loader
Dstv Habarileo  Mobile
SIKU YA UHURU WA DHAMIRI:  Tuvumiliane ili kudumisha amani na upendo kwa jamii

SIKU YA UHURU WA DHAMIRI: Tuvumiliane ili kudumisha amani na upendo kwa jamii

LEO Aprili 5 ni Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Dhamiri. Wengi wanakubali kwamba uhuru wa dhamiri ni mojawapo kati ya haki za msingi za binadamu.

Maadhimisho ya siku hii ya kimataifa ya uhuru wa dhamiri ya mwaka huu ni ya pili kwa Jumuiya ya Kimataifa kuyaadhimisha. Katika historia ya jumuiya hiyo, wazo la kuadhimisha siku ya kimataifa ya uhuru wa dhamiri lilitolewa tarehe 25 Julai 2019 kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa. 

Na kwa mara ya kwanza siku hii iliadhimishwa tarehe 5 Aprili 2020, kwa kutafakari kuhusu amani duniani na kwa kuzingatia uhuru wa dhamiri na uwajibikaji kwa ajili ya mafao mapana zaidi ya binadamu. 

Pia inalenga kusikiliza na kujibu kilio cha Mama Dunia na masikini, ili kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto zinazoibuliwa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hii ni siku ambayo inapata chimbuko lake kutoka kwenye ushuhuda wa Aristed de Sousa Mendes, mwanadiplomasia kutoka Hispania. 

Alifuata dhamiri nyofu, akasimama kidete kulinda, kutetea na kuokoa maisha ya maelfu ya Wayahudi na wale wote waliokuwa wanateswa na kunyanyaswa.

Kwa tafsiri rahisi, dhamiri ni hukumu ya akili ambamo mwanadamu hutambua sifa adilifu ya tendo halisi analoelekea kulitenda, angali akilifanya au amekwisha kulitekeleza. Katika yote asemayo na atendayo, mwanadamu hana budi kufuata kiaminifu anachojua kuwa ni haki na sahihi. 

Mwanadamu hufahamu na kutambua maagizo ya sheria ya Mungu kwa hukumu ya dhamiri yake. Hadhi ya binadamu yadokeza na kudai unyofu wa dhamiri adilifu.

Pia dhamiri ni kipawa cha binadamu kinachomwezesha kuamua kuhusu uadilifu au uovu wa tendo fulani analolikabili au alilolitenda. 

Ndiyo sababu mtu hatakiwi kulazimishwa kwenda kinyume cha moyo unavyomtuma, hata kama wengine wengi wanafanya tofauti. Dhamiri hiyohiyo inamsukuma daima kutenda lililo adilifu na kukwepa lililo ovu.

Katika falsafa ya maadili wengi wanakubali kwamba uamuzi wa dhamiri unategemea ukweli ambao upo nje ya mhusika na ambao yeye anatakiwa kuutambua.

Baadhi ya wataalamu wa elimunafsia wanashikilia msimamo kuwa uamuzi wa dhamiri unategemea zaidi malezi na mang’amuzi ya mtu.

Hakuna mtu wa jana, leo au kesho aliye sawasawa na mwingine: kila mmoja ni wa pekee. Mungu ametufanya kuwa tofauti ili tutimilizane. Kila mmoja anawahitaji watu wengine, na kila mmoja ni muhimu kwa wenzake. Katika shirika, kwa mfano, mlinzi ana umuhimu wake, mfagiaji, karani hadi meneja. Wote wanahitajiana.

Katika maisha ya jamii kuna sehemu ambayo ni yeye tu anaweza kuijaza. Wazo hilo linaweza kumsaidia kijana ambaye ni mwepesi kukata tamaa na kujitupa. 

Uhai ni zawadi nzuri kwa mhusika na kwa wenzake wote. Kijana ni zawadi yenye nguvu na wema hata kwa taifa, kiasi kwamba kujali ustawi wa kijana ni kujenga taifa.

Mwanadamu anayo sheria moyoni mwake iliyoandikwa na Mwenyezi Mungu. Dhamiri yake ndiyo kiini cha ndani sana na siri kubwa ya mwanadamu, ndipo sehemu muhimu ambamo yumo peke yake pamoja na Mwenyezi Mungu; ambamo sauti yake inasikika. 

Dhamiri adilifu iliyo moyoni mwa mtu huamuru, kwa wakati ufaao, kutenda mema na kuepuka mabaya. Huchagua pia upande mmoja, ikithibitisha upande ulio mzuri na kulaumu ule mbaya. 

Na kwa njia hii, jamii inawajibika na kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. 

Ni wakati wa kuamsha dhamiri zilizolala au kusinzia kwa kusimama kidete ili kutokubali mtu kuchezea dhamiri yako. Ni wakati wa kuwajibika barabara kwa kuzingatia dhamiri nyofu ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu. 

Utangulizi wa Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu unasema kwamba “kukiri heshima ya asili na haki sawa kwa binadamu wote ndiyo msingi wa uhuru, haki na amani duniani, kutojali na kudharau haki za binadamu kumeletea vitendo vya kishenzi ambavyo vimeharibu dhamiri ya binadamu na kwa sababu taarifa ya ulimwengu ambayo itawafanya binadamu wafurahie uhuru wao wa kusema, kusadiki na wa kutoogopa chochote imekwisha kutangazwa kwamba ndiyo hamu kuu ya watu wote…” 

Kwa kuongezea, kifungu cha 1 cha Azimio hilo kinasema kwamba “Watu wote wamezaliwa huru, hadhi na haki zao ni sawa. Wote wamejaliwa akili na dhamiri, hivyo yapasa watendeane kindugu.”

Hata hivyo, kazi ya Umoja wa Mataifa kuokoa vizazi vijavyo kutokana na janga la vita inahitaji mabadiliko kuelekea utamaduni wa amani, ambao una maadili, mitazamo na tabia ambazo zinaonesha na kuhamasisha mwingiliano wa kijamii na kushiriki kwa kuzingatia kanuni za uhuru, haki na demokrasia, haki zote za kibinadamu, uvumilivu na mshikamano.

jambo hili ni muhimu katika kukataa vurugu na kujitahidi kuzuia mizozo kwa kushughulikia sababu za msingi za kutatua shida kupitia mazungumzo na makubaliano ambayo yanahakikisha utekelezaji kamili wa haki zote na njia za kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo ya jamii yao.

Pia kazi nyingine ni kutambua hitaji la kuundwa kwa hali ya utulivu na ustawi na uhusiano wa amani na urafiki unaotegemea heshima ya haki za binadamu na uhuru wa kimsingi kwa wote bila ubaguzi wa rangi, jinsia, lugha au dini. 

Ndiyo maana Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa uliitangaza tarehe 5 Aprili kuwa siku ya kimataifa ya uhuru wa dhamiri.

Mkutano Mkuu ulialika nchi zote wanachama, mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa na ya kikanda, sekta binafsi na asasi za kiraia, pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi.

Mwaliko huo ulizingatia kujenga utamaduni wa amani, upendo na dhamiri kulingana na utamaduni na mazingira mengine yanayofaa au mila ya jamii zao za kieneo, kitaifa na kikanda, ikiwa ni pamoja na kupitia elimu bora na shughuli za kuhamasisha umma, na hivyo kukuza maendeleo endelevu.

Kwa maana hiyo, tunapaswa kuvumiliana kwa sababu kila mmoja ni wa pekee na Mungu ametuumba kuwa tofauti ili tutimilizane.

0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/d4f53f791a7b7170ad46699bb48f607e.png

WAFUGAJI wa ng'ombe wa maziwa nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka 

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi