loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wafanyabiashara wamfurahia Rais Samia

WAFANYABIASHARA nchini wamesema Rais Samia Suluhu Hassan amewapatia zawadi ya Pasaka huku wakibainisha kwamba mazingira ya ulipaji kodi yakiboreshwa kama alivyoagiza, serikali inaweza kukusanya zaidi ya Sh trilioni mbili kwa mwezi.

Kupitia vyombo vyao, wafanyabiashara hao waliozungumza na HabariLEO, wameainisha namna ambavyo serikali inaweza kuongeza wigo wa kukusanya mapato kwa kujielekeza kwenye vyanzo vingine ikiwamo wenye nyumba za kupangisha  badala ya kujielekeza zaidi kwa wafanyabiashara na wafanyakazi.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo amesema wizara yake itakutana na wafanyabiashara muda si mrefu kuzungumza nao kuhusu umuhimu wa kulipa kodi ya serikali.

Washangilia

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta ya Binafsi Tanzania (TPSF), Francis Nanai, alisema agizo la Rais la kutaka mazingira ya ulipaji kodi yaboreshwe, kuzuia kufunga biashara za watu, akaunti za wafanyabiashara au kuchukua fedha zao, kilikuwa kilio cha wafanyabiashara cha siku nyingi.

“Sisi tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais Samia na alichokisema ni zawadi nzuri sana ya Pasaka kwa wafanyabiashara. Tutakula pilau letu, soda zetu na wine (divai) zetu zikishuka kwa amani kwa sababu ametupatia ile kitu ambayo tumeisubiri kwa miaka mingi kuisikia,” alisema Nanai.

Nanai alisema maagizo hayo kwa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Mamlaka ya Kodi (TRA), ndicho kilikuwa kilio wafanyabiashara kwamba masuala ya kodi yanapaswa kuwa shirikishi kwa mantiki kwamba mlipakodi na mkusanya kodi wafanye kazi kwa ushirikiano wa kindugu na urafiki kwa lengo moja la kukusanya mapato.

 

 “Kwa hiyo ushirikiano na mkakati mzuri wa ukusanyaji mapato ambao kama TRA wataamua kufuata kama walimsikiliza vizuri Mheshimiwa Rais, nina imani hata hiyo shilingi trilioni mbili kwa mwezi ni kidogo,” alisema.

Wigo wa kodi

Nanai alisema ipo haja ya kuwapo kwa mkakati wa kurasimisha sekta isiyo rasmi. Alisema vitambulisho vya wamachinga ni hatua moja lakini ipo haja ya kwenda hatua ya pili ya kuwafanya wawe rasmi kwa sababu kwenye sekta hiyo kuna kodi nyingi ya serikali.

“Shida iliyopo sasa hivi ni kwamba ng’ombe ni mmoja na anakamuliwa huyo huyo mpaka anatoa damu, kwa hiyo kama alivyosema Mheshimiwa Rais tuwe wabunifu, tutumie akili na tabia ya kukusanya kodi kimazoea iishe, halafu ubabe hausaidii,” alisisitiza.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA), Gotfrid Muganda, alisema tatizo la wakusanyakodi nchini ni kutokuwa na mkakati wa kutanua wigo wa kukusanya kodi na badala yake wanakamuliwa watu wale wale wakiwamo wafanyabiashara na wafanyakazi.

Alisema ni vema Wizara ya Fedha na Mipango na TRA wakaanza kugeukia vyanzo vingine ambavyo havijawahi kuguswa wakiwemo wamiliki wa nyumba wanaopangisha katika maeneo mbalimbali.

“Ukiangalia uchumi wa nchi hii umekaa kipiramidi yaani walipakodi wachache wako juu na wasiolipa kodi wengi wako chini, kwa hiyo waliopo juu ndiyo wanaonekana kwa haraka na wakusanya kodi wanaona rahisi kuwafikia kukusanya kodi. Kwa hiyo pamoja na kuendelea kukusanya kodi kwa hao walio juu, waongeze vyanzo vingine vya walipa kodi,”alisema Muganda.

Aliongeza, “Kwa mfano kwenye eneo la upangishaji nyumba hawakusanyi kodi, watu wanaoishi kwa kupanga ni wangapi? kwa hiyo kuna haja kwa serikali kuwafanya wenye nyumba siyo tu kulipa kodi ya Sh 10,000 ya majengo lakini pia walipe kodi kwa watu wanaowapangisha.”

Waziri Mkumbo aahidi

Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo alisema wizara yake itakutana na wafanyabiashara muda siyo mrefu ili kuzungumza nao kuhusu umuhimu wa kulipa kodi ya serikali.

Profesa Kitila alisema wizara yake ina wajibu wa kuhakikisha biashara zinalindwa, zinakua na kupanuka kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara mpya kuibuka pamoja na kutoa elimu wafanye biashara zao kwa uhuru, utulivu, kwa haki na kwa kuzingatia sheria za nchi.

“Kwa hiyo lazima tukutane na wafanyabiashara kwa sababu tuna rais mpya na tunapaswa kuwapa mwelekeo wa Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wailewe, na kauli ya juzi Mheshimiwa Rais anataka biashara zikue na ziende vizuri,”alisema Profesa Kitila.

Juzi wakati wa uapisho wa Katibu Mkuu Kiongozi pamoja na Mawaziri Wateule Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Rais Samia aliagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuangalia mbinu mpya ya ukusanyaji mapato kwa kuongeza walipa kodi zaidi kuliko inayotumika ya sasa ambayo inafilisi wafanyabiashara.

Alisema hali hiyo inasababisha wafanyabiashara kufilisika na kufunga biashara zao na wengine kukimbia nje ya nchi kuangalia fursa nyingine za biashara.

 

WATU hutegemea mvua ili kufanikisha shughuli mbalimbali, ikiwamo ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi