loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mpango akemea wabadhirifu

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amewataka watumishi wa serikali ambao ni wabadhirifu wa mali za umma wafufuke na Kristo kwa kufanya kazi kwa uadilifu sambamba na kuwa na kiu ya kuwatumikia Watanzania bila kujali maslahi binafsi.

Dk Mpango pia jana aliwaagiza watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wawaache wafanyabiashara wafanye biashara kwa uhuru kwa sababu yeye anahitaji kodi zitakazotumika kuboresha maisha ya Watanzania wanyonge na kuleta maendeleo ya taifa.
Aliyasema hayo katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Kuu la Dodoma baada ya Paroko wa kanisa hilo, Padri Onesmo Wisi kumkaribisha azungumze na waumini waliohudhuria Ibada ya Pasaka.

"Ikiwa leo tunaadhimisha siku ya ufufuko wa Yesu Kristo, nawaagiza watumishi wa umma wale wabadhirifu nao wafufuke na Kristo ili waache vitendo vya ubadhilifu.”

“Kama Padri alivyosema Hayati Rais Dk John Magufuli kiwiliwili chake ndicho kimekufa, lakini matendo yake tunayaishi vivyo hivyo watumishi na Watanzania kwa jumla tumuenzi kwa kuyaishi yale mazuri aliyotuachia ikiwemo kufanya kazi kwa bidii," alisema Dk Mpango.

Makamu wa Rais alisema taifa linahitaji watumishi wanaofanya kazi kiadilifu ili kuleta maendeleo ya taifa na kuiinua nchi kiuchumi kama alivyofanya Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli wakati wa uhai wake.

Akizungumzia kipindi cha kwaresima, Makamu wa Rais alisema: "Tumetumia siku 40 kujiandaa kiroho, hivyo tuendeleze matendo mema tuliyotenda katika kipindi cha Kwaresma ili tuishi katika uadilifu kama Maandiko yanavyosema."

Aidha, Dk Mpango aliwataka Wakristo na Watanzania kwa jumla kuendelea kumshukuru Mungu huku wakikumbuka na kuzingatia kuwasaidia wasiojiweza na wahitaji mbalimbali ili nao washerehekee Pasaka kwa kumtukuze Mungu.

"Tuliobakia tunao wajibu wa kuishi yale aliyotuachia Hayati Rais Dk Magufuli huku tukimtanguliza Mungu kwa kila jambo," alisema.

Dk Mpango aliwaomba Watanzania wamwombee kwa Mungu Rais Mpya wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa sababu kazi mpya aliyokabidhiwa ya kuliongoza taifa si nyepesi.

 “Kila akifikiria watu milioni 60 wanamtazama yeye na ukizingatia taifa la wanyonge linahitaji kupiga hatua mbele kimaendeleo,...”

"Tunaomba Watanzania wa dini zote tumuombee Rais Samia Hassan aweze na
serikali nzima kwa jumla ili atembee katika njia ambazo Mwenyezi Mungu anapenda kwa taifa lake Tanzania lifikie," alisema Dk Mpango.

"Nami naomba mniombee sana ili niwe Makamu wa Rais mwaminifu, ninayeangalia haki za wanyonge wanaodhulumiwa katika nchi yetu, msiniache peke yangu," alisema.
Alisema anajua Watanzania wengi sana walimuombea sana wakati akiugua,na walifanya hivyo akaweza kutoka bila shaka mwenyezi Mungu alitaka afanye kazi yake ambayo hakujua  ni kazi gani lakini huenda ni hiyo  aliyokabidhiwa hivi sasa.


"Tunaomba Watanzania muendelee kuiombea serikali na Watanzania kwa ujumla ili tufikie malengo ambayo yalikusudiwa na Hayati Rais Dk Magufuli na serikali yake ambayo ipo madarakani,"alisema Dk Mpango.
Akizungumzia kuhusu TRA, Dk Mpango alisema watumishi wa sekta hiyo wanapaswa kufanya kazi kwa kufuata sheria na si kwa vitisho kwa wafanyabiashara, kwa sababu serikali inahitaji kodi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi.
Mbali na hilo, alitoa salamu za Rais Samia Suluhu kwa waumini wote na Watanzania kwa jumla akiwatakia Pasaka njema na kusheherekea kwa amani huku wakiliombea taifa
Paroko Wisi alimpongeza Dk Mpango kwa kuwa mwanajimbo wa Kanisa Katoliki la Paulo wa Msalaba.

Alimuomba awafikishie salamu za pongezi kwa vyombo vya ulinzi na usalama kutokana na kazi nzuri ya kulinda usalama vinayoifanya hususani katika kipindi hiki.
"Tunavishukuru vyombo vya ulinzi na usalama nafasi yao na kazi yao tumeiona katika kipindi hiki na tunaendelea kuiona; nasi kama Wakatoliki na Watanzania kwa jumla, tunaendelea kumwombea Rais na serikali yake ili wafanye kazi iliyotukuka," alisema Padri Wisi.

Alitoa salamu za pongezi za Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma, Beatus Kinyaiya kwa serikali na waumini huku akiwataka kusherekea Pasaka kwa amani na utulivu.
"Tunashukuru serikali kwa salamu za Pasaka, kutoka kwa Rais Samia
Suluhu, kwa niaba ya Parokia ya Jimbo Kuu, tunakuhakikishia hayo
uliyosema tutayaishi na tunaendelea kuwaombea ili muendelee kutumikia
taifa hili kwa weledi," alisema Wisi.

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi