta pekee ambayo inaweza kuwa amira kwenye ukuaji wa uchumi ni kilimo! Kwa kuwa kilimo ndicho kinaajiri watu wengi maskini, ni dhahiri kitakapokua kwa kasi kitawanufaisha maskini wengi. 

 

Kuwe na mkakati wa makusudi kuhakikisha kilimo kinachowahusisha wakulima wadogo ndicho kinachokua kwa kasi ya aslimia 10 na zaidi. Maana yake ni kwamba, kilimo ndicho kinatakiwa kupewa kipaumble cha kwanza! 

 

Kipaumbele kitajidhihirisha kwa kupewa ruzuku, kuondoa kodi zisizo rafiki, kuongeza kiwango cha bajeti kinachotengwa, kuboresha uzalishaji na bei za mazao ya kilimo (mazao ya kimkakati: korosho, pamba, tumbaku, katani, chai, kahawa, na mazao ya chakula), upatikanaji wa mikopo ya kilimo, kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi na ubora na uwingi wa miundombinu inayounganisha maeneo ya kilimo na masoko ya ndani na nje.

 

 

 

Pili, ukuaji mzuri wa uchumi umeiwezesha Serikali kuongeza ukusanyaji wa mapato na kugharamia uboreshaji wa huduma za jamii hususani elimu (ikwemo elimu ya msingi na sekondari bila ada), afya (hospitali, vituo vya afya, zahanati, madawa, vifaa-tiba, vitendanishi), maji na kuimarisha uzalishaji wa umeme na kuusambaza vijijini. 

 

Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa ukosefu wa huduma hizi umekuwa chanzo cha umaskini. Kwa hiyo, upatikanaji wa huduma hizi bure au kwa gharama nafuu au kwa urahisi, zimewezesha wananchi kuwekeza rasilimali (fedha na muda) walizokuwa wanatumia kupata huduma hizo kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo ambazo zinawapatia kipato.

 

 

 

Tatu, mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 6.8 mwaka 2015 hadi asilimia 3.0 mwaka 2018. Kutokana na kupungua kwa mfumuko wa bei, uwezo wa shilingi kununua vitu umeendelea kuwa imara. Aidha, gharama za maisha kwa mwananchi kwa ujumla, hazijabadilika sana. Kwa hiyo, hali ya maisha ya wananchi ama imebakia vilevile au imeboreka kidogo. 

 

Nne, kuwatetea wanyonge (hasa wafanyabiashara wadogo) kwa kuwejengea mazingira mazuri ya kuendesha shughuli zao za maisha. Hali hii imeamsha ari ya kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa sasa wanafanya kazi bila hofu na hivyo kuongeza uazalishaji na kipato. Kwa mantiki hiyo, maisha yao yameboreka kuliko wakati uliopita.

 

Itaendelea

 

Mwandishi wa makala haya ni mchumi na mshauri binafsi wa masuala ya uchumi, hususani katika eneo la diplomasia ya uchumi.

 

WATU hutegemea mvua ili kufanikisha shughuli mbalimbali, ikiwamo ...

foto
Mwandishi: Profesa Kitojo Wetengere

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi