loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mwigulu: Rudisheni fedha mlizohamisha

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba (pichani) amewataka wafanyabiashara waliohamisha fedha au kuziweka nyumbani wazirudishe benki.

Aidha amesema kwamba itakachofanya serikali ni kutoza kodi ya sehemu ya makusanyo yao.

Aidha, Mwigulu amewataka watanzania kulipa kodi kwa kuzingatia sheria, kujenga utamaduni wa kulipa kodi na kuachana na ujanja wa kukweka kodi, kwani kila atayakwepa kulipa kodi hatavumiliwa.

Alisema hayo katika kikao kazi na wakuu wa idara mbalimbali katika wizara, idara na Mamlaka ya Mapato (TRA) na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo jijini Dodoma jana.

 

Rudisheni fedha 

“Kwa wale wafanyabiashara ambao walishaaanza kuona nikiwa na fedha yangu ikionekana mtandaoni labda itachukuliwa yote. Nitoe rai warudishe fedha kwenye mabenki, zitaliwa na mchwa na panya bila sababu yoyote. Uchumi wa kisasa si kuweka fedha kwenye maboksi. Kodi itatozwa tu sehemu inayotakiwa kukusanywa,” alisema.

Mwigulu alisema kama wizara lazima kutekeleza kikamilifu ili kila mtu kwenye idara yake atoe kipaumbele na ajipange katika kukuza uchumi na kutengeneza walipa kodi wapya.

Aliwasisitiza kutekeleza agizo la Rais Samia la kutaka wakuze uchumi, wapanue wigo lakini bila kuua walipakodi waliopo.

Waziri Mwigulu alisema TRA wanatakiwa kutumia weledi badala ya nguvu katika kukusanya kodi ili kutoua biashara na kutopunguza walipakodi.

Alisema TRA wanatakiwa kuhakikisha wanatoza kodi na hawachukui fedha zote za wafanyabiashara.

“Tuchukue kinachotakiwa kutozwa na siyo fedha zote za wafanyabiashara, tutoze kodi ambayo ni sehemu ya mapato kwa asilimia au kiwango kiichowekwa,” alisema Mwigulu.

Alitaka mamlaka hiyo ya kodi kuacha mtindo wa kufanya ukadiriaji wa kodi usiozingatia sheria na taratibu, ambao unachangia katika kuua vyanzo vya mapato na kupunguza walipakodi pamoja na kuua shughuli zao.

Alisema kumekuwa na mijadala hasa bungeni wakilalamikia vitendo vya ukadiriaji wa mapato ambao hauzingatii sheria na weledi, hivyo akawataka TRA kuachana na maeneo au matendo yanayoleta mkanganyiko katika ukusanyaji wa kodi.

Aliwasisitiza kuachana na mambo yanayosababisha wafanyabiashara kufunga biashara zao.

“Mnatakiwa kuwalinda walipakodi waliopo, kurekebisha upungufu na kurudi kwenye mstari bila kuua vyanzo vya mapato ya serikali na shughuli za wafanyabiashara.

“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni muhimu yatekelezwe ipasavyo ili kulinda na kukuza uchumi wa nchi kwa kutoza kodi kwa staha, weledi na kwa mujibu wa Sheria na turekebishe mahali tulipoharibu”alisisitiza Dk Nchemba.

Aliitaka TRA kuacha kudai taarifa za miaka mingi ya nyuma ambayo iko nje ya sheria kwa wafanyabiashara ambazo zilikwishafanyiwa kazi, kwani utunzaji wa kumbukumbu ni changamoto kwa wengi hivyo ni vema kuzingatia sheria na taratibu za namna ya kufanya ukadiriaji wa kodi.

“TRA nawataka mpeleke ujumbe makini kwa wafanyakazi wa TRA nchini nzima kwamba Serikali haijasema msikusanye kodi au mpunguze jitihada za kukusanya kodi hizo bali kinachoongelewa na kusisitizwa ni kukadiria na kukusanya kodi kwa kuzingatia sheria na taratibu, bila kuonea watu”alisisitiza Dk Nchemba.

Wakwepa kodi kutovumiliwa 

Mwigulu aliwataka pia watanzania kulipa kodi kwa kuzingatia sheria, kujenga utamaduni wa kulipa kodi na kuachana na ujanja ujanja wa kukweka kodi, kwani yeyote atayakwepa kulipa kodi hatavumiliwa.

“Watanzania mnatakiwa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria, msikwepe kodi, kwani mahali popote duniani ustaraabu wa mtu unapimwa namna anavyolipa kodi. Pia mtu anapotazamwa katika jambo kubwa anaangaliwa kama ni mlipa kodi,” alisema.

Alisema TRA wanatakiwa kupunguza utaratibu wa kulipa fedha mkono kwa mkono, bali zilipwe kwa kutumia mashine za kieletroniki kupitia mifumo iliyopo ijapokuwa baadaye itafanyiwa maboresho ili kuwa na mifumo bora.

Mwigulu alisema hatua itakayofuata katika wizara itakuwa kuangalia mifumo mbalimbali ya ukusanyaji kodi ili kubaini iliyo bora kumjenga imani mlipa kodi kwamba imetumika katika kuleta maendeleo ya nchi.

Aliwaonya watumishi wanaobadili maelekezo na kuwatisha wafanyabiashara kuhusu ulipaji kodi .

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Yusufu Masauni akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri alisema kwamba wapo tayari kutimiza malengo yaliyotolewa na Rais Samia 

wakati wa kupokea taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na wakati wa kuapishwa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango na mawaziri.

Alisema wapo hapo kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kufikia malengo na hana wasiwasi katika hilo. Alisema pia wanaangalia hatua iliyofikiwa ili waendeleze kwa kasi zaidi. Katika hafla tatu tofauti; ya kupokea taarifa ya CAG na Takukuru, kuapisha Makamu wa Rais, Dk Mpango na kuapisha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Katanga, mawaziri wanane na naibu mawaziri wanane, Samia alisema mwenendo wa sasa wa ukusanyaji kodi ni wa kuua walipa kodi. 

Alisema TRA wanatumia nguvu zaidi kuliko kutumia akili na maarifa. 

“Wale mnaowakamua, kuchukua vifaa vyao, kufungia akaunti zao na kisha kukiuka sheria ya mapato, anafunga biashara anahamia nchi nyingine, mnapunguza walipa kodi,” alisema.

Alimwagiza Waziri Mwigulu kutengeneza na kutanua wigo wa walipakodi na kuondoa mambo yanayowapunguzia watu ari ya kulipa kodi. Alitaka wizara hiyo kukusanya mapato makubwa ili kukuza uchumi.

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi