loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Samia awageukia wasaka urais, TRA

RAIS Samia Suluhu Hassan ameonya wenye nia ya kutaka kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kuacha mara moja huku akiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuacha tabia ya kutumia nguvu dhidi ya wafanyabiashara hali inayowafanya wakimbie nchi.

“Nafahamu mwaka 2025 upo karibu, kawaida yetu kama Watanzania au wote ulimwenguni, kipindi cha pili, mnakuwa na hili na lile, acheni. Kila mwenye nia ya 2025 aache mara moja,” alisema Rais Samia.

Akizungumza baada ya kumwapisha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga na mawaziri wanane na naibu mawaziri wanane katika Ikulu ya Chamwino mkoani hapa jana, Rais Samia aliwataka waende wakafanye kazi mambo ya mbele yatajulikana baadaye.

“Trend (mwenendo) wa sasa ni kuua walipa kodi, wafanyabiashara, mnatumia nguvu zaidi kuliko kutumia akili na maarifa, wale mnaowakamua, kuchukua vifaa vyao, kufungia akaunti zao na kisha kukiuka sheria ya mapato anafunga biashara anahamia nchi nyingine, mnapunguza walipa kodi, “Mnauwa wafan-yabiashara, nendeni mkatengeneze na kutanua uwigo wa walipakodi, yale mengine yanawapunguzia watu ari ya kulipa kodi. Waziri (Dk Mwigulu Nchemba) naomba ukayasimamie,” aliagiza.

Alimtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu, Naibu Waziri Hamad Yussuf Masauni na watendaji katika wizara hiyo kwenda kuongeza mapato kwa kutimiza kigezo kilichotolewa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango cha kukusanya Sh trilioni mbili kwa mwezi. Alisema rekodi ya kufanya kazi humfuata mtu katika maisha yake na wengine wamekosa nafasi uwaziri au naibu waziri kutokana na rekodi zao.

“Walisahau kwamba rekodi inamfuata mtu katika maisha yake na mimi nitakuwa na jicho kubwa sana pamoja na kwamba yamelegea lakini yanaona, nitakuwa na jicho kubwa kuangalia rekodi zenu,” alisema Rais Samia.

“Hivi sasa ni wakati Bunge la Bajeti, tukaishughulikie Bajeti ya Serikali, mawaziri lazima muwepo bungeni. Mmoja anapokwama mwingine anasaidia, wala msiachiane kwamba shauri yake. Bila bajeti hatutakuwa na fedha na kuendeleza na serikali, msiachiane,” alisisitiza.

Aliwataka kwenda kufanya kazi kwa ushirikiano kwani ni serikali moja, kwani kila sekta inafanya kazi katika serikali hiyo, hivyo hakuna haja kuvutana kugombana, waende wakakae na kuweka mfumo mzuri wa kufanya kazi pamoja.

“Fanyeni kazi kwa lengo moja la kuwatumikia Watanzania. Sisi ni watumishi wa Watanzania. Nitakuwa na kipimo cha mabega, nikiona mtu anajikweza nitamshusha...,” alisema Rais Samia ambaye aliahidi Jumanne ijayo anatarajia kuapisha wateule wengine.

Rais Samia aliwapongeza wateule wote na walioapa akawataka wakachape kazi. “Nawapongeza tena mawaziri, tumerudi wote na mabadiliko kidogo, katika kuendesha jahazi hili, upepo uwe mwingi au kidogo, jahazi hili linatakiwa kukata mawimbi na safari ipo kwenu,” alisema.

Kuhusu Katibu Mkuu Kiongozi, Rais Samia alisema amechagua jina bila hata kumfahamu sura, lakini alisema, “nilipoulizwa unamjua nikajifu si yule anayefanana na hayati Balozi John Kijazi, mpana mpana hivi, lakini kutokana na kuwa balozi nchini Japan inaonesha kwamba ana uwezo na weledi na utendaji bora na uaminifu wa hali ya juu.”

Alimtaka Balozi Kattanga kwenda kuunganisha makatibu wakuu serikalini kwani hivi sasa muunganiko ndani ya serikali mdogo mno, kila mmoja anasimamia eneo lake. “Ugomvi huo ulioibua wewe mwenyewe ndiye daktari nenda ukasimamie hilo,” alieleza.

Pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi, mawaziri wanane walioapishwa na wizara zao kwenye mabano ni Ummy Mwalimu (Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Profesa Palamagamba Kabudi (Katiba na Sheria), Selemani Jafo (Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira) na Dk Mwigulu (Fedha na Mipango).

Wengine ni Profesa Kitila Mkumbo (Viwanda na Biashara), Geoffrey Mwambe (Ofisi ya Waziri Mkuu –Uwekezaji), Balozi Liberata Mulamula (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki), na Mohamed Mchengerwa (Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora).

Manaibu walioapishwa ni William ole Nasha (Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji), Abdallah Ulega (Mifugo na Uvuvi), Mwita Waitara (Ujenzi na Uchukuzi), Pauline Gekul (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo), Mwanaidi Ali Hamis (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto), Masauni (Fedha na Mipango), Hamad Hassan Chande (Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira) na Mbarouk Nassoro Mbarouk (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki).

Alitaja sababu za kufanya mabadiliko hayo ni kuwapeleka mawaziri na manaibu wao kwenye wizara za sekta walizobobea.

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Maulid Ahmed na Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi