loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wamakua; kutoka Madagascar hadi Tanzania

WAMAKUA (pia huandikwa Wamakhuwa) ni kabila lenye idadi kubwa ya watu wanaoishi Mkoa wa Mtwara, Wilaya za Masasi na Nanyumbu. Hili ni moja kati ya makabila zaidi ya 120 yanayopatikana Tanzania. 

Wamakua ni miongoni mwa makabila ya kibantu. Kabila hili kiuhalisia lina lugha aina mbalimbali za Kimakua, lakini lugha ya Kimakua inayozungumzwa Tanzania ni Kimakhuwa-Meetto.

Wamakuwa ni kabila lililosambaa mikoa ya kusini mwa Tanzania, ya Mtwara, Lindi na Ruvuma, lakini pia kabila hili lipo nchi ya jirani ya Msumbiji upande wa Kaskazini.

Hili ni jambo la kawaida kwa makabila yote yaliyopo maeneo ya mipakani kwa vile wakati wakoloni wanagawa mipaka hawakuzingatia makabila, bali walizingatia urahisi wa mpaka kuonekana wakitumia vitu kama vile mito, milima, mabonde, maziwa, misitu, majangwa na kadhalika! 

Hivyo sababu hizo zimekuwa chanzo cha kutenganisha kabila moja kuishi katika nchi mbili; au kutokana na sababu hizo zimeufanya ukoo mmoja uishi katika nchi mbili tofauti; au kulingana na sababu hizo hizo zimewafanya ndugu wa damu kuishi nchi mbili tofauti na hata kushindwa kutembeleana wakati mwingine kulingana na taratibu za viza na mengineyo!

Historia ya Wamakua

Inaelezwa kuwa jamii ya Wamakua ilihamia nchini Tanganyika kutoka Msumbiji. Baadhi ya wanahistoria wanadai kuwa hata hapo Msumbiji, Wamakua walifika tu kwani inasemekana walipata kuishi maeneo ya Madagascar miaka mingi sana hata kabla ya mwaka 1700. 

Na hata neno lenyewe la ‘Madagaska’ na ‘Antananarivo’ ni majina yenye uhusiano mkubwa sana na kabila la Wamakua. Kimsingi Wamakua wana historia ndefu sana hapa Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Inasimuliwa kuwa kabla ya kufika hapa Tanganyika (sasa Tanzania) maeneo ya Masasi, walikuwa wanaishi maeneo ya Msumbiji hasa Msumbiji ya Magharibi. Walipofika Masasi hawakukuta nchi ikiwa pori ingawa waliwakuta Wandonde wakiishi hapo. Wandonde ndio wakazi asili wa Wilaya ya Masasi.

Inasimuliwa kuwa, kutoka huko Msumbiji hawakuhama kwa mara moja, walihama kwa makundi makundi na kwa nyakati tofauti tofauti. Sababu za kuhama huko zilikuwa nyingi na kila kundi lilikuwa na sababu zake za kuja Tanganyika.

Kwa mfano, sababu ya kwanza ni biashara ya utumwa iliyoanzishwa na Wafaransa kutokana na kilimo cha miwa huko visiwani Mauritius. Wafanyabishara wa Kiarabu walikuwa wanashirikiana na Wamakua kuwakamata majirani zao Wayao na kuwafanya watumwa. 

Inasemwa kuwa kwa miaka yote hiyo ya biashara ya utumwa, Wayao na Wamakua walikuwa hawapatani kabisa. Lakini urafiki ulikuwa mkubwa sana kati ya Waarabu na Wamakua. 

Baadaye urafiki huo ukafa na badala yake ukazuka urafiki kati ya Waarabu na Wayao. Kwa kuwa Wamakua waliwasababishia balaa kubwa dhidi ya Wayao kwenye biashara ya utumwa, wakaona haina haja ya kubaki hapo, ndipo walipoondoka na kuja Tanganyika.

Sababu nyingine ni ujio wa kabila la Wangoni waliokuwa na hasira ya kutafuta ardhi kwa ajili ya kuishi. Inasemwa kwamba Wamakuwa ni moja ya makabila ya watu wapole sana, hivyo si watu wa kupenda vita. 

Sasa wakati Wangoni wanafika maeneo ambayo Wamakuwa waliishi, walitaka kuanzisha vita lakini Wamakua waliamua kuondoka maeneo hayo na kuja Tanganyika maeneo ya Masasi.

Sababu nyingine ni masuala ya mabadiliko ya kimazingira, kwani maeneo waliyoishi ni maeneo yenye maziwa na mapori makubwa  yenye wanyama wakali. Hivyo kuna kipindi walikuwa wanashambuliwa na wanyama wakali kama simba waliosababisha maafa makubwa. Kwa ujumla kila kundi lilikuwa na sababu zake za kuhama maeneo hayo. 

Asili ya jina la Wamakua pia lina historia yake, ila kwa mujibu wa mwanahistoria Yusuf Halimoja, anafafanua kuwa jina la Wamakua linahusiana sana na mazingira yao, na maana ya Wamakua ni watu wanaioshi karibu na ziwa. 

Neno “kua” lina maana ya ziwa, na hivyo Wamakua ikiwa na maana ya watu waliokuwa wanaishi karibu na ziwa. Kama ilivyoelezwa kuwa Wamakua huko Msumbiji walipatikana upande wa Magharibi yaani Mashariki mwa Ziwa Nyasa.

Katika kabila hili, kuna koo maaraufu kama Amoro, Amkuvako, Achikatambo, Amiranshi na Arope. Kiutamaduni, kabila la Wamakua bado wanaendeleza tamaduni zao hasa zile zilizo nzuri kwa jamii.

Suala la imani

Jamii hii ilikusanyika chini ya mti ujulikanao kama ‘Msoro’ na si mahali pengine popote. Eneo la mti huo lilitakiwa kuwa safi muda wote na lilitumika kuomba amani.

Tunaelezwa kuwa kila siku asubuhi Wamakua walikusanyika chini ya mti wa msoro ili kumuomba Mungu kwa kuwalinda usiku mzima, huku pia wakiomba sala ya ulinzi wa siku mpya, na baada ya tukio hilo walielekea kwenye mihangaiko yao ya siku.

Wakati jua linapozama jamii hii ilikusanyika kwenye mti huo ili kumshukuru Mungu kwa kuwalinda kutwa nzima na kisha kumuomba tena ulinzi wa usiku na kwamba tukio hilo lilihusisha watu wazima tu.

Hata hivyo, pamoja na mambo mengine kulikuwa na sadaka iliyotolewa ili kumshukuru Mungu, hasa kabla ya msimu wa kupanda na kuvuna. Lakini pia walimtolea Mungu sadaka hasa pale panapotokea ugonjwa, sambamba na kunapotokea kipindi cha ukame.

Jamii ya Wamakua pia walikuwa na utamaduni wa kuzuru kwenye kaburi na baada ya kufika hapo huanza kuita jina la (Mluki kimila) wakiwa na maana ya Mungu. Jina ambalo hulitukuza, kitendo hicho hufanyika ili kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu.

Kwa kufanya hivyo Wamakua waliamini kuwa Mungu alisikia kilio chao na kwamba, ilikuwa rahisi kuwasikiliza matatizo yao kutokana na yeye kuwa muumba pekee ambaye angeweza kutatua changamoto zao.

Na kwa kuwa aliwamba hakuwa na sababu ya kuwaona wakipata mateso na shida za maisha pasi kuwasikiliza kilio na shida zao.

Jambo kubwa kwao lilikuwa kudumisha amani na upendo hasa kwa kuabudu Mungu ambaye walikuwa hawamuoni, kwani inadaiwa kuwa kabla ya kuwasili kwa Waarabu na Wazungu, jamii hii ya Wamakua walikuwa wapagani na hawakujua kabisa juu ya uwepo wa Mungu.

Tohara

Kwenye kabila hili jambo la kufanyiwa tohara ni kitu cha lazima, pale kijana wa kiume anapotimiza miaka 12, ni lazima wazazi wake wahakikishe kuwa wanaandaa mkakati wa kijana wao kufanyiwa tohara.

Chifu mdogo ajulikanaye kama ‘Mwene’ lazima afike kwa wazazi wa mtoto ili kupanga ni namna gani na siku gani mtoto huyo atafanyiwa sherehe mara baada ya kufanyiwa tohara. Ambapo kwenye hilo huandaliwa wanaumme wawili huku mzazi mmoja akitakiwa kushuhudia zoezi hilo.

Baada ya mipango yote kuandaliwa na kukamilika, siku ya siku inapowadia wazazi hujenga nyumba ndogo ya kupumzikia kijana anayefanyiwa tohara.

Baada ya zoezi hilo kukamilika wazazi huandaa sherehe ya ngoma inayowahusisha ndugu, jamaa na marafiki wa karibu wakiwemo majirani ili kufurahia kitendo cha mtoto wao, ngoma hiyo huchezwa usiku.

Ngoma ya Wamakua inayowahusisha wazee

Editha Ndimbo mkazi wa Kunduchi Mtongani jijini Dar es Salaam anasema: “Unajua watu wengi hufikiri kuwa watu wazee hawawezi kucheza; hiyo si kweli kabisa kwa sababu kwetu sisi, ngoma huchezwa zaidi na watu wazee wa umri kati ya miaka 50-55.

“Si kwamba vijana hawapo, la.  Ila tu ni kwa sababu wazee ndio wanaojua kila aina ya ngoma inayochezwa na inachezwa kwa wakati gani,” anasema.

Editha anasema mara chache ngoma hii huchezwa na vijana endapo tu wazee hao wana shughuli zingine za kufanya zilizowalazimisha kushindwa kuishiriki kwa kipindi kinachotakiwa. Shughuli hizo muhimu mara nyingi huwa kama zile za kilimo hasa wakati wa palizi za mazao au wakati wa kuvuna.

Pia ngoma hiyo wachezaji wake huvalia kanga kwa ndani pamoja na kaniki ambayo huvaliwa sehemu za kiunoni pamoja na shanga ambazo huvaliwa shingoni na kichwani.

Wakati wa ngoma huwa ndiyo muda mzuri kwa wazee kukutana na wazee wenzao na kuzungumzia mambo mbalimbali yanayowahusu na pia kujadili yanayopaswa kufanyika pindi wanapomaliza kucheza ngoma.

Inapotokea mmoja kati yao akawa na sherehe au shughuli muhimu kama hiyo katika siku ambayo imepangwa, huwafahamisha wenzake kwa kuwa ndiyo wakati muafaka wa kufahamishana mambo umuhimu kama hayo ya kifamilia.

Editha anasema kuwa ngoma hii haina kipindi maalumu kwani wakati wowote mtu akiihitaji, huwafahamisha watu ili mradi tu, awe na chakula pamoja na vinywaji asilia.

Familia yoyote ambayo haina mtu anayewahusu katika wachezaji hao hulazimika kulipia gharama za fedha ambayo hutumika kwa ajili ya kununulia ngoma pamoja na shanga.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

WATU hutegemea mvua ili kufanikisha shughuli mbalimbali, ikiwamo ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi