loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

MAGUNOMICS Uchumi ulojengwa na JPM  na dhana na kujitegemea

JANA katika mfululizo wa makala haya tuliangalia matokeo chanya yaliyosababishwa na sera za uchumi za Hayati Dk John Magufuli  (JPM) ambazo tumeziita ‘Magunomics’ kwa maana ya Magu (Magufuli) na nomics (economics). Kama ilivyoelezwa awali, lengo la "Magunomics" lilikuwa kujenga uchumi imara - uchumi wa viwanda.

Leo tunaangalia dhana na Tanzania kujitegemea ambayo Magufuli aliiweka mbele sana kiasi cha hata kugoma kusaini mkataba wa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EPA) kwa kuwa ulilenga kuua viwanda vyetu. 

Kujitegemea

Ukuaji mzuri wa uchumi na ongezeko kubwa la ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwezi viliiwezesha serikali kugharimia sehemu kubwa ya matumizi yake. 

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania tulishuhudia takribani asilimia 35 - 40 ya bajeti ikielekezwa kwenye miradi ya kimkakati. Sehemu kubwa ya bajeti ya iliyotengwa kutekeleza miradi hiyo ilitokana na pesa za mapato ya makusanyo ya ndani. 

Kwa mfano, sehemu kubwa za fedha kutekeleza miradi kama ununuzi wa ndege, ujenzi wa reli ya kisasa sehemu ya awali, upanuzi wa barabara ya Ubungo-Chalinze na ujenzi wa meli Ziwa Victoria vimegharimiwa na fedha za ndani. 

Haya ni mafanikio makubwa na muhimu ambayo mara nyingi hayatajwi. Mafanikio haya yanaifanya nchi ijitegemee, hivyo, kupunguza utegemezi wa misaada yenye masharti na ya kinyonyaji kutoka kwa wahisani. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema 'nchi haiwezi kuwa na uhuru kamili kama inategemea misaada na mikopo kwa ajili ya maendeleo yake'.

Wanazuoni wengi wanaamini kwamba Taifa ambalo halijajitegemea kimapato, hasa mapao ya ndani, bado lipo chini ya utumwa na halijapata uhuru kamili. 

Maana yake ni kwamba usipoweza kujitegemea mataifa ya nchi yatajitolea kukusaidia lakini kwa lengo la kutimiza maslahi yao. Wataingilia mambo yako ya ndani na kukuagiza nini cha kufanya. Kwa kuwa nchi yako ni tegemezi hakutakuwa na uchaguzi zaidi ya kukubali kila utakachoagizwa. 

Wakati fulani nilishangazwa na maamuzi ya Bunge la nchi moja ya Ulaya kuiagiza nchi huru ya Tanzania kusitisha mpango wake wa kujenga umeme unaozalishwa kwa maji wa Nyerere. Pengine ni vema tukarejea maneno ya aliyekuwa Waziri mkuu wa Uingereza, David Cameroon kuyakumbusha mataifa ya Ulaya kwamba "Afrika (Tanzania) ni bara (nchi) muhimu katika uchumi wa dunia, lakini mataifa mengi yaliyoendelea yanajisahau kwamba bara (nchi) hilo liko huru". 

Kutetea maslahi yetu

Kwa kawaida kila nchi ina malengo ya kutimiza maslahi fulani. Hata hivyo, mara nyingi nchi moja inalazimika kushirikiana na nchi nyingine ili kutimiza maslahi yake. Katika kufanya hivyo, Nchi za Ulimwengu wa Tatu zinatumiwa na mataifa ya Magharibi kutimiza maslahi yao. 

Dk Magufuli alionyesha kwamba njia moja wapo itakayotuwezesha sisi kama nchi kutimiza maslahi yetu bila woga ni kuongeza uwezo wetu wa kutekeleza mipango yetu kwa kutumia fedha zetu za ndani. Hakuna nchi maskini ambayo inaweza kusema HAPANA au kutetea maslahi yake huku ikiwa ombaomba!

Katika kutekeleza Magunomics serikali ilikabiliwa na changamoto nyingi za kutetea maslahi yetu. Tulipowaomba wafadhili fedha za kujenga reli ya kisasa, kupanua barabara ya Ubungo-Chalinze na mradi wa Bwawa la Nyerere tulipewa masharti ambayo hayakuwa rafiki - takayakataa. 

Tulikuwa na jeuri ya kukataa kwa sababu tulikuwa na fedha zetu kutoka makusanyo ya ndani. Pia, tulipokataa kukumbatia ushoga, aina ya demokrasia ya Ulaya na haki za binadamu, wahisani walitishia kutunyima misaada! 

Nakumbuka pia tulipokataa kuendelea kuwa dampo la nguo na viatu vya mitumba tulitishiwa kunyimwa misaada. Kama hiyo haitoshi kiongozi mmoja wa taifa moja kubwa duniani alisema "misaada ya maendeleo itatolewa kwa nchi za kiafrika ambazo zitaonyesha kuunga mkono ushoga"!

Changamoto za Magunomics

Ni dhahiri kwamba kila jambo jema linalotendwa halikosi changamoto zake. Pamoja na mazuri mengi ambayo serikali ya Magufuli ilifanya, kuna changamoto tano ambazo zimekuwa zikitajwa mara kwa mara. Sehemu hii inajibu hoja hizo kwa kuuliza maswali ambayo kila Mtanzania anapaswa kuyajibu kwa ufasaha ili kujua ukweli wa hoja hizo: 

Ugumu wa maisha/vyuma vimekaza

Je, kabla ya mageuzi yaliyoletwa na Magufuli nilikuwa naishi maisha ya kipato changu halali? Baada ya mageuzi nani wanaolalamika kwamba "maisha ni magumu" (mafisadi, waporaji wa rasilimali za nchi, wanasiasa, viongozi wa dini, wafanyakazi wa serikali, wafanyabiashara au wakulima)?

Jiulize tena. Je, ni kweli kwamba maisha yamekuwa magumu kwa sababu ya ujio wa Serikali ya Awamu ya Tano au tunaimba wimbo wa "maisha magumu" au "vyuma vimekaza" kama kibwagizo?

Kwa kila anayelalamika anaweza kueleza waziwazi serikali ya Awamu ya Tano ilimpunguzia nini halali ambacho kimefanya maisha yake yawe magumu na kama mimi na wewe tulikuwa tunanufaika na maovu yaliyokuwa yanatendeka kwa njia moja au nyingine. Kama ndivyo, ni halali kweli serikali iachie maovu hayo yaendelee kwa sababu tunalalamika kwamba maisha yamekuwa magumu?

Kumbuka, Tanzania ilikuwa inaumwa kansa kwa muda mrefu na ili ipone ilihitaji dozi kamili! Ukisikia mgonjwa wa kansa analia kwa uchungu, nywele zinanyonyoka na ngozi inababuka, ujue mionzi imeingia na inafanya kazi. 

Vivyo hivyo, ukisikia kelele za "maisha magumu au vyuma vimekaza" jua kwamba Magunomics inaingia na inafanya kazi. Wewe ambaye huumwi kansa, Magunomics au wimbo wa "maisha magumu au vyuma vimekaza" unakuhusu nini? Usikubali kutumiwa!

Wachumi wanaamini kwamba nchi aliyoiacha hayati Magufuli  iko kwenye kipindi cha mpito tu ambacho nchi haina budi kukipitia. Utekelezaji wa mageuzi ya kututoa hapa tulipo kuelekea kwenye Uchumi wa juu wa Kati, lazima uumize wengi na pengine uchumi kutikisika kwa kitambo kidogo.  

Tukiwa katika kipindi hiki cha mpito tukumbuke maneno ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere: “Taifa lisilokubali kutaabika kwa maendeleo yake lenyewe bila shaka taifa hilo litataabika kwa maendeleo ya mataifa mengine. Maendeleo ni mtoto wa taabu.”

Kuminywa kwa demokrasia

Kwa kuwa demokrasia inatofautiana kati ya nchi na nchi, ipi ni tafsiri ya demokrasia kwa mazingira ya Tanzania (China wana demokrasia yao, Urusi wana demokrasia yao, Rwanda wana demokrasia yao na Marekani wana demokrasia yao).

Je, demokrasia ni uhuru usio na mipaka (maandamano, matusi, kejeli, fitina, kupigana vijembe, kupinga kila kitu, kukosa uzalendo, kuruhusu ndoa za jinsi moja)?  Kwa kuwa mimi na wewe ni viongozi wa taasisi mbalimbali (taasisi za siasa, dini, mashirika ya serikali na yasiyo ya kiserikali na kaya), wapi tunaweza kujifunza utekelezaji wa aina ya demokrasia tunayoitaka? Yaani tuwe mfano wa kile tunachotaka!

Tunajifunza wapi ambapo waliendekeza demokrasia katika hatua za awali kabisa za maendeleo na katikati ya umaskini tulionao wakafanikiwa? Na Katika hatua ya awali ya maendeleo na umaskini tulionao - Watanzania wanataka nini: maendeleo au hii inayoitwa demokrasia kwa mtazamo wa magharibi au vyote kwa pamoja?

Madai ya kukiuka sheria

Je, ni kweli utawala chini ya Rais Magufuli haukufuata sheria? Kama ni kweli kwa nini ulifanya hivyo? Na Katika hali ya utendaji "holela" uliyokuwepo, ni njia gani bora ya utawala ingetumika?

Matukio ya uvunjifu wa amani

Nani wahusika wa matukio hayo? Tunao ushahidi wa kuthibisha tunayosema?

Katiba ya Wananchi

Kwa kuwa kila jambo lina wakati wake, Je, wakati huu ambapo Dk Magufuli ameiacha nchi ikiwa kwenye mageuzi makubwa ni wakati mwafaka wa kutengeneza katiba mpya?

Serikali na wafanyabiashara

Je, ni kweli kwamba kuna uhusiano mbaya kati ya serikali na wafanya biashara? Nani anasababisha au alisababisha uhusiano huo mabaya? Au nani wa kulaumiwa?

Hitimisho

Kwa miaka michache ya utawala wa Dk John Magufuli dunia ilishuhudia mafanikio makubwa ambayo hayajawahi kutokea katika historia ya Tanzania. Ni vema Watanzania tukatambua mafanikio hayo na tukaendelea kuunga mkono juhudi hizo na zitakazofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza wajibu wetu.

Tufanye kazi kwa bidii, tuipende nchi na bidhaa zake, tuwatie moyo viongozi wetu, tufichue uovu wa kila aina na kulipa kodi ili kuiwezesha Serikali kugharamia miradi ya maendeleo na kupata mafanikio zaidi. Tukifanya hivyo tutakuwa tumetimiza ule msemo "kiongozi mzuri ni yule aliyezungukwa na watu wazuri". 

Hata hivyo, katikati ya mafanikio hayo tumejitengenezea maadui wengi ndani na nje ya nchi. Wengi wa maadui hao ni wanufaika wa rushwa na ufisadi na wahujumu uchumi ambao wanapambana kuendeleza himaya zao ambazo zimebomolewa. Nawasihi Watanzania wenzangu tusikubali kutumiwa na maadui katika vita hii.

MUNGU IBARIKI TANZANIA

WATU hutegemea mvua ili kufanikisha shughuli mbalimbali, ikiwamo ...

foto
Mwandishi: Profesa Kitojo Wetengere

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi