loader
Simba kufa au kupona

Simba kufa au kupona

LEO Jumamosi  wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba, wanashuka kwenye dimba la Benjamin Mkapa kuwakabili AS Vita ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mchezo wa Kundi  A.

Simba wanaingia katika mchezo huo wa marudiano  wakiwa vinara wa kundi hilo, wakiwa na kumbukumbu nzuri ya mchezo wa kwanza ambao waliibuka na ushindi wa bao 1-0, ugenini nchini Congo.

Wawakilishi hao wa Tanzania wanashuka uwanjani leo wakiwa na sapoti ya mashabiki wao 10,000, ambao katika mchezo wa  awali walizuiwa kutokana na tahadhari ya ugonjwa wa corona. Kila shabiki hataruhusiwa kuingia uwanjani kama hajavaa barakoa.

Kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola alisema kuwa wanajua haitakuwa mechi rahisi, lakini wamejipanga kuhakikisha wanashinda ili kujisafishia njia ya kutinga hatua ya robo fainali.

“Tunamshukuru Mungu kikosi chetu kiko kamili hakuna mchezaji ambaye tunaenda kumkosa ingawa utakuwa mchezo mgumu, lakini ili tufike robo fainali tunapaswa kushinda kesho (leo),” alisema Matola.

Naye nahodha wa kikosi cha Simba, John Bocco alisema kuwa kwa maandalizi ambayo wameyafanya wanaamini wataenda kupata matokeo kutokana na morali iliyopo kikosini wanajipanga kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu.

“Najua tulipata matokeo katika mchezo wa mwisho hapa, lakini soka halichezwi kwa historia tunaamini katika maandalizi tuliyoyafanya tangu wiki iliyopita,” alisema Bocco.

Kocha Mkuu wa AS Vita, Florent Ibenge alisema hawaihofii Simba, ingawa anajua utakuwa mchezo mgumu ndio maana mara kadhaa amekuwa akiongea na wachezaji wake wasiogope wafurahie mchezo, kwani wamekuja kusaka pointi tatu ili kuweka hai matumaini yao ya  kufuzu hatua ya robo fainali.

"Tumekuja kucheza, ni mechi ngumu ambayo tutahitaji matokeo iwapo tutapoteza tena itakuwa mwisho wetu sikufurahishwa na matokeo tuliyopata Kinshasa,” alisema Ibenge.

Nahodha wa AS Vita, Nathan Mabruki alisema kuwa wamekuja Tanzania wakijua fika Simba ni timu kubwa Afrika, lakini wamekuja kutafuta pointi tatu ambazo zitatoa mwanga kama watasonga mbele au safari yao itaishia hapo.

“Tumekuja kupambana kuangalia kama tunaweza kushinda hapa kama wao walivyofanya jijini Kinshasa,” alisema Mabruki.

Katika mchezo huo Simba yenye alama 10 kileleni mwa Kundi A juu ya Al Ahly wenye alama saba, inahitaji sare au ushindi ili kufuzu hatua inayofuata ya robo fainali wakati AS Vita iliyoko katika nafasi ya tatu na alama nne unahitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kusonga mbele.

Mchezo wa mwisho hatua ya makundi, Simba itacheza na Al Ahly ugenini huku AS Vita watawakaribisha Al Merrikh nyumbani.

Aidha, Simba imesema kuwa itaondoka nchini mapema kwenda Misri ili kuiwahi Al Ahly katika mchezo wa mwisho wa kukamilisha mechi za makundi utakaofanyika Aprili 9.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/5b33316134c6c3f31390515e68ae14f7.jpg

UMOJA wa Vijana wa Chama ...

foto
Mwandishi: Martin Mazugwa

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi