loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM alivyowaachia Ubungo  zawadi ya shule ya King’ongo

WAZAZI, walimu, wanafunzi na wote wanaohusiana na Shule ya Msingi King’ongo ilioko Kata ya Saranga, Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam ni moja ya makundi ambayo hayatamsahau aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli.

Hii inatokana na namna alivyowaachia zawadi kubwa ya kubadilisha hali ya shule hiyo iliyokuwa mbaya sana hadi kuwa mithili ya shule ya kimataifa. Matarajio yao ilikuwa ni kwenda kuizundua siku moja lakini amekufa kabla ya kutimiza hilo.

Ilikuwa Januari 18 mwaka huu pale Rais Magufuli, akiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Sekondari ya Ihungo mkoani Kagera alipoeleza kusikitishwa na video aliyoona ikionesha mazingira mabovu na yasiyoridhisha ya shule hiyo.

Huku akifanya kazi chini ya kauli mbiu yake ya “Hapa Kazi Tu” hakuchelewa kutoa maagizo akitaka mazingira ya shule hiyo yarekebishwe mara moja.

Alikemea kitendo cha kuwepo kwa shule yenye mazingira mabovu kama hiyo huku akiweka msisitizo kwa watendaji na wasaidizi wake wa mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha kabla hajarejea Dar akute hali imebadilika katika shule hiyo.

Kauli yake hiyo ilisababisha viongozi wa mkoa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge kwenda shuleni hapo na kuanza mara moja mchakato wa ujenzi wa madarasa mapya.

Kazi hiyo ilianza rasmi siku iliyofuata baada ya maagizo ya Rais. Mchanga na kokoto vilifikishwa kwenye eneo la shule hiyo, mafundi walifika siku hiyo hiyo na kazi kuanza kwa mwendo wa haraka.

Siku 21 zilitosha kufanyiwa kazi kwa agizo hilo ambalo zilimalizika kwa wanafunzi waliokuwa wakisoma kwenye mazingira magumu kushuhudia wakianza kusomea kwenye madarasa mazuri.

Hali ilikuwaje

Shule ilikuwa na madarasa yasiyotosheleza idadi ya wanafunzi huku pia yakiwa katika hali mbaya kwa maana ya ubovu.

Madarasa hayo yalikuwa na nyufa kadhaa huku matundu ya vyoo shuleni hapo yakiwa pia mabaya. Ilikuwa si rahisi mtu kuamini kwamba shule hiyo iko katika Jiji mashuhuri na la kibiashara la Dar es Salaam.

Kutokana na uchache pamoja na ubovu wa madarasa wanafunzi wengine walilazimika kusomea chini ya miti huku wakisumbuliwa na vumbi na pale mvua ilipokuwa ikinyesha ilikuwa ni mtafutano baina ya wanafunzi na walimu wao.

Hali ilivyo sasa

Kutokana na agizo la Hayati Magufuli madarasa mapya tisa yamejengwa shuleni hapo, tena yakiwa katika hadhi nzuri.

Sakafu za madarasa hayo mapya ni za marumaru, kuta zimepigwa rangi nyeupe huku nje zikiwa na rangi ya bluu na nyeupe pia.

Madarasa saba kati ya hayo tisa yamewekwa kwenye mstari mmoja ulionyooka na kupendeza.

Ni madarasa makubwa, yakiwa na madirisha makubwa pia, hivyo kila mwanafunzi anaweza kusoma kwa amani huku akipata hewa nzuri.

Mbali na madarasa matundu 12 ya vyoo yameongezwa, sita yakiwa ya wasichana na mengine sita ya wavulana.

Madarasa ya zamani yamevunjwa na sasa  eneo hilo limeachwa wazi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mengine baadaye.

Shule ya Msingi King’ongo ina wanafunzi 2,500. Kabla ya ujenzi huo ilikuwa na madarasa manne tu huku mawili kati ya hayo yakiwa na nyufa kubwa za kutisha, hivyo kusababisha hofu kwa wanafunzi na walimu, ndipo kukafanywa uamuzi wa kuanza kusomea nje, chini ya mti.

 

Wananchi wanavyosema

 

Mkazi wa Kata ya Saranga, Beatrice Manusi anasema yeye na wakazi wenzake wa kata hiyo wameguswa sana na kifo cha Rais Magufuli kwani, pamoja na mengi aliyofanya kwa ajili ya Watanzania wote, wao wameshuhudia namna alivyookoa shule ya kata yao.

 

Anasema wakati wananchi wakimsifia kwa mambo mbalimbali, Saranga wanamkumbuka sana kwa jinsi alivyoagiza ujenzi wa shule hiyo na sasa watoto wao wanaosomea mahala pazuri na salama.

 

Anasema kuwa agizo lake limekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi, walimu na wazazi. Anafafanua kwamba baadhi ya wazazi walilazimika kutafuta shule binafsi ili kuwapeleka watoto wao.

 

Anasema, Rais Magufuli atakumbukwa sana shuleni hapo na kata nzima ya Sarangi kwa uamuzi wake wa kuijenga upya shule hiyo.

 

“Hakika tulikuwa kwenye hali ngumu. Watoto walikuwa wakisoma kama sijui wapo wapi. Huwezi kuamini kwamba shule hiyo ilikuwa katika jiji la Dar es Salaam.

 

“Lakini tangu ujenzi wa shule yetu ukamilike kutokana na kauli ya Rais Magufuli, wanafunzi wanasomea katika mazingira mazuri hata wale waliofikiria kuhamisha watoto wao hawana tena wazo hilo na wale waliokuwa tayari wamewahamisha wanatamani kuwarudisha,” anasema.

 

Mwanafunzi wa darasa la sita shuleni hapo, Anita Prosper, anasema kuwa amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Magufuli na kwamba walikuwa wakimngojea kwa hamu siku ambayo angeenda kuizindua shule yao.

 

“Tuliamini kwamba ipo siku atakuja kuizindua shule hii kwa kuwa yeye ndiye alitoa agizo la kujengwa kwa madarasa mapya, na leo tunasoma kwa amani kabisa. Tumesikitishwa sana na kifo chake,” anasema Anita.

 

 

Walimu wa Shule ya Msingi King’ong’o walisema protakali haiwaruhusu kuzungumza bila ruhusu ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ubungo, lakini wakadokeza kwamba wameumia sana na kifo cha Magufuli. 

 

Hata hivyo walishukuru kwa kuwaachia zawadi ambayo haitasahaulika maishani mwao.

 

Afisa Habari wa Wilaya ya Ubungo, Joina Nzali, anabainisha kuwa shule hiyo imepunguza shida ya wanafunzi kusoma chini ya miti na katika mazingira yasiyoridhisha.

 

Anasema shule pia ilikuwa na uhaba wa madawati lakini kwa sasa madawati yamewekwa madarasa yote na hilo anakiri kwamba limechagizwa na nia ya dhati aliyokuwa nayo Hayati Magufuli kwa shule hiyo na sekta ya elimu kwa ujumla.

 

 

Uongozi wa Hayati Magufuli alijilekeza, pamoja nambo mengine, kwenye maboresho ya sekta za hudma kama afya na elimu, hivyo kifo chake kimewaumiza wengi walioguswa na hatua ambazo serikali yake ilichukua katika kuboresha sekta hizo muhimu.

 

Mwanzilishi wa Shirika linalosaidia vijana kuunganisha nadharia na vitendo katika kutafuta ajira (TEDI), Gloria Anderson anasema kuwa Magufuli ameaga dunia wakati wadau wa elimu wakiwa bado wanamhitaji sana hasa kwenye maboresho ya sekta hiyo.

 

“Kama aliweza kutoa kauli moja tu iliyobadilisha hali ya Shule ya Msingi King’ong’o, bado taifa lilikuwa likimhitaji sana katika mambo mengi,” anasema.

 

Hata hivyo, Gloria anaamini kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa msaidizi wake wa karibu na sasa ameshika hatamu za uongozi atakwenda kutenda makubwa zaidi.

 

Anaamini kwamba, kama kulikuwa na mapungufu yoyote kwa Magufuli kama mwanadamu, Samia atakwenda kurekebisha na hivyo anaweza kufanya mazuri na makubwa zaidi kama ambavyo Magufuli aliboresha yale yaliyopungua kwa marais waliomtangulia. 

WATU hutegemea mvua ili kufanikisha shughuli mbalimbali, ikiwamo ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi