loader
Gomes: Nitabeba makombe yote

Gomes: Nitabeba makombe yote

KOCHA Mkuu wa klabu ya Simba, Didier Gomes amesema amefurahishwa na ushindi mnono wa timu yake dhidi ya AS Vita katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini zaidi anashukuru kutimiza malengo ya timu hiyo.

Aidha, Gomes amesema anataka kufika nusu fainali za michuano hiyo lakini pia anataka kutetea taji la Ligi Kuu Bara na lile la  Shirikisho la Azam, FA.

Simba imefuzu hatua ya robo ya fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa juzi.

Gomes alisema alipofika Simba moja ya jukumu alilopewa ni kufuzu robo fainali hivyo ana shukuru jambo hilo limefanikiwa na sasa anakusanya nguvu kwenye kufuzu nusu fainali za michuano hiyo mikubwa ngazi ya klabu Afrika.

Simba sasa imebakiza mchezo wa mwisho dhidi ya Al Ahly ya Misri, mchezo wa kukamilisha ratiba kwani hata Ahly imefuzu pia robo fainali. Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa mwishoni mwa wiki hii mjini Cairo.

Akizungumza baada ya mchezo wa juzi, Gomes alisema anafuraha sio kwa kufuzu bali kutokana na ushindi mkubwa walioupata ambao umekuwa tiketi ya wao kuingia hatua ya robo fainali wakiwa vinara wa kundi A. Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 13 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye kundi lake.

“Nimejisikia vizuri kutokana na ubora wa wachezaji wangu wamefuata maelekezo yangu vizuri walikuwa wastahimilivu, AS Vita walitupa presha sana ilikuwa mechi nzuri, tulicheza na timu bora  Afrika.”

“Wakati nakabidhiwa timu , jukumu langu la kwanza lilikuwa kuhakikisha timu inaingia robo fainali, Namshukuru Mungu, viongozi, wachezaji wangu na wadau wote wa Simba kuniwezesha kutimiza jukumu hilo.” 

“Sasa tunakwenda katika majukumu ya kimkakati kuhakikisha tunaingia hatua ya nusu fainali klabu bingwa Afrika, ubingwa Ligi Kuu na FA.”

“Hivi sasa Simba imekuwa miongoni mwa timu nane kubwa  Afrika, ni jambo la furaha kwetu  lakini pia tutakuwa na wiki ya kufikiri tunaenda kufanya nini dhidi ya Al Ahly jijini Cairo,” alisema Gomes.

Naye kocha mkuu wa klabu ya AS Vita, Florent Ibenge alisema amefungwa na timu bora Afrika ambayo ina uwekezaji mkubwa kuliko wao ndio sababu ya wao kupoteza mchezo huo ambao umefifisha matumaini yao ya kufuzu hatua ya robo fainali.

“Mpira unaendeshwa na fedha timu za Tanzania zinatumia fedha nyingi hivi sasa  ndio maana wachezaji wengi wanaondoka nchini Congo  na kuja huku.”

“Wachezaji wazuri wanatoka Congo wanakuja huku  ndio maana unaona timu za Tanzania zimekuwa na wachezaji  wazuri  na timu zao zinafanya vizuri,”  alisema Ibenge.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e394c0d194ca70cac2d16c6f3403ce63.jpeg

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewapongeza wachezaji ...

foto
Mwandishi: Martin Mazugwa

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi